Kikwete ‘jino kwa jino’ na Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Edward Lowassa na Rais Jakaya Kikwete

HATUA ya kukivua gamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), imegeuka vita vya “jino kwa jino” kwa viongozi kukamiana.

Lakini kama Rais Jakaya Kikwete alilenga kuwafukuza watuhumiwa wa ufisadi kwenye chama, hakika ameshindwa.

Ameishia kuwaengua Rostam Aziz na Andrew Chenge kutoka Kamati Kuu (CC) lakini ameshindwa kuwang’oa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Pamoja na kwamba mjadala ulikuwa mkali kuanzia CC na hatimaye kwenye NEC ambako watuhumiwa hao wawili na Edward Lowassa walikamiwa kung’olewa, Kikwete “alipoteza mwelekeo” na kikao kumalizika bila maamuzi juu yao.

Vikao vya CC na NEC vilimalizika juzi Jumatatu usiku mjini Dodoma.

Uwezekano wa kung’olewa kwa vigogo hao ulionekana mapema katika hotuba za wajumbe wa CCM na kauli za hapa na pale za mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete tangu mwanzo wa vikao Ijumaa iliyopita.

Ndani ya CC, Kikwete amenukuliwa akisema, “Kanuni ya chama chetu inataka kila kiongozi anayeshiriki katika masuala yanayotilia mashaka uadilifu wake, haraka ajitoe katika uongozi, asipokubali, basi chama kimtose.”

Alisema, “Sitaki kusikia tuhuma za ufisadi katika chama na (madai kuwa) uadilifu wa viongozi siyo tatizo. Hilo ni tatizo na lazima lipatiwe ufumbuzi.”

Alitaka wajumbe wa CC kujadili hoja hiyo kwa kina na bila kile alichoita, “Kumung’unya maneno.”

Akiwa mzungumzaji wa kwanza baada ya Kikwete kutema nyongo, alikuwa Yusuf Mohammed Yusuf (Mrefu).

Alinukuliwa akisema, “…Chama hiki kina utaratibu wa kulinda haki za wanachama. Tuhuma pekee hazitoshi. Kufanya hivyo (kuwatema watuhumiwa), tutakuwa tunakiuka haki za wanachama wetu.”

Katika mjadala wa Jumamosi jioni, kila mjumbe aliyesimama kuchangia, ukiondoa Sophia Simba na wajumbe wengine wawili wa Zanzibar, wote waliunga mkono hoja ya Kikwete.

Hoja ambayo ilikuwa mbele ya wajumbe wa CC wakati huo, ilihusu tathimini ya uchaguzi na maadili ya viongozi wa chama hicho. Iliandaliwa na Profesa Eginald Mihanjo na kada wa muda mrefu, Wilson Mkama.

Miongoni mwa sababu ambazo zilitajwa na baadhi ya wachangiaji kuwa zilisababisha CCM kupata matokeo ambayo haikutarajia katika uchaguzi mkuu, ni migawanyiko iliyoletwa na utaratibu wa kura za maoni.

Sababu nyingine ni “kutoandikwa vizuri” na baadhi ya vyombo vya habari, kampeni kutoratibiwa vizuri na tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi ya viongozi.

Taarifa zinasema, mara baada ya hoja hiyo kuingizwa ndani ya mkutano wa CC, Yusuf akiongea kwa njia ya kutetea watuhumiwa wa ufisadi alisema, “Mwenyekiti tumetoka katika uchaguzi jana tu. Si vizuri kuanza kushughulikiana.”

Akichangia hoja hiyo, Bernard Membe alisema, “Utawala wa Roma ulianguka kwa mambo hayahaya ya ufisadi. Tuhuma tu? Tusidanganyane. Tuchukue hatua.”

Membe aliwataka wajumbe wenzake wa CC kuacha kupuuza tuhuma zinazokikabili chama chao, badala yake akasema,  “Tusitumie kisingizio hicho cha kukosa ushahidi kulinda watu ambao si waadilifu.”

Taarifa zinasema hadi hapo hakukuwa na mjumbe hata mmoja aliyekuwa ametaja jina la mtuhumiwa.

Lakini alikuwa Sophia Simba, mtetezi mkuu wa Chenge, aliyesema “Mwenyekiti, haya ni maneno ya magazeti. Kibaya zaidi, magazeti hayo ni yale ya wapinzani.”

Akirejea kauli yake ya siku nyingi, kwamba Chenge ameshasafishwa na shirika la upelelezi la makosa ya jinai la Uingereza (SFO) kuhusiana na ufisadi wa rada ya kijeshi, Simba alisema, “Tuhuma zenyewe si za kweli. Ameshasafishwa na SFO.”

Kauli ya Simba kwamba Chenge ameshasafishwa na SFO, iliibua mguno na minong’ono kwa wajumbe wa kikao.

Mguno wa wajumbe utakuwa ulitokana na taarifa zilizotangazwa kwa mapana na marefu zikisema Ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam, umekanusha na kukosoa kauli ya Simba kuhusu kazi ya SFO.

Mara baada ya Simba kumtaja Chenge, ndipo mtoa taarifa anasema, Kikwete alipata ujasiri wa aina yake na kutoa kauli yenye uthabiti.

“Mimi sitaki unafiki. Nataka tuseme hapa, nani hao mafisadi wanaosemwa. Hatuwezi kukaa hapa kwenye kikao, huku tukiwa tumepewa dhamana na wananchi na wanachama wetu, kisha tunataja watuhumiwa bila kutaja majina.”

Akionekana mwenye hasira kali, Kikwete aliuliza, “Hivi tunamdanganya nani? Kwa nini watu wazima tunakuwa wanafiki?”

Kauli hiyo ilimwinua Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara. Alitaja majina ya Lowassa, Rostam na Chenge.

“Nikiwa mwenyekiti wa Kamati ya udhibiti na nidhamu, majina ambayo yamekuwa yakitajwa na wana-CCM, ni Rostam Aziz, Edward Lowassa na Andrew Chenge.”

MwanaHALISI limeelezwa mara baada ya Msekwa kutaja majina hayo matatu, ndipo Kikwete akasema, “Sasa tumeshapata majina na tuendelee. Tuache kumung’unya maneno.”

Naye George Mkuchika, aliyekuwa naibu katiku mkuu hadi juzi Jumamosi, akichangia suala hilo, imeelezwa alikumbusha wajumbe sakata la kujiuzulu kwa Ali Hassan Mwinyi.

Mwinyi alijiuzulu uwaziri kutokana na mauaji ya wafungwa katika gereza la Kahama mkoani Shinyanga katika miaka ya 1970.

Mkuchika alisema wakati Mwinyi anajiuzulu alimwandikia Rais wa Jamhuri, Julius Nyerere “…akisema yeye hakushiriki katika mauaji ya wananchi wale. Hakushauriwa wala hakujua. Lakini aliombwa kujiuzulu kwa kuwa hayo yalitokea chini ya utawala wake.”

Katika kile kinachoonekana kuwa “liwe na liwalo,”  Abdulrahaman Kinana, mmoja wa wajumbe wa CC wanaoheshimika, aliamka na kusema yale ambayo baadhi ya wajumbe wamekiri hawakutegemea kusikia yakitoka kinywani mwake.

“Mwenyekiti, vyama vyote makini vya siasa, vinajali na kuthamini uadilifu wa viongozi wake. Suala la viongozi kutoingia katika mambo yanayochafua uongozi wao, na kutilia mashaka, ni masuala muhimu sana. Yasipoangaliwa yatakiathiri chama, tena vibaya sana,” amenukuliwa Kinana akisema.

Kinana alisema, “Ufisadi upo. Watuhumiwa wa ufisadi wanajulikana. Hivyo basi, wanapaswa kuwajibika.”

Alisema, “Ili tusiendelee kubishana na kubabaishana, ni vema CC na sekretarieti yake vijiuzulu ili kumpisha mwenyekiti kuunda upya kamati kuu.”

Pendekezo la Kinana liliungwa mkono na rais mstaafu Mwinyi aliyesema, “Kwanza, naunga mkono hoja ya Kinana ili kumpa fursa rais kupata wasaidizi wapya.”

Pili, Mwinyi alinukuu msemo wa kiarabu unaosema, “Ukitembea na mlevi, nawe utaitwa mlevi.” Akasema, “Kama kwenye CC kuna mafisadi, basi kuna hatari ya kuathiri hadhi na heshima ya CC.”  

Akihitimisha hoja hiyo iliyoonekana kupunguza, kwa kiwango kikubwa, kasi ya Lowassa ya kuwania urais, mwaka 2015, Kikwete alisema, “Kinana alisema, ‘Sitaki kuwadanganya.’ Nami sitaki mtu anidanganye. Lazima tuimarishe tabia ya wana-CCM kusema ukweli, hasa sisi viongozi.”

Alisema, “Ninaafiki uamuzi wa Kamati Kuu kujiuzulu na sekretarieti yake; na mimi mniachie nitaunda Kamati Kuu nyingine na nitaleta mapendekezo NEC kwa lengo la kuijenga upya CCM.”

Kikwete alihoji “…nani kati yenu anaweza kwenda kwenye mkutano wa hadhara na kusema hakuna ufisadi na wananchi wakampigia makofi?”

Akiongea kwa sauti ya ukali, Kikwete alisema, “Wote watakaotuhumiwa kwa ufisadi, rushwa na ufujaji wa mali ya umma, nawaomba waanze kujiondoa wenyewe kwenye chama chetu. Iwapo hawatajitoa, chama kiwaondoe…”

Wakati wa mjadala katika Halmashauri Kuu, Jumatatu jioni, wajumbe wawili walioongea mwanzo walikubaliana na uamuzi wa kuvunja Kamati Kuu lakini walipendekeza makubwa zaidi. Walitaka watuhumiwa waachie nafasi za uongozi.

Profesa Mark Mwandosya alisema chama kimedhoofika kutokana na tuhuma za muda mrefu za ufisadi, hoja yake ikishindilia hoja za awali kwamba watuhumiwa wajiondoe kabisa katika uongozi.

Naye Makongoro Nyerere alisema watuhumiwa wakuu watatu “washuke kutoka kwenye jahazi kwa kuwa linazama;” akimaanisha Lowassa, Rostam na Chenge.

Makongoro amenukuliwa akisema, “Rostam ni kaka yangu. Kaka yangu Rostam; kaka yangu Lowassa; kaka yangu Chenge, ondokeni jahazi hili linazama kwa ajili yenu…Kikwete ni rafiki yenu…mtaendelea kuwa marafiki lakini katika hili tuachieni…”

Kushindwa kwa Rais Kikwete kutekeleza alichotamani, wameeleza wachunguzi wa mambo ya siasa, “kumewaponza walioongea kwa uaminifu na uadilifu kwa chama.”

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: