Kifo cha polisi Suzana Kabanza


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Darasa elekezi kwa wanaochunguzaa

KUNA kila sababu ya kujenga mashaka juu ya mazingira ambamo kilitokea kifo cha polisi Suzana Taabu Kabanza (WP 7338).

Msichana mdogo wa miaka 22, aliyekuwa ametoka mafunzo ya awali ya uaskari, anadaiwa kujiua akiwa kwenye eneo la kituo cha polisi cha Boma, mjini Tarime, mkoani Mara.

Kumekuwa na ndimi nyingi: Alipotosha msafara wa Rais Jakaya Kikwete. Alitishwa na wakuu wake kazini. Aliogopa. Alijiua akiwa kaunta ya polisi. Aliswekwa rumande. Alijifungia ofisini. Alijiua akiwa ndani ya ofisi ya kamanda wa polisi. Alijipiga risasi tatu. Mengi, mengi tu.

Ni kauli zinazokinzana ambazo zimekuwa zikitolewa na maofisa wa polisi, baadhi ya maaskari na hata daktari wa hospitali ambako Suzana alithibitishwa kuwa amefariki; wananchi na vyombo vya habari.

Tayari Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) Said Mwema ameunda tume kuchunguza mazingira ya kifo hicho.

Ni bahati mbaya kwamba sikushirikishwa katika uchunguzi huu; na kaimu kamanda wa polisi mkoa maalum wa Tarime/Rorya, Sebastian Zakaria, anathibitisha kuwa wajumbe wa tume wamemaliza kazi na kuondoka.

Kwa kuwa taarifa ya tume ya uchunguzi haijawekwa wazi, ni vema kutahadharisha kwamba sharti iwe inajibu maswali mengi na hoja kuu, vinginevyo hadhi ya Mwema, jeshi lake na serikali, itaporomoka. Hapa kuna maeneo ya kujengea mashaka:

Kwanza, Suzana alikuwa wapi alipokumbwa na mauti? Kuna ndimi mbili: kwamba alikuwa mapokezi kwenye kituo cha polisi; na kwamba alikuwa ofisini kwa kamanda wa polisi alimojifungia.

Kama alikuwa mapokezi, bunduki aliipata wapi? Hakuwa kwenye lindo. Bunduki haziwekwi mapokezi. Hakuna taarifa za Suzana kumnyang’anya askari bunduki pale mapokezi.
Kama bunduki ilikuwa imeachwa tu pale, kwa uzembe wa askari mmoja, mbona hakuna juhudi za kumzuia Suzana kuchukua bunduki hiyo?

Katika hatua hii, sharti tujue kulikuwa na nani mapokezi. Nani walikuwa zamu? Waliona nini na walichukua hatua gani? Inawezekana WP 7338 alichukua bunduki kutoka mapokezi na kwenda nayo hadi ofisi ya kamanda?

Kama hakuchukua bunduki kutoka mapokezi, Suzana alipata wapi bunduki? Kama alibeba bunduki, bila kuwa zamu na bila kukabidhiwa kihalali, kutoka mapokezi, askari wa zamu alichukua hatua gani?

Pili, kama hakubeba bunduki, sasa ile ya aina ya smg inayodaiwa kutumika, aliipata wapi? Silaha haziwekwi ofisini kwa kamanda.

Kutoka mapokezi hadi ofisini inapodaiwa alijipigia risasi kuna umbali wa hatua kumi au zaidi. Katika umbali huo, nani alimwona Suzana akibeba bunduki?

Bila kudharau madai kuwa muhusika alikuwa “anakwenda kujiua” au kutenda jinai; na kwa kuzingatia madai kuwa alikuwa ameamriwa kwenda au alikuwa amekamatwa na kupelekwa mapokezi, alijinasua vipi hadi kupata silaha?

Akiwa na silaha au hata bila silaha, WP 7338 aliweza vipi kutoka mikononi mwa waliokuwa wanamshikilia na kumtuhumu, na kwenda umbali wa hatua zaidi ya kumi, kufungua ofisi na kujifungia?

Tatu, kama Suzana alipata bunduki mapokezi, kwa nini hakujiua palepale au hata hatua mbili kutoka mapokezi? Alikuwa na sababu gani ya kujificha?

Kujiua kwa bunduki ni tendo la papo kwa papo. Ni tofauti na kujinyonga kwa kamba ambapo wapitanjia wanaweza kukuta ukitupa miguu na kufanikiwa kukata kamba na kukuokoa.

Kuna mantiki gani kwa Suzana “aliyeamua” kuondoa uhai wake, na ndio amerejea kutoka mafunzo ya matumizi ya silaha, kujiulia ndani ya ofisi ya kamanda “alimojifungia” badala ya kujiulia barazani, chooni au masijala?

Nne, hadi siku ya pili tangu tukio, kitasa cha mlango wa ofisi ambamo inadaiwa Suzana alijipigia risasi, kilikuwa hakionyeshi kubomolewa ili “kuondoa maiti.”

Hivi ni kweli mlango wa ofisi hii huwa unafungwa? Kama hufungwa je, mwenye ofisi anapotoka huacha funguo kwenye kitasa? Je, huko ni kufunga?

Kama kitasa hakikubomolewa, nani mwenye ufunguo wa ziada aliyefungua mlango ili kuondoa maiti? Hata kabla ya hilo, nani alijua kuwa kuna Suzana ndani ya ofisi na amejiua? Yuko wapi shahidi wa kwanza?

Tano, kuna madai ya WP 7338 kujimiminia risasi tatu. Nani aliona hilo? Daktari anazumgumzia risasi (siyo moja wala tatu – kwa mujibu wa taarifa za magazeti).

Kwa nini haikutoka risasi moja ambayo inatosha kuondoa uhai kutegemea na alipolenga? Kwa nini hazikutoka risasi zaidi ya tatu kama kubonyeza tu katika mazingira ya kukata tamaa na kujikana yanavyoelekeza?

Hili linatuongoza katika kutaka kujua ni bunduki ya aina gani, ilikuwa na risasi ngapi na ilibakiwa na risasi ngapi.

Hii ni muhimu ili kuweza kujua iwapo aliyejipiga risasi moyoni anaweza kupata nguvu za kujiongezea risasi nyingine; au kama zilitoka mfululizo, zilibaki ngapi au ziliisha?

Rekodi hazionyeshi Suzana kupewa bunduki siku hiyo. Je, bunduki hiyo alikuwa amepewa nani; kwenda wapi na kwa nini ilipatikana mahali pale na kutumiwa kwa kazi ambayo haikupangiwa? Vipi?

Sita, kuna madai ya WP 7338 kuwekwa mahabusi. Lakini mahabusi hakuna silaha. Hata wembe hauruhusiwi.

Hata kama kungekuwa na silaha, Suzana angechomokaje humo na silaha, kutoka nje ya jengo, kutembea umbali wa hatua zaidi ya kumi, kujifungia ofisini hadi kujiua wakati yuko chini ya ulinzi?

Saba, madai kwamba Suzana “alipoteza msafara wa rais,” yanasemwa na watu wengi mjini Tarime, pamoja na baadhi ya askari polisi.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa hata njia aliyoonyesha Suzana ilikuwa njia mbadala inayokwenda kulekule ambako rais alikuwa akienda.

Hakujapatikana ushahidi kuwa Suzana alikuwa na nia mbaya katika kuelekeza njia. Lakini inasimuliwa kuwa wakubwa wake walikasirishwa na tendo hilo.

Sasa nani aliamuru Suzana achukuliwe hatua? Nani aliamuru aripoti kituoni? Nani alitoa amri kuwa ahojiwe na “kushughulikiwa?”

Kamanda Zakaria ananukuliwa akisema, “…tunahisi alitishwa na wenzake…” Vyovyote itakavyokuwa, Suzana aliogopa hatua gani ambayo ni kali kuliko kupoteza maisha?

Wakati wa ziara ya mke wa rais, Salma Kikwete mwaka huu, polisi wanadaiwa “kugonga” watu watatu, lakini hakuna aliyetajwa kuwa amesumbuliwa.

Iweje Suzana aliyeonyesha njia, tena inayokwenda kulekule kulikotarajiwa, ndiye akumbane na kashkash?

Nane, kama kweli Suzana alijiua kutokana na vitisho, nani alimwambia nini – kilichozamisha fikra zake zote – na kuamua kuondoa uhai wake? Kitu gani kilimtisha na kilisemwa kwa nia ipi?

Tisa, kwa nini kunakuwa na kauli nyingi zinazotofautiana kutoka kambi moja? Nani alisema nini; katika nafasi ipi na kwa shabaha gani?

Iwapo tume ya inspekta jenerali Said Mwema haitakuja na majibu kwa maswali haya na mengine, umma utasita kuamini nia ya Mwema, polisi na serikali.

0
No votes yet