KIFO CHA GADDAFI: Watawala Afrika wamejifunza nini?


Profesa Abdallah Saffari's picture

Na Profesa Abdalla... - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version

PICHA iliyomuonyesha kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kavuliwa shati, kabaki na suruali bila viatu; huku kichwa na kifua chake vikiwa vimejaa michirizi ya damu kutokana na majeraha ya  risasi na kipigo alichokipata kutoka kwa waasi wa Libya, imenikumbusha mengi.

Kwamba kiongozi wa Afrika kukutwa na mauti kama haya, ni jambo la kawaida. Katika kitabu Association of Patrice Lumumba (yaani kuuawa kwa Patrice Lumumba), mwandishi mashuhuri Ludo De Wittke, amesema kwa ufasaha na simanzi sura inayoelezea siku na saa ya mwisho ya kuuawa kwa Patrice Lumumba.

Lumumba alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Jamuhuri ya Kongo, aliyechaguliwa na Wakongomani katika uchaguzi halali wa demokrasia wa vyama vingi, miezi sita tu kabla ya kuuawa kwake. 

Kuuawa kwa Kanal Gaddafi kumezua mitazamo miwili mikubwa: Wapo wanaompinga na kufurahia kifo chake, na wapo wale wanaomkubali na kuomboleza kifo chake. 

Madai makubwa ya wanaompinga ni matano:  Kwamba alikaa sana madarakani; hakufanya uchaguzi wa kidemokrasia; alitawala kwa mabavu; alichezea utajiri wa Libya na alikuwa anaandaa watoto wake kuchukua madaraka ya urais.

Ni kweli kuwa Gaddafi alikaa sana madarakani. Lakini hayuko peke yake Afrika na duniani kwa jumla. Uingereza ina Malkia hadi leo ambaye yeye na genge la familia yake wanakula bure fedha za wavuja jasho wa nchi hiyo.  Hali hiyo ipo pia kwenye nchi nyingine za Ulaya zenye ufalme ikiwamo Hispania, Norway na Sweden.

Ndivyo ilivyo pia kwa Saudi Arabia-kipenzi cha Marekani ambayo inachota mafuta ya dezo na kuweka vituo vya kijeshi inavyotaka. Urusi na Uchina hakuna demokrasia ambayo inazingatia misingi ya haki za binadamu.  

Kuhusu kutofanya uchaguzi, nchi nyingi duniani haziendeshi chaguzi kabisa au zinaendesha chaguzi feki zisizozingatia masharti ya sheria za kimataifa.

Ndiyo maana Umoja wa Afrika hauthubutu kukemea chaguzi bandia Afrika kwa vile ukiachia Ghana na Afrika Kusini, chaguzi nyingine nyingi hazikidhi misingi ya sheria za kimataifa kutokana na kutokuwapo kwa tume huru ya uchaguzi. 

Madai ya utawala wa mabavu sio mageni kutolewa na nchi za Magharibi kwa viongozi wasiowapenda duniani.  Rais Mobutu wa Congo, aliyeshiriki kumuua Patrice Lumba akitumiwa na Wamarekani na Wabelgiji, alitawala kwa mabavu. Lakini alibaki kipenzi cha Wamarekani na Wazungu hadi alipoondolewa madarakani kwa nguvu ya umma baada ya miaka mingi!

Rais halali wa Chile, Salvador Allende aliuawa na washirika wa Marekani na badala yake akasimikwa dikteta Augusto Pinnochet ambaye alikaa madarakani kwa miaka mingi sana kinyume na ridhaa ya watu wa Chile.

Dk. Kwame Nkrumah, rais wa kwanza  na kipenzi cha watu wa Ghana, na mwanasiasa mashuhuri wa Karne Afrika – kwa  mujibu wa utafiti wa BBC -  aling’olewa  madarakani na mabeberu wa kizungu kutokana na msimamo wake imara kupinga ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo.

Jenerali Murtala Mumhamad, kiongozi shupavu wa Nigeri , inadaiwa aliuawa kwa ushirika wa wazungu kupinga ukoloni nchini Nigeria. 

Sio viongozi tu!  Hata wanamageuzi wa kweli wameandamwa.  Mfano mzuri ni Dk. Ernesto Ghe Guevara.  Baada ya kuiisaidia Cuba kung’oa utawala wa  Batista, (ghe Guevara, raia wa Argentina, alikwenda Congo kushiriki mapambano dhidi ya kibaraka wa Marekani, Mobutu. 

Lakini alipoona Wakongo hawakuwa na msimamo thabiti alikwenda Bolivia, Amerika Kusini, kusaidia watu wa huko kujikomboa ambako Marekani ilimkamata, kumtesa na kumuua. 

Inadaiwa walikata viganja vyake na kumtumia sahibu yake kipenzi, Rais wa Cuba, Fidel Castro.  Sasa Bolvia inaongozwa na rais shupavu, Envo Morales anayetetea maslahi ya watu wake kwa vitendo, sio maneno.

Wengine ni Dedan Kimathi, Jemadari wa wapigania uhuru wa Kenya, aliyenyongwa na serikali ya kikoloni ya Uingereza, wakati akigombea ukombozi wa nchi yake.  Hadi leo hii, haijulikani amezikwa sehemu gani! 

Lakini Marekani inawadhamini waasi wa Afrika, kama ilivyokuwa kwa Dk. Jonas Savimbi wa Angola kuipinga serikali ya nchi yake.  Inafanya hivyo pia Amerika Kusini.

Na kama ni kutumia mabavu, Israel inaongoza kwa kupigiwa kura nyingi na umoja wa mataifa kwa kuwaua, kuwanyanyasa na kuwatesa Wapalestina.  Lakini hadi leo, Israeli ndiyo mshirika mkubwa wa Marekani na umoja wa NATO.  Wala haijawahi kuwekewa vikwazo vya uchumi kama Libya. 

Rais George Bush, aliyekuwa Rais wa Marekani na Tony Blair, aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza walivamia Iraq, kuipiga na kuua malaki ya watu bila idhini ya umoja wa mataifa. Kwa kifupi vita dhidi ya Irag vilikuwa batili. 

Kwa hiyo, ilitosha kumkamata Bush na Blair. Kuwashtaki kama wahalifu wa kivita kama walivyofanyiwa Rais Slobodan Milsosovic wa Serbia, waziri mkuu wa Bosnia Karadic na Jemadari wake Mladic, Charles Taylor wa Liberia na Jean Pierr Bemba wa Congo. 

Sasa wanataka kumkamata Omar Bashir, Rais wa Sudan ya Kaskazini.  Lakini ndiyo kwanza Blair amepewa cheo cha msuluhishi wa mashariki ya kati, wakati Bush akiendelea kutesa na pesa alizozipata wakati wa utawala wake.  Alipotembea Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, alisema kwa uchungu kuwa yeye asingeruhusu hata ndege yake kuruka juu ya anga ya Afrika Kusini kwa kuwa mikono ya Bush ilichuruzika damu na kwamba alikuwa mwovu kuliko Dikteta Adolf Hitler wa Ujerumani.

Kuhusu kuchezea utajiri wa Libya hamna ushahidi madhubuti mintarafu juu ya jambo hili.  Hata wapinzani wa Dk. Kwame Nkrumah walimsingizia kwa madai kama haya wakati ambapo alitegemea mirabaha ya vitabu vyake tu. Ila lililo wazi kwa ushahidi duniani yanaelezea ufanisi mkubwa wa Gaddafi katika kuendeleza Libya.

Kuna mashirika mengi ya habari katika nyanja zote tangu mapinduzi dhidi ya mfalme Idris mwaka 1969.  Kwa mujibu wa taarifa hizo, raia wa Libya waliishi maisha bora zaidi kuliko raia wengi wa Marekani, ufaransa, Uingereza na Italia nchi ambazo zilikuwa mstari wa mbele kumng’oa Gaddafi madarakani. 

Italia na Ufaransa zinanuka madeni wakati Libya haidaiwi hata ndururu!  Kwa kukosa majibu ya ukweli huu, wapinzani wa Gaddafi hugeuza kauli na kudai kuwa, “mwanadamu haishi kwa mkate na siagi tu!” Sharti ashiriki katika serikali ya nchi yake. 

Kwa hiyo wanamponda Gaddafi kwa kutaka kurithisha utawala wake kwa mwanaye, hawawezi kujibu swali hili: Nani amesalimika katika jambo hili duniani, Afrika na hata Tanzania? 

Ubadhirifu wa mali katika bara hili imekuwa bidaa. Nchi zote zinanuka kashfa baada ya kashfa za ufisadi kuanzia Mashariki hadi Magharibi, Kusini hadi Kaskazini. 

Kiongozi mmoja wa Afrika Mashariki alikiri kutumia ndege ya serikali kumpeleka binti yake kujifungua Ujerumani.

Kwa upande mwingine, wapo wanaoamini Gaddafi ameponzwa na uzalendo katika kutetea maslahi ya watu wake. 

Hivyo bara la Afrika sharti liamke kusaka viongozi thabiti hivi sasa. Kilichompoza Gaddafi ni kuamini ugomvi wake na Marekani na Ulaya umekwisha!  Kinachowatia wengi mashaka ni kwamba inawezekana wakatokea watu watakaotaka kulipiliza kisasi cha kuawa kwa Kanali Gaddafi. Hilo likitokea Libya yaweza kugeuka Iraq.

0754 – 262623
0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)