Kifo cha Osama, mwisho wa ugaidi?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Osama Bin Laden

MTUHUMIWA namba moja wa ugaidi duniani, Osama Bin Laden hayuko tena nasi. Ameuawa kwa makombora ya majeshi ya Marekani katika viunga vya Pakistan, alfajiri ya Jumatatu 2 Mei 2011.

Kama ilivyo kwa kipanga anavyomshukia kifaranga cha kuku na kumkuta hajajiandaa, kukwapuliwa kwa kucha kali zisizoachilia, ndivyo majeshi ya Marekani yalivyokatisha mauti ya Bin Laden.

Katika kile ambacho wachambuzi wa kijeshi wanaita “operesheni fungakazi,” Osama Bin Laden gaidi ambaye baadhi ya wafuasi wake waliua Watanzania 11 na kujeruhi wengine zaidi ya themanini, 7 Agosti 1998 baada ya kulipua ofisi za ubalozi wa Marekani, jijini Dar es Salaam amemaliza maisha yake hapa duniani kwa kujiandikia historia ya aina yake.

Osama hakuwa na nafasi ya kukwepa hukumu ambayo hatia yake aliithibitisha yeye mwenyewe kwa kukiri kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyoushtua ulimwengu ya 11 Septemba 2001 huko New York na miji mingine ambapo watu takribani elfu tatu kutoka mataifa kadhaa ulimwenguni, walipoteza maisha yao kwa kuuawa kwa kosa ambalo hawakulijua.

Shtukizo la hukumu ambayo Osama na watendaji wake waliipitisha kwa Wamarekani siku ile na kwa Watanzania miaka mitatu hivi nyuma yake, ndivyo hivyo hivyo Osama alishtukizwa. Pamoja na jitiahada za kurushiana risasi na makomandoo wa ngazi ya juu kabisa katika majeshi ya Marekani, Osama na walinzi wake waliuawa bila ya shaka wakijua hukumu hiyo ilipitishwa dhidi yao kwa makosa gani.

Hawakufa kama mashahidi. Osama siyo shahidi. Ni muuaji ambaye unyama wake ulifanywa kwa jina la dini na kwa kiasi kikubwa alikuwa mchonganishi wa kidini na kitamaduni kati ya nchi za Kimagharibi ambazo nyingi zina Wakristo wengi na jamii ya waamini wa dini ya Kiislamu pote duniani.

Kutokana na vitendo vyake, alisababisha Waislamu wasio na hatia sehemu mbalimbali duniani na hasa huko Marekani kuishi kwa kushukiwa na kuwalazimisha mara kwa mara kuonesha uzalendo wao.

Hakuwa shahidi kwa sababu pamoja na kutumia maandiko ya kidini kuhalalisha uhalifu wake, Osama hakuwa chochote zaidi ya mhalifu wa kimataifa ambaye alitumia dini kama kiinimacho cha kumwaga damu za maelfu wasio na hatia na wale wasio mkosea yeye kwa namna yoyote ile.

Kwa wengi wetu ambao tunakumbuka tukio la Agosti 7, 1998 katika ardhi yetu ambalo liliingiza Tanzania kama mhanga wa uhalifu wa Osama, habari za kunyamazishwa milele kwa mhalifu huyo zinakuja na kupokelewa kwa furaha.

Wapo wale ambao watatoa hoja kuwa kwanini wasingemkamata na kumfikisha mahakamani, lakini ukweli na kama ambavyo tumesikia siku hizi chache Wamarekani ambao waliapa tangu siku ile iliyojaa hofu kuwa “wangemletea haki au kumpelekea haki huko aliko” hawakuwa na nia wala mpango wa kumpatia jukwaa la kueneza propaganda zake za vitisho katika mahakama za Kimarekani. Mpango ulikuwa ni kumfunga mdomo moja kwa moja.

Lakini vile vile Osama hakuwa mtu wa kujisalimisha. Ndio maana walinzi wake walikuwa tayari kupambana na makomandoo lakini kwa mtu yeyote anayejua utendaji kazi wa vikosi vya Wamarekani haviendi kwenye mapambano wepesi wepesi; huenda wakiwa full nondo!

Hivyo, mauaji ya Osama ni hitimisho la ukurasa uliokuwa wazi wa kumbukumbu za majonzi ya maelfu ya watu waliokufa kutokana na sera za siasa zake za vitisho ambazo tunaziita ni ugaidi. Ugaidi ni matumizi ya vitisho na nguvu ili kulazimisha matokeo ya kisiasa yanayotakiwa. Ni wazi wapo wengine ambao watasema “ugaidi kwa mtu mmoja kwa wengine ni harakati za ukombozi.”

Nitawaachia wengine wajadiliane juu ya hilo lakini kwangu binafsi ninaelewa ya kuwa kama Mtanzania ninashukuru kwamba aliyejitangaza ni adui yetu kwa kuwashambulia watu wetu, hatimaye haki imemfikia.

Ndugu zangu, sisi hatukuwa na bado hatuna uwezo wa kukabiliana na watu ambao ni tishio kwetu kama kina Osama. Hatukuwa na bado hatuna uwezo wa kutenga na kuandaa mpango usiokuwa na muda wa kukoma wa kuwafikia maadui wetu popote pale duniani.

Japo tulijua nani aliwaua Watanzania wenzetu, bado hatukuwa na jinsi ya kuweza kutuma Jeshi la Wananchi Tanzanuia (JWTZ) kwenda Tora Bora au Pakistani kumsaka mhalifu huyo.

Tulibakia kutegemea uwezo wa marafiki zetu ambao wana nyenzo na zana za kuweza kumfikia mtu yeyote wamtakaye. Sote tumeshuhudia tangu kukamatwa kwa Sadam Hussein, kukamatwa kwa Khaled Sheikh Muhammed na sasa kuuawa kwa Osama kunathibitisha kuwa marafiki zetu wana uwezo huo na sisi hatuna budi kuwashukuru.

Hili libakie kuwa somo kwa wale wote ambao wanafikiri kushambulia nchi ndogo kama ya kwetu basi hawatajibiwa. Liwe somo kwa wale wote wenye kutukuza ugaidi kwa sababu yoyote ile kuwa katika ulimwengu uliostaarabika vitisho vya nguvu na umwagikaji damu havina nafasi tena. Ugaidi umepata pigo ambalo lilichelewa kuufikia. Kwa hili hatuna budi kushukuru uongozi shupavu wa Rais Barack Obama.

0
No votes yet