Kikwete aikosesha CCM jeuri ya mwaka 1995


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 August 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MWAKA 1995 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa na jeuri. Baada ya mkutano mkuu kumteua Benjamin Mkapa kuwa mgombea urais wake, na Mwalimu Julius Nyerere akapita kumnadi, hofu ya kushindwa ilifutika.

Ndiyo maana lilipotolewa pendekezo la kuandaliwa kwa mdahalo kwa wagombea urais, hawakuwa na wasiwasi.

“Mgombea wetu, yuko tayari iwe sasa, kesho, usiku au mchana,” alisema kwa jeuri kabisa, katibu wa uenezi Kingunge Ngombale-Mwiru nilipomuuliza mwanasiasa huyo mkongwe. Wakati ule nilikuwa gazeti la Uhuru.

Aliongeza, “Tena mgombea wetu yuko tayari kwa lugha yoyote; Kiswahili, Kiingereza au Kifaransa. Sasa nenda kawaulize, na wao wamejiandaa kwa Kiingereza na Kifaransa?”

Kingunge alikuwa anatambia uwezo wa Mkapa ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hakujulikana sana kwa wananchi, lakini pia hakuwa na doa la kisiasa.

Swali la Kingunge “kawaulize na wao wamejiandaa kwa Kiingereza” lilimlenga aliyekuwa mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi, Augustine Lyatonga Mrema, ambaye alivuma sana. Hakuwa na elimu ya Chuo Kikuu na kwa hiyo lugha hiyo ya Malikia Elizabeth inadaiwa haikuwa inapanda.

Siku ya mdahalo ikafika. Katika mdahalo ule uliofanyika Hoteli ya Kilimanjaro (Leo Kilimanjaro Kempiski), Mkapa alionyesha uelewa mkubwa na alishawishi watu kwamba anaweza kuaminiwa Ikulu.

Mwelekeo wa nani atakuwa rais ulionekana pale na kura za Mrema aliyekuwa anapewa nafasi kubwa kushinda zilipungua. Mrema aliwaangusha wafuasi wake.
Kwa nini? Takriban mwezi mzima wasomi wa NCCR -Mageuzi Mabere Marando, Dk. Masumbuko Lamwai, Prince Bagenda nk walikuwa wakimfundisha mambo muhimu ya kuzungumza katika mdahalo, lakini ilipofika siku yenyewe akawa hajahitimu.

Mrema aliishia kueleza historia yake; alivyokamata almasi uwanja wa ndege, alivyosuluhisha ndoa za watu nk lakini hakuwa na ubavu wa kuelezea masuala ya kiuchumi na maendeleo ya wananchi.

Mgombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Prof Ibrahim Lipumba alijieleza vizuri ila aliathiriwa na hila za CCM waliokichafua chama hicho kwamba kimejaa Chuki, Udini, Fitina. John Momose Cheyo wa United Democratic Party (UDP) alifurukuta bila malengo.

Baadaye Cheyo, akiwa amezama katika lindi la mawazo wakati wa chakula alizinduka na kusema; “After all, I am a business man” (isitoshe mimi ni mfanyabiashara).

Na wakati wa uchaguzi alipokosa kura hata kwenye kijiji chake, mwelekeo wa siasa wa Cheo ulibadilika akaanza kuamini kwamba haiwezekani kuishinda CCM. Kwisha!

Mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara katika mkoa wa Shinyanga, Cheyo alimumwagia sifa kiongozi huyo wa kitaifa akisema hakuna wa kushindana naye. Msimamo huo anao hadi leo.

Wenye fikra kama hizo ni pamoja na Mrema ambaye sasa anapita kila mahali kumpigia debe JK ilhali chama chake cha TLP kimemteua na kumpitisha Mutamwega Mugayuwa. Mrema yuko TLP kimwili, kifikra yuko CCM kama Cheyo.

Mwaka 2005, TPP Maendeleo ilifanya kichekesho kama hicho. Kilimteua mgombea kiti cha urais mwanamke, Anna Senkoro lakini mwenyekiti wake, Peter Kuga Mziray alikuwa shabiki mkubwa wa Kikwete. Kwa hasira ya kutoswa Senkoro amerudi CCM.

Mwaka 1994 Mchungaji Christopher Mtikila wa DP alialikwa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aeleze sera zake. Alipotaka kujieleza kwa Kiswahili fasaha ili wanafunzi wamwelewe vizuri, wakamwambia “English please”.

Aah! Mtikila alimwaga ung’enge na baada ya mkutano ule wanafunzi walimbeba juujuu hadi kwenye gari lake. Mtikila wa wakati ule alikuwa anahutubia na unapata msisimko. Alipohutubia umati wa watu Jangwani, akiita Wahindi magabacholi, watu waliondoka na kwenda kuvunja magari ya Wahindi Kariakoo.

Leo vipi? Mtikila wa leo amebadilika amekuwa ‘friendly fire’ yaani risasi inayofyatuka na kuua ndugu zake wa upinzani. Mtikila ni adui wa kambi ya upinzani kuliko hata CCM.

Sababu ni moja tu, analipa fadhila za kibopa mmoja wa CCM aliyechangia kanisa lake na inadaiwa amesaidiwa kulipa deni asifungwe. Sasa anaachia friendly fire.

Aliwahi kugombea kiti cha ubunge kupitia CUF katika uchaguzi mdogo wa Ludewa, aliposhindwa alidai CUF wana mapepo.

Katika uchaguzi mdogo Jimbo la Tarime kujaza nafasi ya Chacha Wangwe, Mtikila alikuwa ‘beneti’ na Yussuf Makamba kuinanga CHADEMA. Kwa hiyo, haishangazi kusikia ameapa kummaliza Dk. Willibrod Slaa.

Huo ndio mwelekeo wa upinzani, kila ukipiga hatua fulani ya mafanikio unakumbwa na friendly fires chini ya usimamizi wa CCM.

Nimeeleza haya ili vijana wajue kwamba baadhi ya viongozi wetu kama Mtikila, Mrema, Mziray, Cheyo ni friendly fires kwa upinzani. Kwa lugha nyepesi hawa ni wapinzani wanaohujumu upinzani.

Kwa hiyo, ukiwepo mdahalo leo kama walivyoomba CUF, wajue watakabiliwa na changamoto nzito kutoka friendly fires na siyo CCM ambayo imesema haitaki.

Rais Kikwete alimjibu Prof. Lipumba mjini Dodoma: “Tutakutana jukwaani”. Makamba alipigilia msumari hivi karibuni akisema Rais hatafutwi kwa mdahalo.
Siri nyuma ya majibu hayo ni kwamba CCM hawana ujasiri waliokuwa nao CCM mwaka 1995.

Sababu za kuukataa zipo. Mwaka 1995 Mkapa hakuwa na doa lolote kisiasa wala kiutendaji ndiyo maana CCM haikuwa na shaka. Isitoshe Mkapa alikuwa mteule wa Baba wa Taifa.

Lakini miaka mitano ya utawala wa Rais Kikwete (2005-2010) imemwacha majeruhi wa ahadi zake. Aliomba apelekewe orodha ya mafisadi, wala rushwa, wauza unga na wahalifu wengine, lakini majina yamebaki kwenye mashubaka ya ikulu.

Ameshindwa kuwasaidia wapambanaji wa ufisadi na amewakumbatia mafisadi; wmeshindwa kuwachukulia hatua vigogo wenye kashfa mbalimbali; ufisadi katika ununuzi wa ndege ya rais, uidhinishaji kampuni tata ya Richmond kwa ajili ya kufua umeme wa dharura, ujenzi duni wa shule za sekondari za kata, safari zisizo na tija, kukataa kuwapa nyongeza wafanyakazi, kubagua watu wa kuwashtaki kati ya waliokwapua pesa za EPA nk.

CCM wanapotazama yote hayo katika kipindi hiki ambacho kila kona ya nchi inalalamikia uongozi na utawala wa CCM—japo wamejipanga kusaidiwa na friendly fires—wanaona kasoro ni nyingi, hivyo suluhu pekee ni kukwepa mdahalo Kikwete asiumbuliwe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: