Kikwete ‘afukuza bundi’ Zanzibar


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 July 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Dk. Mohammed Gharib Bilal

HATIMAYE ndoto ya Dk. Mohammed Gharib Bilal imetimia. Kukurukakara zake za miaka kumi zimezaa matunda na tayari amerudi ulingoni.

Alitamani kuwa rais wa Zanzibar. Alitumia kila fursa inayopatikana kujiimarisha kisiasa na hata kiuchumi. Alifanikiwa na sasa mtandao wake wa aina ya kipekee umemtua kileleni.

Dk. Bilal hakuteuliwa kugombea urais Zanzibar ili ajihusishe moja kwa moja na siasa na minyukano yake Visiwani, lakini hapa halalamiki.

Rais Jakaya Kikwete amemteua kuwa mgombea mwenza wake; naye atatulia kwenye nafasi ya makamu iwapo rais atashinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.

Sasa Dk. Shein atagombea urais Zanzibar. Dk. Bilal atakuwa mgombea mwenza Bara. Iwapo Dk. Shein atashinda Zanzibar, atakuwa rais wa kwanza wa Visiwa hivyo anayetoka Pemba.

Vilevile iwapo mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharrif Hamad atakuwa mshindi katika kinyang’anyiro cha mwaka huu, basi rais atakuwa anatoka Pemba.

Jina la Bilal liliibuka mwishoni mwa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliomalizika mjini Dodoma, Jumapili baada ya kupata chini ya nusu ya kura alizopata Dk. Ali Mohammed Shein na kuwa mgombea urais Zanzibar.

Wakati wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar wakiwa bado wanasubiri miujiza – wapi Bilal atachomekwa kufuatia ufuasi wake mkubwa Unguja – wengine walikuwa wameridhika kuwa mzee huyo sasa amepotea kabisa katika siasa za Muungano.

Toleo la MwanaHALISI la wiki iliyopita liliandika kuwa mpango wa Rais Kikwete na Rais Karume kufanya Dk. Shein kuwa mgombea urais umekamilika.

Liliandika kuwa sasa Dk. Bilal atabaki kutegemea fadhila za rais mpya. Ndivyo ilivyokuwa katika maeneo yote mawili.

Kuibuliwa kwa Dk. Bilal, kwa hiyo, kuwa mgombea mwenza, kumetokana na Rais Kikwete kufaulu “kupanda farasi watatu” kwa wakati mmoja.

Amefurahisha pande tatu kwa wakati mmoja. Amembeba Dk. Shein, Dk. Bilal na kusimama imara na Dk. Karume.

Kuna wakati wapambe wa Dk. Shein walitumia jina la Kikwete kujinadi. Kwamba mgombea wao ametumwa na wakubwa kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Hata ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), madai kwamba Shein alikuwa chaguo la Kikwete na Karume yalikuwa wazi. Haiingii akilini kwamba Kikwete na Karume hawakuyasikia; bali hawakuyakana.

Ni kawaida ya Rais Kikwete kusema kuwa kati ya wagombea waliojitokeza, “hakuna niliyemtuma.”

Hakusema hivyo mara hii. Wachunguzi wa mambo wanasema huenda hakutaka kumuudhi Karume ambaye inadaiwa alikuwa na msimamo kama wake juu ya nani awe mgombea urais Zanzibar.

Nje ya ukumbi, wajumbe walikuwa wakisema waziwazi kuwa kwa hatua ya Kikwete kukaa kimya juu ya madai hayo, basi Dk. Shein alikuwa hakika chaguo lake.

Taarifa zinasema ndani ya mkutano wa NEC, mmoja wa wajumbe kutoka Kanda ya Ziwa Viktoria alihoji hatua ya Kamati Kuu “kututeulia mgombea.”

Alituhumu baadhi ya kauli za rais kwamba “zilikuwa elekezi.” Hakuna mwenye kujua kwa uhakika, sababu zilizomfanya Kikwete kumpigia debe Dk. Shein kwa kiwango kile.

Taarifa kwamba Rais Karume ndiye angekuwa mgombea mwenza, sasa zimeyeyuka. Wachunguzi wa siasa za CCM wanasema hilo limetokana na hali iliyojitokeza Zanzibar baada ya uteuzi wa Dk. Shein kuwa mgombea urais.

Kwani baada ya Dk. Shein kupitishwa, moto uliwaka Zanzibar, wengi wakililia Dk. Bilal waliyetarajia kuteuliwa. Ilihitajika busara ya aina yake kutuliza kilichoonekana mara moja kuwa itakuwa vurugu.

Uamuzi uliofuatia, hata kama utaudhi baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM, umepoza wafuasi wa Dk. Bilal visiwani kuliko kurudi mikono mitupu kutoka Dodoma.

Tayari vyombo vya habari vilinukuu baadhi ya makada wa chama hicho kutoka Zanzibar, wakituhumu uamuzi wa kumpitisha Dk. Shein. Walisema wako tayari kupigia kura upinzani kuliko “mgombea huyo wa Kikwete na Karume.”

Sasa Dk. Bilal aweza kutulia na kufanya kazi na Rais Kikwete; lakini iwapo ataendelea kutaka kutimiza ndoto yake ya urais Visiwani, basi italazimu aelekeze wafuasi wake kupigia kura wapinzani ili iwe rahisi kwake kujitosa mwaka 2015 kama “mkombozi.”

Mtaalam mmoja wa mambo ya siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema Rais Kikwete “hapangi muda gani apande farasi yupi.”

Amesema angekuwa anapanga muda wake vizuri, asingeruhusu Dk. Bilal kujeruhiwa kiasi kile hadi kuvuruga chama chake.

“Angemuita na kumtaka kutoweka jina lake ili hatimaye amteue kuwa mgombea mwenza,” ameeleza msomi huyo aliyesema hahitaji kutajwa gazetini.

Lakini hatua yake hii ya kumuacha katika kinyang’anyiro hadi mwisho, huku yeye na Karume wakikaa kimya, imesababisha madhara makubwa kwa CCM.

Kumekuwa na madai kuwa Bilal ni mtu wa visasi na kwamba akichukua madaraka hataweza kuthamini rais anayemaliza muda wake.

Imekuwa ikidaiwa pia kuwa ndani ya miaka 10 ya utawala wa Rais Karume, rais mstaafu Dk. Salmin Amour (Komandoo) hakuthaminiwa, hakuenziwa wala kutambuliwa kama rais mstaafu.

Hii ndiyo maana kuwepo kwa Salmin kwenye mkutano wa NEC, baada ya kutohudhuria vikao vingi, kulichukuliwa kuwa fursa ya kipekee ya kujenga hoja kwa manufaa ya Dk. Bilal.

Wachunguzi wa mambo wanasema kuibuka kwa upinzani Zanzibar katika hatua hii, ambako kumesababisha Dk. Bilal kuteuliwa mgombea mwenza, ndiko kumepoteza nyota ya Zakhia Meghji kuwa mwanamke wa kwanza mgombea mwenza Bara.

Kwa zaidi ya miezi sita sasa kumekuwepo tetesi kwamba Meghji ndiye angeteuliwa kuwa mgombea mwenza Bara.

Hata hivyo, matukio Dodoma na Zanzibar yataleta msisimko mpya na ulazima wa kujipanga upya.

Kauli za Rais Kikwete na Dk. Shein zinaelekeza kwenye fikra za kuondoa mgawanyiko na mifarakano katika siasa za Zanzibar.

Je, baada ya hapa kutakuwa shwari? Nani anaweza kujiaminisha kuwa sasa Rais Kikwete amefaulu kufukuza bundi Zanzibar?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: