Kikwete ‘ameza uchafu’ Arumeru


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete amemezea uchafu uliokithiri katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake jimboni Arumeru Mashariki, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichofanyika ikulu jijini Dar es Salaam, juzi Jumatatu, zinasema pamoja na kuthibitika kwa tuhuma za rushwa, Kikwete ameamua kuzinyamazia.

Badala yake, taarifa zinasema, mkuu huyo wa nchi amebariki watuhumiwa wa rushwa kurudia mchakato kwa maelezo kuwa wote wawili “hawakutimiza akidi ya kura zilizotakiwa.”

“Ndugu yangu, chama hiki kinaelekea kubaya. Tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wagombea zilikuwa wazi na nzito mno; lakini mwenyekiti amekataa ushauri wa wajumbe wengi. Badala yake ameamuru kura zilirudiwe,” ameeleza mtoa taarifa wa gazeti hili.

Taarifa zinasema ripoti za vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, zilizowasilishwa katika CC, ilipelekwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Siyoi Sumari, mmoja wa wagombea katika kura za maoni aliyeongoza kwa kura nyingi, alituhumiwa kuongoza pia katika kutoa rushwa.

Wakati wenzake wanne wanadaiwa kutoa rushwa ya kati ya Sh. 30,000 na 80,000, kutegemeana na “uzito” wa mpigakura, Siyoi amedaiwa kuhonga kati ya Sh. 100,000 na 200,000 kwa kila mjumbe.

Kwa mara ya kwanza, baadhi ya wajumbe wa CC wamepongeza TAKUKURU kwa kuwa makini kuhusu mchakato wa kura za maoni.

Aidha, moja ya nyaraka ambazo gazeti hili limeona inasema, mwanasiasa Siyoi, ambaye ni mtoto wa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari, anadaiwa kuwatumia wazee wa kimila kumfanyia kampeni.

“Tarehe 19 Februari 2012, siku moja kabla ya kupiga kura za maoni, Siyoi alifanya misa ya shukurani kwa ajili ya kuomboleza kifo cha baba yake mzazi. Imeelezwa kuwa misa hiyo ilitumika kumfanyia kampeni,” umeeleza waraka mmoja uliopelekwa CC.

Kwa mujibu wa waraka huo wa Takukuru, Siyoi alitumia misa hiyo ya shukurani kutafuta kura.

“Misa iliyofanyika 19 Februari 2012, ilitumika kwa ajili ya kampeni ya mmoja wa wagombea. Wapambe wa mgombea huyo walitumia hafla ile kuwafariji watu mbalimbali waliohudhuria ikiwamo kuwapa nauli,” unaeleza waraka huo.

Mbali na kutumia misa kufanya kampeni, Siyoi anadaiwa kumtumia Mshiri Mkuu (kiongozi mkuu wa kimila wa Washiri), kumfanyia kampeni kwa kuwa yeye ni baba mdogo wa mgombea,” zinaeleza taarifa kutoka CC.

Ndani ya CC, taarifa zinasema baadhi ya wajumbe walihoji kitendo cha viongozi wa kimila kubeba mmoja wa wagombea na kuacha wengine na kukitaka chama chao kufuta wagombea wote walioshiriki vitendo vya rushwa.

Imeelezwa kuwa hata baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa, kwa mfano Onesmo Nangole, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, walishiriki vitendo vya ukiukwaji taratibu.

Ndani ya kikao cha CC, taarifa zinasema Kikwete alionyesha kukerwa tu na kitendo cha Nangole kumshabikia mmoja wa wagombea.

Akiongea kwa sauti ya ukali, Rais Kikwete amenukuliwa akisema, “Viongozi waliotarajiwa kusimamia haki, ndio waliokuwa mstari wa mbele kupindisha kanuni kwa kuegemea upande mmoja. Hili jambo limenisikitisha sana.”

Akiongea kwa kuonyesha uchungu huku akimtolea macho Nangole ambaye alikuwa mjumbe mwalikwa wa mkutano huo, Kikwete alisema, “…Mwenyekiti umenisikitisha…”

Habari za awali zinasema, mgawanyiko mkubwa ulitokea kwenye kamati ya siasa ya wilaya ya Arumeru hadi kushindwa kupendekeza jina la mgombea mmoja.

Inaelezwa kuwa kamati hiyo ilitoa alama B kwa wagombea wanne walioongoza ambao, ni Siyoi Sumari aliyepata kura 361, William Sarakikya aliyepata kura 259, Elirehema Kaaya aliyepata kura 205 na Elishiria Kaaya aliyeambulia kura 176.

Anthony Musani alipata kura 22 na Rishiankira Urio aliambulia kura 11.

Kile ambacho wajumbe wengi walitaka kifuatwe, ni kufuta matokeo ya wagombea wote waliotoa rushwa, akiwamo Siyoi aliyeongoza kwa wingi wa kura.

Habari zinasema, ndani ya kikao cha CC, tuhuma kwa baadhi ya wagombea zilikuwa wazi, lakini Kikwete aliamua kuzinyamazia kwa staili ya “funika kombe mwanaharamu apite…”

“Hata huyu wa pili, William Sarakikya aliyepata kura 259, hakustahili kurejeshwa. Kimsingi kati ya wagombea wale watano waliosalia, ni mmoja tu ambaye alikuwa na sifa ya kupitishwa kugombea,” anaeleza mtoa taarifa huyo ambaye ni mjumbe wa CC.

Amesema, “…kuruhusu uchaguzi kurudiwa ni kukiangamiza chama chetu. Hii maana yeke ni kwamba tumeona ile rushwa ya kwanza ni ndogo; na hivyo tunataka wakahongane zaidi,” ameeleza kwa sauti ya masikitiko.

Ambaye alionekana kuwa na sifa na ambaye ndiye aliyeonekana kuwa alistahili kubeba bendera ya chama hicho, ni Elishiria Kaaya aliyeambulia kura 176.

Kaaya ni mkurugenzi mtendaji wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha – Arusha International Conference Centre   (AICC) na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM.

Mtoa taarifa amesema, “Katika mazingira hayo, kunyamazia taarifa hiyo kwa mtu kujifanya hamnazo, ni kukidhalilisha chombo hicho mbele ya jamii na kuwakatisha tamaa watendaji wake.”

Kura za maoni katika uchaguzi mdogo jimbo la Arumeru Mashariki, zilifanyika 20 Februari 2012 ambapo Siyoi alitangazwa mshindi.

Jingine ambalo lilionekana kumchukiza Kikwete ni madai kuwa James Millya, mwenyekiti wa umoja wa vijana (UV-CCM), mkoani Arusha, alihudhuria kikao cha viongozi wa UV-CCM wilayani Arumeru, huku akiwa si mjumbe halali.

Ni kikao hicho ambacho kilishirikisha viongozi wa UV-CCM kutoka kata 17 wilayani humo ambapo Millya anatuhumiwa kubadilisha azimio la kikao.

Azimio ambalo Millya anatuhumiwa kulibadilisha ni lile lililotaka chama kupitisha mgombea mwenye sifa na kuahidi kuunga mkono mgombea yeyote atakayepitishwa.

“Millya alichukua lile azimio, kung’oa ukurasa mmoja na kisha kuongeza maneno, ‘Siyoi asipoteuliwa, vijana tutasusa,’” ameeleza mtoa taarifa.

Mbali na Millya, mwenyekiti wa CCM wilaya ya Arumeru, anadaiwa kupindisha baadhi ya tararibu ili kumbeba Siyoi.

Mwenyekiti aliyetajwa kwenye CC kuwa alimbeba Siyoi, ni Ole Sayivoe ambaye ni ndugu wa mgombea huyo.

Pamoja na tuhuma hizo, Sayivoe anadaiwa kueleza baadhi ya viongozi wa mkoa, wilaya na kata, kwamba Siyoi ni mgombea mahususi aliyeletwa na Edward Lowassa.

Mtoa taarifa amesema kurejesha wanaotuhumiwa kutoa rushwa katika kinyang’anyiro cha kura za maoni, ni kukubali vitendo vya rushwa.

“Angalau hapa TAKUKURU walikuwa wametusaidia. Sasa sisi wenyewe tunajirudisha kwenye tope. Tutajivunia nini?” amehoji.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: