Kikwete achemka


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Nyaraka za serikali zamuumbua
Wasomi, TUCTA wamshangaa
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ameelezwa kuwa ni dikteta, asiyetii sheria, asiyesema ukweli na aliyepotoshwa na wasaidizi wake, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwanza, nyaraka za majadiliano kati ya serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), hazionyeshi serikali kukosa uwezo wa kulipa wafanyakazi mshahara wanaopendekeza.

TUCTA inataka serikali kulipa kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma Sh. 315,000 kwa mwezi.

Katika nyaraka za majadiliano, serikali inajitapa kuwa makini katika ukusanyaji wa kodi kwa kila mlipa kodi nchini, hasa wafanyabiashara wakubwa.

Majibu hayo ya serikali yametokana na malalamiko ya TUCTA, kuwa serikali ni dhaifu katika kukusanya kodi kwa wafanyabiashara ambao wengi wao hukwepa kodi au hupewa misamaha.

TUCTA inatuhumu serikali kukamua wafanyakazi kwa kuwafanya “…kuwa eneo kubwa pekee la kulipa kodi za juu wakati wafanyabiashara wakilipa kodi ndogo na wakati mwingine kukwepa.”

Malalamiko hayo yalikuwa katika ajenda ya pili ya majadiliano yalioishia 6 Aprili 2010. Ajenda ya kima cha chini cha mshahara ilishafungwa na tena bila kukubaliana.

Waliotia saini majadiliano hayo ni Nicolas Mganya kwa niaba ya TUCTA, Abraham H. Senguji kwa niaba ya serikali na Cosmas Msingwa kama msuluhishi.

Pili, watu mbalimbali waliohojiwa mara baada ya hotuba ya rais kwa “wazee wa CCM” wa mkoa wa Dar es Salaa juzi, walieleza kutoridhishwa na mantiki katika kauli za rais.

Wakili Mabere Marando wa Dar es Salaam amesema rais hawezi kuzuia mgomo. Amesema kikatiba, mahakama ndiyo imepewa kazi hiyo kwa vile hufanya maamuzi baada ya kusikiliza pande zote zinazokinzana.

“Rais hawezi kubatilisha mgomo. Hilo ni kosa. Yeye ni serikali, kwa hiyo kwenye hili ana upande. Mahakama pekee ndiyo inaweza kutenda haki kwenye hili,” alisema.

Marando alisema asingeweza kutoa maoni yake kuhusu hotuba ya Kikwete kwa ujumla kwa vile hakuwa ameisikiliza yote.

Mchungaji Christopher Mtikila, amesema hotuba ya rais imekuwa ya vitisho kwa wananchi.

Amesema, “sasa hatuna rais. Naona tuna amiri jeshi mkuu. Badala ya kusikiliza wafanyakazi, yeye anawatisha.”

Kiongozi huyo wa chama cha siasa cha DP amesema, “Tunaona anataka kutumia jeshi kutishia wafanyakazi waliotumia jasho lao kwa ajili ya nchi hii.”

Katika lugha yake ya ukali na ushawishi, Mtikila alisema, “Wafanyakazi wanadai wanachostahili. Sasa kama rais anatishia, vema wananchi sote tuandamane tuone kama risasi zake zinaweza kutumaliza wote.”

Naye, Mgaya amesema kuwa kimsingi chama chake kimesikitishwa na kauli za rais.

“Huyu bwana ametumia vitisho kwa wafanyakazi na kuonyesha udikiteta. Lakini sisi wafanyakazi hatutishwi kwani tunajua wajibu wetu. Hata rais anachaguliwa na wafanyakazi,” amesema.

Katibu huyo amesema, “Kwanza, kwa mujibu wa sheria, rais hana mamlaka ya kuzuia mgomo. Mgomo unaweza kuzuiwa na Mahakama ya Kazi ambayo imepewa uwezo wa kisheria wa kutamka iwapo mgomo huo ni halali au batili.”

Alisema kama serikali ilitaka kubatilisha mgomo, ilitakiwa kuwasilisha maombi mahakamani kupinga kuwapo kwa mgomo.

Aidha, Mgaya amesema rais amepotosha umma kwa kusema kwamba mazungumzo kuhusu mishahara ya wafanyakazi inaendelea, kwani hilo lilikwisha kufungwa.

Amesema badala yake, kinachoendelea sasa ni majadiliano kuhusu namna ya kupunguza makato ya wafanyakazi hao kwenye mifuko ya jamii.

“Sisi hatujui ni kwa nini rais aliamua kusema alichokisema. Mjadala kuhusu mshahara umefungwa. Kinachoendelea ni kuhusu mambo mengine kabisa. Sasa hatujui lengo la rais lilikuwa nini kwa maneno yake yale,” amesema.

Katika mkutano wake huo na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Rais Kikwete alilitaja jina la Mgaya zaidi ya mara tatu, na kiongozi huyo wa TUCTA ameliambia MwanaHALISI kwamba ameshangazwa na hatua hiyo ya rais; ingawa “imeniongezea umaarufu.”

Wakati hayo yakiendelea, TUCTA imetangaza kusitisha mgomo wake kusubiri mkutano wa majadiliano wa tarehe 8 Aprili mwaka huu.

Aidha, taarifa zinasema kinyume na maelezo ya rais Kikwete, kwamba TUCTA imekuwa ikichelewa vikao vya majadiliano, barua ya mwaliko inaonyesha kuwa rais hakusema ukweli.

Barua ya serikali iliyotumwa kwa TUCTA kuwataka kuhudhuria mkutano yenye Kumb. Na. TYC/B/280/69 ya tarehe 22 Aprili 2010 inaonyesha kuwa TUCTA walitakiwa kufika kwenye kikao saa nane na nusu mchana.

“Nimeagizwa nikualike tarehe 23/04/2010 saa 8:30 mchana ili uwasilishe mada yenye hoja ya shirikisho la wafanyakazi inayohusu kodi wanayotozwa wafanyakazi,” inasema barua ya serikali iliyosainiwa na Shogholo C. Msangi kwa niaba ya katibu mkuu wa hazina.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Kikwete alisema mgomo unaoshinikizwa na viongozi wa TUCTA ni “batili” na “kinyume cha sheria.”

Alituhumu viongozi wa TUCTA kuwa ni waongo na kwamba hawahudhirii vikao vya majadiliano kama wanavyotakiwa na serikali.

Aliwataka wafanyakazi kutoandamana, akitishia kuwa watakaoandamana wanaweza “kutwangwa” na polisi wanaotumia mabomu ya machozi, risasi bandia na hata risasi hai.

Alikejeli kuwa hata wakiandamana, itabidi warudi kwenye mazungumzo na labda wakati huo wakiwa na “plasta” kichwani.

Akiongea kwa ukali, Kikwete alisema, sheria ya ajira na mahusiano kazini, inaainisha, pamoja na mambo mengine, majadiliano kazini, maslahi ya wafanyakazi, mwajiri na maslahi ya wananchi.

Rais alisema makubaliano binafsi ya wafanyakazi hayawezi kukubaliwa kuumiza wengine na kwamba wafanyakazi wasilazimishwe kugoma kwa maslahi ya watu wasiowafahamu.

Alisema hata wafanyakazi wakigoma, mshahara huo haupo. Alisema anayeona hawezi kufanyakazi na serikali kwa mshahara wa sasa, basi aache kazi.

Alisisitiza, “Tusipoteze muda kudai kisichowezekana, hamtakipata.”

“Ahadi yangu iko palepale, tutaendelea kupandisha mishahara ya wafanyakazi. Nisikilizeni mimi. Msimsikilize Mgaya. Huyu ana ajenda yake” alisema Kikwete.

Tatu, kuhusu agenda ya tatu ya maboresho ya mishahara, alisema wao walitaka kima cha chini kiwe Sh. 315,000, lakini serikali ikataka kiwe Sh. 135,000, jambo ambalo hawakuafikiana.

Amiri jeshi mkuu alisema nchi ina wafanyakazi karibu 350,000 lakini ina watu milioni 40. Alisema wanachotaka wafanyakazi ni kupewa chote na “sisi tutelekeze watu milioni 40.”

Rais Kikwete alisema serikali ikikubaliana na madai ya wafanyakazi, italazimika kulipa kiasi cha Sh. 6.9 trilioni kwa mwaka.

Alifanya hesabu kuwa wafanyakazi 350,000 wakilipwa Sh. 315,000 kila mmoja kila mwezi kwa mwaka, serikali itakuwa imelipa Sh. 6.9 trilioni wakati mapato ya serikali kwa mwaka wa fedha uliopita ni Sh. 5.8 trilioni.

Hata hivyo, MwanaHALISI limegundua kuwa hata kama wafanyakazi wa serikali watakuwa 500,000 na kila mmoja akalipwa kiasi cha Sh. 500,000, serikali itatumia kiasi cha Sh. 3 trilioni tu kwa mwaka.

Bado kiasi hiki cha kulipa watu wengi kwa kiasi kikubwa, ni kidogo kwa Sh. 3.9 trilioni kwa mwaka ikilinganishwa na “hesabu za ikulu.”

Wachunguzi wanasema ama serikali imekosea hesabu au imetoa takwimu hizo kwa makusudi kukidhi matakwa ya kisiasa.

Katika hali ambayo haikutegemewa, Rais Kikwete alisema kama madai ya wafanyakazi ni shinikizo kwake ili wampe kura kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, basi hahitaji kura zao.

Aliwaita viongozi wa TUCTA kuwa waongo na wanafiki kwa kusema serikali yake haiambiliki na kwamba ndio maana alichagua kujibu hotuba zao za Mei Mosi kwenye sherehe ambazo hakualikwa.

Kikwete alituhumu viongozi wa TUCTA kuwa na ajenda zao za siri ambazo alisema zinalenga zaidi kisiasa.

Mwaka huu chama cha wafanyakazi kilikataa kumwalika rais kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani. Hii ni mara ya kwanza kutofanya hivyo katika historia ya Tanzania.

Akionekana kutaka kulitupa zigo la wafanyakazi kwa wapinzani wake wa kisiasa, Kikwete alisema, wanayo kila sababu ya kuhoji dhamira za viongozi wa TUCTA na kwamba wana lao jambo.

Kauli hiyo ilichukuliwa kama majibu kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa ambaye siku ya Mei Mosi aliishutumu serikali kwa kutosikiliza vilio vya wananchi.

Hatua ya wafanyakazi inachukuliwa na wachambuzi wa mambo kuwa mtihani mkubwa kwa Rais Kikwete na serikali yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: