Kikwete aanza kutema wanamtandao?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 May 2009

Printer-friendly version
Gumzo
RAIS Jakaya  Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ametupa wanamtandao wake waliomuingiza madarakani miaka minne iliyopita? Hilo ndilo swali ambalo bila shaka wafuatiliaji wa mkondo wa siasa nchini wanajiuliza hivi sasa.

Mashaka ya wengi yanatokana na kimya cha Kikwete katika kipindi hiki ambacho mmoja wa wanamtandao wake muhimu, mfanyabiashara na mbunge wa Igunga Rostam Aziz, anasakamwa na lundo la tuhuma za ufisadi.

Kwa takribani miaka minne sasa, Rostam amekuwa akishushiwa lawama na tuhuma mbalimbali kwamba amehusika na baadhi ya mikataba ya kinyonyaji nchini.

Rostam ametajwa kuhusika katika ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Ametajwa kuwa mbia katika kampuni ya kushusha na kupakia mizigo bandarini (TICS) na mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC).

Kikwete amekaa kimya. Hajasema lolote kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Rostam. Inaonekana ameamua kumuachia mwenyewe zigo la tuhuma, lawama na shutuma.

Kwa mara ya kwanza Rostam kutajwa hadharani kuhusika na ufisadi wa kuangamiza nchi, ilikuwa Agosti 2008. Ni viongozi wa upinzani, wakiongozwa na Dk. Willibrod Slaa, waliomtaja Rostam katika mkutano wa hadahara wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa kumi na moja nchini waliowapachika jina la “watafuna nchi.”

Wiki mbili zilizopita, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi alitaja orodha ya watu watano, Rostam akiwamo, na kuwapachika jina la “Mafisadi papa.”
 
Ni utamaduni wa Kikwete kutetea kila anayemtaka hata kama tuhuma juu yake ziko wazi. Angalau amefanya hivyo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Dk. Idrissa Rashid.

Dk. Rashid alikuwa amejitumbukiza katika mgogoro na malumbano na Bunge, vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali, pale alipong’ang’ana kwamba ni lazima serikali iruhusu Tanesco kununua mitambo chakavu ya kufua umeme kutoka kampuni ya Dowans Holding Limited.

Kikwete alionekana wazi akifanya kazi ya ziada ya kutetea Dk. Rashid. Alisema katika kutekeleza  miradi mikubwa ya umeme, “Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA) isiwe kikwazo.”

Hakuishia hapo. Kikwete alilazimika kutoa hata ufafanuzi wa kile kilichoitwa “kauli tata za Dk. Rashid,” kwamba “ifikapo Oktoba mwaka huu nchi itaingia gizani,” kuwa kauli hiyo haikulenga kuhatarisha usalama wa taifa, bali kueleza hali halisi ya uhaba wa umeme nchini.

Hapa rais Kikwete aliamua “kula mfupa uliomshinda” Ofisa Uhusiano wa Tanesco.

Rais alifika mbali zaidi. Katika moja ya hotuba zake za kila mwezi kupitia vyombo vya habari, alitaka wananchi kufunga mjadala wa Dowans kwa kile alichosema, “mjadala huo hauna maslahi kwa taifa.”

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwa Kikwete kumtetea Dk. Rashid. Awali Kikwete alinyamazia hatua ya Dk. Rashid ya kuandika barua ya kujiuzulu kutokana na madai kuwa aliamrishwa na aliyekuwa waziri mkuu Edward Lowassa kurudisha umeme katika kiwanda cha Tanga Cement.

Tanesco waliamua kukata umeme katika kiwanda cha Tanga Cement kutokana na uongozi wa kiwanda hicho kushindwa kulipa deni kubwa walilokuwa wakidaiwa.

Haya ndiyo wananchi walitarajia kusikia kutoka kwa Kikwete mara baada ya Rostam kuanza kushushiwa tuhuma. Lakini hajafanya hivyo.

Ni kimya chake kinachowafanya wafuatiliaji wa siasa za nchi hii kuhoji iwapo Kikwete amevunja mtandao wake na sasa na ameamua kumuacha kila mmoja lwake.

Ni Kikwete aliyemtetea na ambaye anaendelea kulinda mtangaulizi wake, rais mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na kuhusishwa na baadhi ya tuhuma za ufisadi na utovu wa “utawala bora” wakati wa kipindi chote cha utawala wake – 1995 hadi 2005.

Mwaka 2007, Rais Kikwete aliwaambia waandishi wa habari, alipoulizwa iwapo atachukua hatua dhidi ya Mkapa kufuatia tuhuma alizokuwa akibebeshwa kuwa, “viongozi waliostaafu waachwe wapumzike.”

Hata tuhuma za kuwa na mkono wake (Mkapa) katika ubinafsishaji wa mgodi wa mkaa wa mawe wa Kiwira na mgodi wa chuma wa Mchuchuma zilipozidi kupamba moto, bado msimamo wa Kikwete umeendelea kuwa uleule, “Mwache Mkapa apumzike.”

Lakini Kikwete hajaonyesha kumtetea Rostam, mmoja wa wanachama wake muhimu katika mtandao uliomuingiza madarakani.

Hata Salva Rweyemamu, mkurugenzi wa mawasiliano ikulu ambaye amekuwa na kawaida ya kutetea kila anayetuhumiwa na ufisadi, hata kama si mtumishi wa serikali, katika hili ameamua kukaa kimya.

Salva ambaye aliwahi kutetea kampuni ya kitapeli ya Richmond, ambako Rostam ametajwa kuwa muhusika, hajasema lolote juu ya wanaomtuhumu na kumhusisha Rostam na ufisadi.

Je, kwa tabia ya sasa ya Kikwete na Mkurugenzi wa Mawasiliano ikulu, yawezekana Kikwete “amejiengua” katika kundi la wanamtandao wake?

Ingawa serikali ya Kikwete haijachukulia Rostam hatua za kisheria, lakini kule  kukaa kimya kwa Kikwete na kuachia wananchi kumsulubu watakavyo, kunaonyesha wazi kuwa Kikwete sasa “amejitenga” na kundi lake.

Hata Mustafa Mkullo, waziri wa fedha wa sasa, amewahi kutetewa na Kikwete pale alipotuhumiwa kubeba Kagoda na wakwapuaji wengine wa EPA.

Mkullo alisema “fedha za EPA” zilizokwapuliwa na wachache kwa kusaidiwa na maofisa wa serikali, hazikuwa za umma, bali zilikuwa ni fedha za wafadhili. Kauli yake ilileta zogo hadi bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Kikwete aliamua kufa na Mkullo pale aliposimama hadharani kumtetea na kwa kurudia kauli ya waziri wake, kuwa fedha za EPA si za serikali. Alilazimika kuchukua  uamuzi huo mgumu ili kumwokoa Mkullo na shinikizo la Bunge.

Baadhi ya wabunge walikuwa wanazungumza bila kutafuna maneno, “Mkullo awajibike kwa kujiuzulu” kutokana na kauli yake ya kutetea ukwapuaji katika EPA.

Kikwete angalau alijaribu pia kumlinda hata Andrew Chenge anayetuhumiwa kwa rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi. Akiongea na Watanzania nchini Uingereza, Kikwete alisema serikali yake inaachia Uingereza kuchunguza sakata la rada.

Alisema ni ajabu kwa nchi tajiri kama Uingereza, ambako kuna kampuni ya BAE iliyouza rada kwa bei kubwa kupindukia, kuiibia nchi masikini kama Tanzania. 

Sasa swali la kujiuliza ni nini kimesababisha Kikwete kuvunja au kusaliti wanamtandoa wenzake? Jibu liko wazi, kwamba mtandao uliomuingiza madarakani ulikuwa na dhamira na malengo tofauti.

Kuna wale walioamini kuwa “maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.” Wafuasi wa itikadi hii waliamini na bado wanaamini mpaka sasa kwamba hilo linawezekana na linatekelezeka.

Lakini kuna wale waliokuwa wanahubiri wimbo huo midomoni tu, huku wakitenda kinyume. Kuna madai kwamba Rostam ni miongoni mwao.

Ndiyo maana mara baada ya Kikwete kuingia madarakani zimeibuka shutuma nyingi zinazomhusisha Rostam.

Kwamba Rostam hakuingia katika kambi ya Kikwete ili kuendeleza kauli mbiu ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania,” inaweza kuthibitishwa na mlolongo wa matukio ya sasa na ya huko nyuma.

Mwaka 1995 mara baada ya Kikwete kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya chama chake na Benjamin Mkapa, Rostam alirudi Dar es Salaam usiku wa manane, haraka akajiunga na kambi ya Mkapa ambako alifanywa kuwa mwekahazina wa kampeni zake.

Wakati huo, Kikwete na marafiki zake wa karibu, walikuwa bado wanaendelea kujiliwaza na kufuta machozi baada ya mgombea wao kushindwa.

Rostam alijipenyeza kwa Mkapa kupitia kwa Balozi Ferdinand Ruhinda. Hatimaye Ruhinda na Rostam wakawa wanahisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom na waanzilishi katika kampuni ya Mwananchi inayochapisha magazeti ya Mwananchi Communication Ltd., The Citizen na MwanaSpoti.

Hakuna uhakika kama Kikwete alikuwa anayajua haya. Pengine hakumfahamu kwa undani. Lakini baada ya kuingia madarakani na kuwa na vyombo vinavyomulika kila pembe, ndiyo maana ameamua kukaa kimya na kwa kutumia methali ya Kiswahili, “pilipili usiyoila yakuwashia nini?”

Kimya cha Kikwete kina jambo. Jambo hilo ni ama ameshindwa kumsaidia Rostam kutokana na tuhuma nyingi zinazomkabili au ameamua Rostam ajiokoe au ajinyonge mwenyewe bila kuhusisha urais.

Kwa mwendo huu, safari yaweza kutabirika: Rostam kukiri na “kuongoka” au kufa akipigana, ambao ni mkondo pekee kwa aliyetemwa na kinara wa mtandao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: