Kikwete ajibu tuhuma dhidi yake


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli
RAIS Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete aliishajijengea utamaduni wa kutojibu shutuma dhidi yake. Kazi hiyo aliikabidhi kwa wapambe wake, Yusuph Makamba, Kingunge Ngombale-Mwiru, George Mkuchika, Sophia Simba na Salva Rweyemamu.

Haikujulikana hasa nini kiini cha yeye kushindwa kujibu kile kilichomhusu, au kilichohusu serikali yake. Lakini sasa Kikwete ameamua kuvunja mwiko wake. Inawezekana ni baada ya kuona wale aliowatuma au waliojipachika, wameshindwa kumsaidia.

Ninampongeza. Ni vema aendelee kujibu tuhuma zote zinazomkabili yeye binafsi, chama chake na serikali yake. Ingawa baadhi ya majibu yake hayakubaliki, lakini kuna kila sababu ya kumshajiisha ili aanze kujibu hoja hata kama amechelewa.

Sasa anapaswa kujibu tuhuma ya kwanza, kwamba ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa 2005 uliwezeshwa na fedha za EPA zilizoibwa kutoka Benki Kuu ya Taifa (BoT).

Tunamtaka ajibu kuhusika wake, nyuma ya pazia, katika sakata la mkataba tata wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Asiishie hapo. Ajibu tuhuma kuwa aliacha kutangaza mali zake kutokana kuogopa kuulizwa alivyozichuma. Ajibu tuhuma kwamba ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi alizotoa wakati wa kampeni zilizomwingiza madarakani, hadi wakongwe wa chama kuanza kupendekeza “apigwe buti.”

Kuna tuhuma kuwa Kikwete anazidiwa nguvu na mitandao na kwamba ni mitandao ambayo inamwendesha na inayolihujumu taifa. Hajakanusha.

Kuna madai kuwa anamtumia mtu aliyejipachika unajimu mkuu Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahya Hussein kuwatisha wanaotaka asipewe nafasi kubeba bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) au hata kupingana naye. Hajakanusha.

Mlolongo wa tuhuma unaendelea. Kuna madai kuwa anafanya uteuzi mwingi kwa kuangalia mtandao, urafiki, dini na kulipa fadhila. Lakini rais amezidi kuziba masikio huku watu wasio na udhu wa nyadhifa zao, kama Sofia Simba au watuhumiwa wa kughushi vyeti vya taaluma, wanaendelea kupeta ingawa ni aibu kwa rais.

Kikwete anatuhumiwa kukumbatia watuhumiwa wa ufisadi, mmojawapo akiwa mshirika na rafiki yake, Rostam Aziz mbunge wa Igunga anayetuhumiwa kuwa mmiliki wa Richmond, Kagoda.

Tuhuma zinasema hii ndiyo siri ya kutokamatika kwa wamiliki wa Kagoda na wezi wengine kama alivyobainisha mkuu wa jeshi la polisi Said Mwema hivi karibuni.

Hili nalo linataka majibu. Kwanini taasisi yenye kila nyenzo na wataalamu wa uchunguzi wa jinai ishindwe na wahusika wasiachie ngazi kwa kushindwa kutimiza wajibu wao?

Rejea tuhuma kuwa kampuni ya kuzalisha umeme, IPTL ambayo imegeuka donda ndugu kwa uchumi wa taifa, iliingia mkataba wakati Kikwete akiwa waziri mhusika kwenye masuala ya nishati. Tuhuma hii haijajibiwa.

Rais anashutumiwa kukalia kesi nyingi za wahalifu mbalimbali kama alivyowahi kukiri na kutangaza kuwa ana orodha za majambazi, wauza unga, mafisadi, wezi wa bandarini, wala rushwa na nyingine.

Kuna tuhuma kuwa rais anaendesha nchi kirafiki ambapo mamlaka yake yanatumiwa vibaya kuwalinda marafiki zake. Rejea kutofikishwa mahakamani kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi na Andrew Chenge.

Hawa wanatuhumiwa kushiriki, kwa nyakati tofauti na kwa pamoja au mmojmmoja, kuipa mkataba kampuni ya Richmond, wa kufua umeme wakati haikuwa na sifa wala hadhi.

Tuhuma nyingine ni kuwa ameshindwa kurekebisha mikataba ya uwekezaji ya kijambazi iliyoingiwa na awamu ya tatu.

Kuna tuhuma kuwa, kwa vile alikuwa waziri wa Benjamin Mkapa, alishiriki kujipatia nyumba za umma hata kushiriki “uchafu” wa Mkapa. Akanushe au kutoa maelezo.

Tuhuma nyingine ni kwamba rais amekuwa mateka na mtumwa wa mafisadi. Wanasema nchi sasa ina ombwe la utawala. Haya ni madai mazito yasiyopaswa kunyamaziwa au kupuuziwa.

Pia kuna madai kuwa Kikwete anatawala bila sera kwani ni wachache wanajua sera yake ukiachia mbali kauli mbiu yake ya kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya ambayo imegeuka na kuwa kinyume.

Kuna hili la kukwepa majukumu ya ofisi yake na kupoteza muda mwingi ughaibuni kwenye ziara zisizo na manufaa kwa taifa. Rejea ziara zaidi ya kumi alizofanya kujitambulisha kwenye nchi mbalimbali; utadhani ndiyo walimpigia kura.

Madai mengine ni kuwa siku hizi majina ya watu anaoandamana nao nje yanafanywa siri. Hili nalo linaonekana kama ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Rejea kutotangazwa kwa waliokuwa katika ujumbe wake kwenye ziara yake huko Cuba, Jamaica, Trinidad and Tabago na Marekani ambako cha mno tuliambiwa alibembea na kuonana na mwanariadha maarufu wa Jamaica, Usain Bolt na kuomba makocha wa riadha.

Kuna tuhuma kuwa NGO ya mke wa rais, WAMA, ni bomu sawa na EOTF ya Anna Mkapa; kwamba ipo kutegeneza pesa na wachangiaji na wahisani wake wengi wana harufu ya ufisadi na wanafanywa siri.

Wengi wanahoji, kwanini mkewe awe na uchungu na akina mama mara tu baada ya Kikwete kupata urais.

Rejea mama Salma Kikwete kuonekana karibu kila mkoa na kwenye kurasa za mbele za magazeti akimpigia kampeni mumewe kinamna hata kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza kuanza kampeni.

Yanatakiwa majibu yanayoingia akilini na utekelezaji wa kuifutilia mbali NGO hii ambayo umma unaiona kwa jicho baya hasa kutokana na uzoefu wa EOTF (mfuko wa fursa sawa kwa wote ya Anna Mkapa) wa kufanya biashara ikulu.

Kwa vile Kikwete ameamua kujibu mapigo, tungemshauri ajibu hoja na si mapigo dhidi ya madai haya mengi, mazito na ya muda mrefu.

Japo ukimya ni dhahabu, mwingine ni adhabu. Martin Luther King Jr. aliishawahi kusema, maisha yetu huanza kupukutika siku tunapoanza kunyamazia mambo makuu na muhimu (Our lives begin to end the day we become silent about things that matter).

Hizi ni baadhi tu ya tuhuma. Tunangojea Rais Kikwete kujitokeza mbele na kujibu hoja na tuhuma anazotwisha. Kwa njia hii ataeleweka na atakuwa ametoa mwanga au elimu juu kinachojadiliwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: