Kikwete ajiulize, ajihoji


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala
Rais Kikwete na Dk. Hoseah

DOKTA Edward Hoseah hana kazi. Anakwenda ofisini kila siku, anatia saini, anapekua mafaili lakini hana kazi ya kufanya. Anasema alikosa kazi ya kufanya tangu Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani.

Julai 2007, Dk. Hoseah ama alijipendekeza au alizuzuka na wazungu wa Marekani, akamshtaki rais eti alimzuia kufanya kazi.

Kwa hiyo, hatua yake ya kukiri kuagizwa asishughulikie kesi kubwa za rushwa hasa zile zinazohusu viongozi wastaafu, ilikuwa hatua ya kujiumbua, kujimaliza na kujifukuzisha kazi.

Mtandao wa WikiLeaks umethibitisha Dk. Hoseah anafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya ikulu kwamba “washtaki Joseph Mungai na Frederick Mwakalebela, lakini waache huru mzee wa rada na wezi wa Kiwira.”

Ndiyo maana aliwashika wana-CCM (Arusha) waliotoa rushwa mwaka 2007 akavuruga mashtaka; akawashika wengine mwaka huu, akawaachia isipokuwa Mungai na Mwakalebela.

Dk. Hoseah na Rais Kikwete wataacha lini kutania Watanzania kuwa wako mstari wa mbele katika kutokomeza rushwa?

Awali malalamiko yalikuwa ubutu wa sheria iliyounda Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB/Takuru) lakini hata ilipoundwa upya kisheria kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB/TAKUKURU), si Dk. Hoseah wala Rais Kikwete aliyeonyesha dhamiri safi.

Rais alikabidhiwa orodha ya wahalifu; wauza ‘unga’, majambazi na walarushwa; akaishia kuwataka wajirekebishe eti baada ya krisimasi 2007 watakiona. Nani amekiona? Mramba na Yona?

Hata baada ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kumhusisha aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge katika rushwa ya ununuzi wa rada kutoka BAE Systems ya Uingereza, si Dk. Hoseah wala Rais aliyethubutu kutoa maelezo. Walifunika kombe kupisha mwanaharamu.

Dk. Hoseah alipoibuka akataka kudanganya watu eti kesi ya rada inayoikabili BAE Systems na kumhusisha Chenge imefutwa. Nani alimtuma kudanganya?

Mahakama Kuu ya Uingereza katika hukumu yake wiki iliyopita imethibitisha kuwa rushwa ilitumika kulainisha vigogo wa Tanzania wakubali kununua rada hiyo kwa bei mbaya.

Vilevile Dk. Hoseah alinaswa katika mtego mdogo alipoagizwa kuchunguza iwapo kampuni ya Richmond ilipata kwa hongo zabuni ya mkataba wa kufua umeme wa dharura.

Wakati waliomtuma walijua vizuri mchezo ulivyoisha, Dk. Hoseah, bingwa huyu wa kufunika, akatoa ripoti ya kufunika mambo. “Hakuna rushwa,” alisema.

Rais hakushtuka, akafurahia majibu hayo ya mtumishi mtiifu Dk. Hoseah. Serikali ikafanya usanii, ikakubali mapendekezo ya Bunge kuhusu adhabu kwa watumishi waliohusika kufanikisha rushwa, lakini serikali ikagoma kuwaadhibu.

Serikali ikaunda kamati nyingine ya kuwachunguza tena watuhumiwa, ikasafisha watu muhimu, halafu ikafanya njama mjadala wa Richmond ukazimwa kiaina bungeni.

Ukiwafuatilia Rais na Dk. Hoseah katika kipindi chote zilipoibuka kashfa, walichafua hewa badala ya kusafisha. Wote wawili wamefungamana katika kundi la viongozi wasiofaa kuongoza Watanzania wanaoamini rushwa ni adui wa haki.

Ripoti ya WikiLeaks imethibitisha kile kilichokuwa kikiripotiwa na MwanaHALISI: Fungamano la kifisadi lililoiweka serikali ya Kikwete mfukoni mwa mafisadi. Imezalisha mafisadi, ikawalea na inawaogopa. Kikwete amesamehe mijizi ya EPA, serikali yake imezuia Meremeta kukaguliwa, akaruhusu Richmond na sasa wamepandisha bei ya umeme ili wapate pa kuchota Sh. 185 bilioni za kuilipa Dowans, kampuni hewa wanayodai ilishinda kesi.

Kwa udhaifu huu, Rais Kikwete ameumbuka na hawezi kupata heshima anayoifikiria. Kwa kuwa ameshindwa kazi aliyoiomba ajiulize kama yeye na Dk. Hoseah wana sifa za kuendelea kuongoza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: