Kikwete ageuka zigo CCM


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KABLA ya Yusuf Makamba kung’olewa ukatibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikuwa na msemo wa kumsifia Rais Jakaya Kikwete akisema, “Kikwete ni mtaji wetu.”

Makamba ambaye baadaye aligeuzwa gamba la kwanza kuondolewa, alikuwa na maana kuwa Kikwete ni mtaji wa chama chake.

Lakini kwa maoni ya wengi sasa, Kikwete amegeuka mzigo mkubwa ndani ya chama na serikali, tofauti na majigambo ya awali ya Makamba na wenzake. Hata Makamba wa sasa – January, ambaye ni mtoto wake, anaweza kumzungumzia tofauti Kikwete wa sasa na yule wa awali.

Wa sasa anazungumza bila kupima athari ya anachokizungumza. Miongoni mwa matamshi ya Kikwete ambayo yamegeuka mzigo kwa chama chake na kumwondolea sifa ya kuitwa “mtaji wa chama,” ni maelezo yake kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema alikuwa tayari kukosa kura za wafanyakazi kuliko kuwaahidi mishahara minono.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Kikwete alimtaja mara saba Nicholaus Mgaya kana kwamba tatizo la mishahara ya wafanyakazi lilikuwa tatizo binafsi la Mgaya.

Hii inaonyesha wazi kuwa kauli ya rais halikuwa jambo aliloshauriana na wenzake kabla ya kulisemea.

Kauli nyingine tata aliyoitoa Kikwete inayomfanya aonekane mzigo kwa chama chake, ni ya kudai kuwa baadhi ya viongozi wa kidini walijiingiza kwenye siasa. Kauli hiyo ilisababisha umaarufu wake mbele ya wananchi kupungua.

Kauli hii ilifuatiwa na harakati za CCM kufanya mikutano wilaya zote nchini kujichunguza kwa nini kura za “kiongozi wao mpendwa” zilipungua. Wengi tulisikia na kuambiwa kwamba udini ulichangia.

Hadi leo, hatujaambiwa ilikuaje Kikwete ambaye ni muislam alipata kura nyingi kuliko Dk. Willibrod Slaa mkiristo katika mikoa yenye wakristo wengi kama Ruvuma, Kagera, Morogoro, Singida na Mbeya! Hii peke yake ni sababu tosha kuwa tathmini ya CCM ilikosa mashiko.

Rais Kikwete kwa sasa anawapa kazi ngumu watetezi wake baada ya kutoa kauli nyingine tata na isiyo na mashiko ya kuwaomba wenzake katika chama kujivua gamba.

Kama vile amesahau ni yeye mwenyewe aliwainua majukwaani – hata wale waliotuhumiwa kwa ufisadi – na kuwapigia debe.

Eti chama tawala kimekosa mvuto kwa vijana na hivyo kinapaswa kujivua gamba ili kipendwe na vijana. Nini?

Nikiri kwamba sielewi kujivua gamba kutaisaidiaje CCM kupata umaarufu kwa vijana wakati siku zote zinatolewa kauli tata na za kinafiki. Je, kijana gani atayemwamini mnafiki?

Iweje leo mwenyekiti atake wenzake katika CCM wajivue gamba kwa kuwatosa watu ambao yeye mwenyewe aliwatetea jana akidai hakuna ushahidi wa kuwachukulia hatua za kisheria?

Kabla ya uchaguzi wa 2010 tulielezwa kuwa hakuna ushahidi wa kuwajibisha wanaodaiwa kuhusika na kashfa za EPA, Meremeta, Richmond/Dowans, rada na ndege ya rais tunayoambiwa inatua viwanja vitano tu nchini.

Elimu hii kuwa hakuna ushahidi ilifuatiwa na taarifa za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwamba kashfa kadhaa zimefanyiwa uchunguzi na penye ushahidi wa kutosha watapelekwa mahakamani, lakini mpaka leo wananchi wanaendelea kusubiri.

Kama hiyo haitoshi, kabla ya watetezi wa Kikwete kupata majibu ya hoja za wanaohoji umakini wake, yeye amekuja na kauli nyingine tata.

Alipokaribishwa katika hafla ya kumsimika askofu mjini Songea wiki mbili zilizopita, aliamuru maaskofu waache kuuza madawa ya kulevya (unga).

Kauli hii ya maaskofu kuuza unga ilifuatiwa na vipindi vya televisheni kwenye TBC vilivyoandaliwa kuhalalisha hoja hiyo. Katika moja ya taarifa hizo, walionyeshwa vijana walioathirika na madawa ya kulevya wakieleza kuwa madawa hayo huingizwa nchini na viongozi wa dini.

Mimi naungana na wale wanaosema rais wetu huwa hatafakari kwa pamoja na washauri wake kauli anazolenga kwenda kuzitoa hadharani.

Chukulia mfano wa hoja hii madawa ya kulevya. Hata kama kweli askofu mmoja au wawili wamewahi kuhusika, kauli yenyewe kaitolea wapi?

Wewe unakwenda kwenye mkutano wa maaskofu na waumini wao kumsimika askofu halafu unawaambia maaskofu hao waliokualika kuwa ni wauza madawa ya kulevya tena maneno yenyewe unayasema mbele ya waumini wao?

Na madai haya ya maaskofu kuuza unga unayasema leo wakati jana ulisema maaskofu walihusika katika kampeni chafu dhidi yako na kwamba walisababisha umaarufu wako upungue hata ukapata asilimia 60 chini kabisa ya asilimia 90 za mwaka 2005!

Sasa, kama Rais Kikwete hakuambiwa na washauri wake au kama hakufahamu uzito wa madai yake, najitolea kumwelimisha. Maana ya madai yake ni mbaya sana sawa na madai kuwa ‘Yesu si Mungu’ yakitolewa sokoni. 

Maana ya madai yale ya maaskofu kuuza unga kutolewa mbele ya waumini wa kikristo ni sawasawa na kuwaambia waumini hao kwamba “ninyi wakristu msiwafuate viongozi wenu hawa kwa sababu wao si lolote si chochote bali wauza unga.”

Madai haya, hata yangekuwa na ukweli kiasi gani, yanamaanisha kashfa na matusi dhidi ya waumini hao, familia na rafiki zao. Umetukana mke, ndugu, mtoto wa askofu mbele yao.

Kueleza kuwa maaskofu wanauza unga ni sawa na kuwakashifu au kuwavunjia heshima mbele ya waumini wao na familia zao.

Mwambie Mhaya mambo ya kumkashifu mbele ya mkewe uone. “Wangambira stupid infront of my wife” ndivyo utajibiwa. Hao ni Wahaya. Bali kauli yenye maana hiyohiyo itatolewa na mtu yeyote atakayekashifiwa namna hiyo mbele ya wale anaojua wanamheshimu.

Alichokifanya rais ni sawa na kuwazuia waumini kutoa sadaka na zaka makanisani kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kuwawezesha wauza unga kwa kuwapa pesa wapate nauli ya kusafiria Ulaya na Marekani kufanya biashara ya unga.

Mimi sijawahi kuona mtu amekaribishwa mahali, badala ya kutoa ahadi za ushirikiano na kusifia ushirikiano katika mambo yaliyopita, akaanza kutusi waliomkaribisha. Diplomasia ya aina hii ni mpya kwangu.

Niseme kutoka rohoni kabisa kwamba kiongozi anayelalamikiwa kutodhibiti mafisadi, aliyeshindwa kutumia vyombo vyote vya dola kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahusika wa kashfa za kampuni ya Kagoda Agriculture, Meremeta na Deep Green hapaswi kutuhumu mtu.

Amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama wakiwemo polisi, usalama wa taifa, jeshi na hata TAKUKURU, ambaye serikali yake imeshindwa kuwaambia wananchi wake kuwa mmiliki wa Kagoda ni nani, hakutarajiwa kabisa kurusha kombora kwa maaskofu.

Ni muhimu Rais ajue kuwa kila kauli moja potofu anayoitoa, kila tuhuma isiyo na mashiko na kila hoja muflisi anayoitamka, inapandisha chati wapinzani wake kisiasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: