Kiingereza na 'uhuru wa kujiua'


Rehema Kimvuli's picture

Na Rehema Kimvuli - Imechapwa 22 July 2008

Printer-friendly version

WAZAZI wengi wa Tanzania wamekuwa wakikimbilia kupeleka watoto kusoma katika shule zilizo nje ya nchi hasa Uganda, bila kufuatilia wasifu wa ndani na nje wa shule hizo.

Ukiwauliza kwa nini wanawapeleka watoto wao wadogo, wa kati ya miaka mitano na 18, utaambiwa kuwa ni kwa ajili ya kupata 'elimu bora.'

Wazazi wengi wa Tanzania wanaamini Uganda kuna elimu bora zaidi. Kisa? Eti watoto wao wanaporudi nyumbani wanakuwa wanaongea Kiingereza kizuri, tena kilichonyooka na bila kigugumizi!

Hivi tujiulize elimu bora ni kuzungumza Kiingereza au ni kuelewa ulichofundishwa na kukifanyia kazi kwa manufaa yako binafsi najamii?

Sisemi kuwa siyo muhimu kujua kusoma, kuandika na kuongea Kiingereza. Nasema lugha hiyo isiwe sababu ya kuwapeleka watoto nje ya nchi wakiwa bado wanahitaji malezi ya wazazi.

Kuna wafanyakazi wengi waliopo maofisi hapa Tanzania wanaofanya kazi zao kwa ufasaha; hakika kama inavyotakiwa ingawa hawajui Kiingereza kwa ufasaha.

Hata hivyo, wazazi wanaopeleka watoto wao nchini Uganda, sijui kama wamekuwa wakifuatilia maendeleo yao wawapo huko.

Aidha, haifahamiki kama wamekuwa wakifuatilia mienendo ya watoto wao wanaporudi kutoka shule ili kuangalia kama kuna mabadiliko yoyote kitabia.

Kwa wazazi waliokuwa makini na watoto wao watakuwa wamegundua mabadiliko makubwa wanayokuwanayo watoto pale wanaporudi nyumbani wakati wa likizo.

Wale waliogundua hitilafu katika tabia za watoto wao wameamua kuwarudisha nyumbani ili wasome shule za kutwa au za karibu ambako wataweza kuwatembelea na kupata kujua mahudhurio na maendeleo yao shuleni.

Wengi wa wanafunzi wanaosoma Uganda wanakuwa na mabadiliko kitabia, kimavazi na hata kielimu.

Kama walikuwa wakifanya vizuri darasani, utaona wanaanza kufeli; kama walikuwa wakivaa kiheshima, wataanza kuvaa nguo fupi na na za kuonyesha maungo; na kama walikuwa wenye nidhamu utaona waziwazi kuwa inamomonyoka.

Wanafunzi wadogo wa umri wa chini ya miaka 18 wamekuwa wakiharibika kitabia hasa ukizingatia katika umri huo wengi wao wanakuwa katika hatua ya kupevuka; ule umri wa mabadiliko ya mwili na hata saikolojia.

Wengi wa vijana hao wameshawishika kuingia tabia za uvutaji bangi, unywaji pombe na vitendo vya ngono.

Yote haya ni kutokana na sababu kubwa mbili. Kwanza, ni suala la wanafunzi kuwa mbali na wazazi wao na kukosa malezi na ufuatiliaji wa wazazi.

Leo hii wazazi wako mbali. Hawawezi hata kupata muda, japo mwisho wa mwezi, kwenda kuwatembelea shuleni kujua mahudhurio na maendeleo yao.

Wanafunzi hawana tena usimamizi waliojengewa wakiwa karibu na wazazi wao. Hakuna wa kutaka kujua leo wamejifunza nini, kuona mahudulio wala kuwahimiza kimasomo.

Sababu ya pili ni ile ya mwanafunzi kujiona wana kile wanachoita 'uhuru' wa kufanya kila wanachojisikia kufanya pasipo kuingiliwa na mtu.

Baadhi ya wanafunzi sasa hawatamani hata kurudi nyumbani kwao kwa kutoa sababu ya kubaki huko kuendelea kujisomea kumbe wanafanya starehe.

Shule nyingi za Uganda ni za kibiashara. Wanachojali ni wanafunzi kulipa ada tu na sio kufuatilia mahudhurio yao shuleni.

Hii ndio maana wanafunzi wamekuwa na uwezo hata wa kujihamisha kutoka shule moja kwenda nyingine pasipo mzazi anayemlipia ada kujua. Wamefanikiwa kupata nafasi katika shule wanayoitaka.

Wamekuwa wakianguka mitihani mara kwa mara kutokana na kusahau kilichopelekea wao kuwepo nchini Uganda. Wanapoanguka mitihani ya shule, badala ya kurudia darasa, wao wamekuwa wakiamua kuhama shule.

Kama huo ndio uhuru, basi ni uhuru ambao inabidi usimamiwe ili uwe wa manufaa kwao na jamii kuliko kuwa 'uhuru wa kujiangamiza.'

Hakuna mtu mwenye haki ya kudai kuwa ana uhuru wa kujiua. Anayejaribu kujiua hukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa hatua ya kutaka kujiua.

Wanafunzi hawa wanastahili kulindwa ili wasijiue kupitia tabia mbovu ambazo pia zina uwezekano wa kuambukizwa kwa wanafunzi wengine.

Kama wazazi wanataka watoto wao wajue Kiingereza vizuri, na wana fedha za kuwagharimia, kwa nini wasiwapeleke Uingereza badala yaUganda?

0
No votes yet