Kikwete na ahadi za matrioni


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Jakaya Kikwete, mgombea Urais tiketi ya CCM

RAIS Jakaya Kikwete ameanza ngwe nyingine ya kuzunguuka nchi katika harakati zake za kuwania muhula wa pili wa uongozi.

Katika mzunguko wa kwanza ulioanzia mkoani Dar es Salaam, Kikwete amefika katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Kigoma, Rukwa na Mbeya. Kote alikopita, ameacha lundo la ahadi.

Mkoani Kagera, kwa mfano, mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kununua meli mpya ya abiria ili kufidia meli iliyozama miaka 14 iliyopita – Mv Bukoba.

Janga hilo lililotokea 21 Mei 1996, watu zaidi ya 1,000 walifariki dunia; mamia ya wengine walibaki wajane, wagane na wengine kadhaa wakabaki yatima.

Tangu wakati huo, hakuna kiongozi yeyote wa serikali na CCM aliyezungumzia ununuzi wa meli mpya, ama umuhimu wa urejeshaji wa huduma za usafiri katika eneo hilo, kutokana na huduma kuzorota.

Mtangulizi wa Kikwete, rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye wakati janga hili linatokea alikuwa na mwaka mmoja madarakani, amemaliza kipindi chake cha miaka 10 bila kununua meli mpya.

Mbali na Mkapa kushindwa kununua meli mpya, alishindwa hata kulipa fidia wahanga wa ajali hiyo.

Naye, Kikwete amemaliza kipindi chake cha kwanza cha uongozi bila kununua meli mpya, au kuzungumzia suala hilo.

Pamoja na kwamba Kikwete amewahi kutembelea mkoa wa Kagera mara kadhaa, lakini hakuwahi kusema mahali popote, kwamba serikali italipa fidia wahusika.

Kingine ambacho Kikwete ameahidi wananchi wa mkoa wa Kagera, ni ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa Kimataifa wa Bukoba.

Hata hivyo, Kikwete hakusema serikali itapata wapi mabilioni ya shilingi yanayohitajika kugharamia ujenzi wa uwanja mpya?

Wala hakusema kama serikali imeshindwa kujenga uwanja wenye hadhi katika jiji kuu kama Dar es Salaam, itawezaje kujenga uwanja wa kisasa?

Kingine ambacho Kikwete ameahidi, ni kuwarejesha katika makazi yao ya asili wananchi wa vijiji vya Kakunyu, Bubale, Bugango na Byeju, wilayani Misenyi, waliohamishwa kwa nguvu na serikali.

Maefu ya wananchi hawa walihamishwa ili kupisha mmiliki wa ranchi ya Kakunyu kufanya shughuli zake bila usumbufu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni, Kikwete alituhumu viongozi wa mkoa wa Kagera kwa kile alichiota, “kumpa taarifa zisizo sahihi.”

Alisema viongozi hao walimueleza kuwa eneo hilo la Kakunyu halina makazi ya binadamu, bali wanaoishi humo ni wanyama pekee.

Kwanza, hatua ya rais kukiri kudanganywa na wasaidizi wake, inathibitisha madai ya wapinzani wake wa kisiasa kwamba Kikwete si makini.

Pili, kwa mujibu wa katiba ya CCM, yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa vikao vya uteuzi – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa wagombea ubunge na udiwani.

Hivyo basi, kama alijua alidanganywa na wasaidi wake, asingekubali kumtosa mbunge wa Nkenge, Deodorus Kamala.

Kwa mujibu wa Kikwete, kushindwa kwa Kamala katika kura za maoni ndani ya chama chake, kumetokana na msimamo wake wa kutetea wananchi.

Tatu, rais wa Jamhuri ndiye anateua wakuu wa mikoa na wilaya. Je, amechukua hatua gani kwa wasaidizi wake waliomdanganya? Jibu ni moja: Hakuna!

Nne, matamshi ya Kikwete kumsafisha aliyeshindwa katika kura za maoni, yanaweza kuwa na tafisiri moja: Kwamba ni muendelezo wa ukiukaji wa maagizo ya NEC iliyotaka kuzikwa kwa makundi yaliyotokana na kura za maoni.

Jingine ambalo aliahidi ni kuimarisha mradi mkubwa wa umeme. Amesema mradi huo, utagharimu zaidi ya dola za Marekani 1.6 bilioni.

Kama ilivyokuwa katika miradi mingine, Kikwete hakusema fedha za kutekeleza miradi hiyo zitatoka wapi. Hakusema, kama serikali inashindwa kutosheleza Dar es Salaam kwa umeme, itawezaje kumaliza tatizo la umeme mikoani.

Ahadi nyingine, ni kupanua uwanja wa ndege wa Bukoba mjini ili uweze kupokea ndege kubwa. Hapa napo hakusema, fedha za ujenzi na zinazohitajika kulipa fidia wananchi wanaozunguuka uwanja, zitatoka wapi.

Inawezekana anataka serikali kuhamisha wananchi bila kulipa fidia.

Katika mkoa wa Mwanza, Kikwete ameahidi kulipa ya madeni chama cha ushirika cha Nyanza.

Lakini hakueleza waliofilisi ushirika huu uliokuwa tegemeo la wakulima wako wapi; wamewachukua hatua gani na lini watachukuliwa hatua?

Kama serikali imeshindwa kufikisha watuhumiwa mahakamani, kuna sababu zipi za msingi serikali kubebesha wananchi deni hili?

Nani anaweza kuhakikishia wananchi, kwamba fedha zitakazotolewa zitatumika kufufua ushirika?

Mkoani Mbeya, nako wameshibishwa ahadi. Kwanza, ameahidi kukamilisha, uwanja wa ndege wa Songwe. Pili, ameahidi kuwapa bajaji 400 zitakazotumika kwa wajawazito!

Awali ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe ulipangwa kukamilika miaka sita iliyopita. Lakini kutokana na vita ya urais kati ya wanamtandao wa Kikwete na wafuasi wa Profesa Mark Mwandosya, mradi huu ukahujumiwa.

Taarifa zinasema, mpaka sasa wapo baadhi ya viongozi wa mkoa na taifa, waliojipiza kuwa uwanja huo hautamalizika, hadi mwaka 2015.

Wanadai hatua yeyote ya kumaliza uwanja sasa, itakuwa mtaji mkuu kwa Mwandosya katika mbio zake za kutaka kurithi urais kutoka kwa Kikwete.

Katika baadhi ya maeneo, mengi yaliyoahidiwa hayakuwa katika ilani ya uchaguzi. Ndiyo maana wengine wanatilia shaka kile kilichoahidiwa.

Tatizo kubwa la serikali ya Kikwete, ni kushindwa kutambua vipaumbele vyake. Je, kipi kianze, kujenga barabara, au kununua magari ya kifahari:

Je, serikali ianze na kuimarisha elimu ya msingi, kati na juu au ianze na Kilimo Kwanza.

Serikali makini lazima ingefanya utafiti na kugundua kuwa ni bora kuimarisha vituo vilivyopo, kuliko kuanzisha mikoa mipya ya polisi.

Ingefahamu kuwa mikoa mipya itahitaji magari ya viongozi, ofisi za kisasa zilizosheheni viyoyozi, nyumba zenye hadhi ya cheo cha kamanda wa mkoa aliyeteuliwa.

Ingefahamu lipi lianze, kati ya kuagiza magari ya kifahari kwa ajili ya kubebea viongozi, ama kununua magari aina ya Land Rover yatakayoweza kutumika kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

Lipi lianze kati ya kununua gari lenye thamani ya Sh. 200 milioni litakalotumiwa na mganga wa hospitali ya wilaya, kutumia Sh. 80 milioni kununua gari la hospitali litakalotumika kubebea wagonjwa.

Kushindwa kutambua vipaumbele hivyo, ndiyo chimbuko la kuibuka kwa ahadi kila uchwao. Je, Kikwete ataweza kutekeleza haya yote yanayohitaji trioni za shilingi? Tusubiri tuone!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: