Kifo cha Wangwe: Msiba wa CHADEMA mikononi mwa CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version

KITENDAWILI kuhusiana na kilichosababisha kifo cha mbunge wa Tarime, mkoani Mara, Chacha Zakayo Wangwe (CHADEMA), bado hakijateguliwa.

Wangwe, mwanaharakati na mwanasiasa, alikutwa na mauti Jumatatu 25 Aprili, 2008, katika kijiji cha Pendamili, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma, baada ya gari alilokuwa akisafiri kudaiwa kupata ajali.

Mbali ya kuwa mbunge wa Tarime, Wangwe alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mara, na Diwani wa Tarime mjini.

Mengi yamesemwa kuhusiana na kifo chake. Kuna waliosema alikufa kwa risasi na wengine kusema ni mapenzi ya Mungu tu. Kuna ya kweli na kuna yaliyotiwa chumvi.

Hata hivyo, bado kuna maswali mengi ambayo hayajapatiwa majibu mpaka sasa.
Kwanza, katika gari la marehemu kulikuwa na watu wangapi? Je, ni kweli kwamba kulikuwa na mtu mwingine wa tatu? Yuko wapi sasa?

Suala hili la kuwapo kwa mtu mwingine wa tatu, mbali na marehemu na Deus Mallya, ambaye tayari amekiri kuwa alikuwa katika gari la marehemu siku ya tukio, limeibuliwa na Mwiguni George, anayedaiwa kufika eneo la tukio dakika chache baada ya ajali.

George amethibitisha kwamba alimkuta marehemu Chacha akiwa amefunga mkanda katika kiti cha mbele kushoto mwa dereva.

Ni yeye aliyesema alimkuta Mallya akiwa kiti cha nyuma. Ni George aliyesema Mallya hakuwa dereva wa gari hiyo, na kwamba Chacha pia hakuwa akiliendesha.

Awali Mallya katika maelezo yake kwa waandishi wa habari na polisi, alisema kuwa hafahamu hata kuendesha gari.? Lakini hakuna chembe ya mashaka kwamba Mallya anajua kuendesha gari, ingawa inawezekana akawa hana leseni.

Pili, nani alikuwa wa kwanza kuijulisha familia ya marehemu juu ajali hiyo? Swali hili ni muhimu sana kutokana na kile kinachoelezwa kwamba mmoja wa wake zake Wangwe, Mariam Chacha Wangwe, alikuwa miongoni mwa watu wa awali kabisa waliojulishwa juu ya tukio hilo.

Kama alijulishwa na Mallya, kwa nini basi Mallya hakuwajulisha kwanza viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA? Je, hafahamu simu zao? Mbona anadai kuwa anawafahamu? Na hakika anawafahamu.

Tatu, nani aliyekuwa wa kwanza kutoa taarifa polisi? Alipata wapi namba za polisi? Alipiga namba gani ?zile za kawaida au alipiga kwa mmoja wa polisi? Ilichukua muda gani polisi kufika kwenye eneo la tukio tangu ajali kutokea? Mtoa taarifa alijuaje kama Wangwe amefariki?

Hili ni muhimu pia kwa sababu kuna utata wa mtu aliyetoa taarifa polisi. Huyu akipatikana anaweza kusaidia kujulikana taarifa nyingine za ziada, ikiwamo alijuaje kwamba Wangwe amepata ajali na amefariki.

Itajulikana jinsi yeye alivyopata taarifa. Nani alimjulisha? Alikuwa wapi wakati wa tukio? Kama alikuwa katika eneo la tukio, ni kweli kwamba Mallya hakuwa anaendesha gari linalodaiwa kuwa lilipinduka na kumuua Wangwe? Kama ndiyo, nani alikuwa dereva. Alimuona nani mwingine ndani ya gari? Huyu anayedaiwa kuwa alisema, "Chukua fedha katika koti," alikuwa nani? Sasa yuko wapi?

Nne, nani aliyewajulisha watu wa Tarime kuhusiana na kifo cha mbunge wao? Hii ni muhimu kutokana na ukweli kwamba watu wa Tarime walikuwa miongoni mwa watu wa awali kupewa taarifa.

Inaelezwa kuwa wapiga picha hawa walipata taarifa kabla ya viongozi wa CHADEMA waliokuwa mita chache kutoka eneo la tukio.

Tano, mkuu wa mkoa wa Dodoma, William Lukuvi, alijulishwa na nani kuhusu kifo cha Wangwe, hadi naye akaziamini taarifa hizo na kumjulisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurance Masha, ambaye naye aliwajulisha viongozi wa CHADEMA.

Je, Lukuvi alijulishwa na Mkuu wa wilaya ya Kongwa, anayesema kwamba alifika eneo la tukio dakika 30 baada ya ajali? Kama ni hivyo, yeye alijulishwa na nani na alijuaje kuwa ni muda huo tangu ajali itokee? Alikuwa wapi wakati huo?

Taarifa kwamba viongozi wa CHADEMA walijulishwa na Waziri Masha zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe.

Sita, zipo taarifa zinazosema marehemu Wangwe, alikuwa na kompyuta ya mkononi (Laptop) na inaelezwa kwamba siku ya tukio alikuwa nayo. Je, hivi sasa iko wapi? Nani anaishikilia?

Inaelezwa pia kwamba Wangwe alikuwa na silaha ya kujilinda (bastola). Sasa anayo nani?

Saba, Deus Mallya ambaye sasa imethibitika kwamba alikuwa na marehemu kabla ya ajali, ni nani hasa? Anafanya shughuli gani? Anaishi wapi? Uhusiano wake na marehemu ni upi na ulianza lini?

Je, ni kweli kwamba Mallya amepata mafunzo ya kijeshi, au mafunzo mengine nchini Libya? Kama ndiyo, ni mafunzo yapi na yalichukua muda gani?

Madai kwamba Deus Mallya anajua kwa ufasaha lugha ya Kiarabu yana ukweli gani? Kama madai haya yana ukweli, vyombo vya ulinzi na usalama vinafahamu jambo hilo? Kwa kiwango gani?

Ni wapi Mallya alijifunzia lugha hiyo? Nini kilimshawishi kujifunza Kiarabu? Alitaka kutumia lugha hiyo kwa kazi gani?

Nane, viongozi wa CHADEMA wana uhusiano gani na Mallya hadi wakadiriki kumuacha kufuatana na makamu mwenyekiti wao na mbunge wao pekee katika eneo la Kanda ya Ziwa Viktoria?

Wamemfahamu toka lini na wapi? Kabla ya hapo hawakuwahi kumtilia mashaka? Kama ndiyo ni kwa kiwango gani? Walichukua hatua gani?

Tisa, mahusiano ya marehemu na familia yake yakoje? Je, walikuwa wanapikika chungu kimoja na mdogo wake, Peter Wangwe.

Peter Wangwe alikuwa diwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, wakati Chacha Wangwe akiwa diwani wa Tarime mjini, kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, mwaka 2000.

Vituko na vitimbi alivyofanyiwa Wangwe wakati huo bado vinakumbukwa. Kwa kile Wangwe alichopenda kuita, "mtandao wa viongozi wa CCM," alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Alitoka gerezani baada ya viongozi wa CHADEMA, chini ya mwanasheria Tundu Lissu, kukata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Mwanza.

Alipotoka gerezani alikuwa ni Wangwe aliyeandaa kaburi la kisiasa la Peter, mdogo wake ambaye alidondoshwa kwenye nafasi ya diwani na kupotea kabisa kwenye ngazi ya uongozi wa CCM.

Hii ndiyo maana kuna wasioshangazwa na taarifa kwamba siku ya mazishi Peter alibeba bango lililokebehi viongozi wa CHADEMA na CCM kwa pamoja kwa kuuliza, "Ni ajali au risasi?" Ni Peter aliyebeba bango ambaye anajua alikopata msamiati wa "risasi."

Kumi, Wangwe alikuwa anajiandaa kupeleka hoja binafsi bungeni kuhusiana na kile alichoita, "Vitendo vya mwekezaji katika mgodi wa North Mara." Mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya Barrick iliyokumbwa na mizozo na wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Siku moja kabla ya kukutwa na mauti, Wangwe alimueleza Spika wa Bunge, Samwel Sitta kwamba anadhamiria kupeleka hoja binafsi bungeni; akisema watu 84 walikuwa wamekamatwa na polisi katika eneo la Nyamongo, wilayani Tarime.

Je, mahusiano yake na wawekezaji waliopo katika jimbo lake na mkoa wa Mara kwa ujumla yalikuwaje? Walikuwa wanaiva? Kama walikuwa hawaivi, ni kwa nini na kama walikuwa wanaiva ni kwa kiwango gani? Je, mahusiano hayo yaweza kuhusishwa, kwa aina yoyote ile, na kifo chake?

Ukiacha yote hayo, msiba huu umekuja wakati kuna mnyukano wa uongozi kati ya Wangwe na wenzake katika CHADEMA.

Lakini jambo jingine kubwa ni kwamba msiba ulikuwa wa CHADEMA, lakini bado ulikuwa mikononi mwa makada wa CCM na serikali yao.

Profesa Samwel Wangwe, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na mdogo wake Peter Wangwe, ni mmoja wa waumini wa CCM anayetaka kurejea katika udiwani wilayani Tarime.

Kutokana na hali hiyo, hakuna ubishi kwamba vitimbwi vya aina yoyote vingeweza kutokea kwenye mazishi yake.

Katika hoja yake ambayo alikuwa awasilishe bungeni kupinga kukamatwa kwa wapigakura wake 600, Wangwe anahoji, "Jambo la kushangaza, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kueleza ni vipi wananchi hao waliingia ndani ya mgodi wenye uzio na ulinzi mkali wa polisi na mbwa."

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: