Kigogo ang'olewa Bima


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version

HATIMAYE Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Margret Ikongo ameng’olewa kwenye shirika hilo.

Habari kutoka shirika hilo na Wizara ya Fedha, zinasema, “Ni suala la muda tu, Ikongo atatoweka NIC. Atahamia wizarani katika kitengo cha bima.”

Ikongo anang’oka NIC baada ya malalamiko ya muda mrefu kwamba ameshindwa kuendesha shirika na kwamba NIC imekosa usimamizi, mwelekeo na imeporomoka kibishara.

MwanaHALISI liliongea na Ikongo kutaka kujua ukweli wote kuhusu suala hilo; naye alijibu haraka na kwa ufupi tu:

“Nisubiri hadi Alhamisi ili tuzumgumze. Hapo nitaweza kutoa back ground (historia ya mambo) yote. Vitu vingine ni personal (binafsi), lakini ninyi waandishi mnafanya mambo kuwa makubwa,” alisema Ikongo.
 
Taarifa zinasema tayari serikali imemtaka Ikongo kukabidhi ofisi ya NIC kutokana na shirika kushindwa kuleta ufanisi na kwamba alikuwa katika hatua za mwisho kufanya hivyo.

Imeelezwa kuwa serikali imemtaka Ikongo akabidhi ofisi kwa mwenyekiti wa Bodi ya NIC, Dk. Hamis Kibola na yeye (Ikongo) kuripoti wizara ya fedha, Idara ya Usimamizi wa Bima ili kupangiwa kazi nyingine.

Ikongo na menejementi yake walikabidhiwa uongoza wa NIC tangu mwaka 1999, lakini hadi sasa halijaweza kuleta tija; badala yake limeendelea kuleta hasara mwaka hadi mwaka.

Ni kutokana na hasara hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, chini ya mbunge wa Handeni, Tanga, Dk. Abdallah Kigoda, iliagiza serikali kuondoa menejementi, wafanyakazi na Bodi ya wakurugenzi wa NIC ili kulinusuru shirika hilo na hatari ya kufilisika.

Tayari serikali imeondoa wafanyakazi wote wa NIC isipokuwa menejementi ya Ikongo na Bodi ya Kibola.

Ikongo aliahidi kuzungumza na MwanaHALISI Alhamisi (kesho) 16 Aprili 2009 kwa madai kuwa “kwa sasa mimi si msemaji katika suala hilo.”

Uongozi wa Ikongo umekuwa ukikabiliwa na shutuhuma na tuhuma kadhaa ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, kuporomoka kwa shirika kutoka kumiliki asilimia 99 ya soko la bima mwaka 1997 hadi asilimia 25 mwaka 2008.

NIC inaendelea na mgogoro wa wafanyakazi ambao wanadai kutolipwa stahiki yao na tayari wameburuza uongozi mahakamani.

Ikongo aliyeanza kazi NIC mwaka 1978 kama karani katika Idara ya Bima za Madai ya Magari, mpaka anateuliwa kuliongoza shirika hilo hakuwahi kufanya kazi katika idara nyingine.

0
No votes yet