Kikwete akaliwa kooni


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version
Naye atakiwa kujiuzulu
Waraka mzito wavuja
CHADEMA yaitwa ‘mchawi’

RAIS Jakaya Kikwete amekaliwa kooni. Wakati chama chake kinakabiliwa na wimbi la kukimbiwa na wanachama na viongozi, swahiba wake anashikilia kuwa wenye “tuhuma za ufisadi” wajiuzulu kama yeye.

Katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) mjini Dodoma (20 – 21 Novemba), wajumbe walisomewa waraka unaoelezea hali ya wasiwasi ya viongozi wao kuhamia vyama vya upinzani.

Waraka Na. 7 uliowasilishwa na January Makamba unasema, kuna uwezekano wa viongozi wengi kuhama chama chao na kuingia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Waraka wa Makamba unakiri kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakabiliwa na wimbi kubwa la wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kuhamia CHADEMA.

Makamba ambaye ni katibu wa NEC anayehusika na siasa na uhusiano wa kimataifa anasema, “…wenyeviti hawa wanajiuzulu kwa ushawishi wa viongozi wa CHADEMA.”

Eneo ambako NEC imeambiwa viongozi wake wengi ngazi ya chini wamehamia CHADEMA ni Babati mkoani Manyara. Makamba anakiri katika waraka wake kuwa zoezi la kuhama limefanikiwa na kwamba iwapo litaendelea kufanikiwa katika sehemu nyingine nchini, CCM itadhoofika zaidi.

Makamba anamtaja ambaye anadhani ni adui mkubwa wa CCM kisisiasa wilayani Babati. “…wenyeviti hawa wanajiuzulu kwa ushawishi hasa wa Rose Kamili (Rose Kamili Slaa). Zoezi hili likionekana limefanikiwa Babati, litaweza kuhamishiwa katika sehemu nyingine za nchi na hivyo kukijenga CHADEMA katika ngazi za chini kabisa za utawala.”

Aidha, CCM inatishiwa na matokeo ya mpango wake wa kubadilisha katiba ambao unaonekana wazi kuwa utaziba baadhi ya viongozi kuingia NEC ambacho ni chombo kikuu cha utendahi cha chama na hivyo kuzua malalamiko, shutuma na tuhuma.

Katika kikao cha NEC ambamo taarifa za viongozi wake kuhamia CHADEMA ziliwekwa wazi, ndimo pia swahiba wa Kikwete, Edward Lowassa aliamka na kumtunga kidole usoni akidai kuwa anajua vema chanzo cha kashfa ya kufua umeme ya kampuni ya Richmond.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Lowassa kumgeuzia kibao Kikwete baada ya kipindi kirefu kwa kunyamazia tuhuma kuwa yeye (Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge) anatuhumiwa ufisadi na kwamba sharti wajiuzulu kwa kuwa wanachafua chama.

Edward Lowassa aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya kutoa mkataba wa upendeleo kwa kampuni ambayo haikuwa na sifa za kufua umeme, alimwacha hoi Kikwete kwa kumwambia kuwa hakuna asichojua juu ya sakata hili na kwamba alikuwa akimshikikisha kwa kila hatua.

Kwa kauli hiyo ndani ya kikao kikuu cha utendaji cha chama chao, Lowassa alikuwa amemuunganisha rasmi Kikwete kwenye orodha ya watuhumiwa wa ufisadi katika kashfa ya Richmond.

Ijumaa wiki iliyopita, katika mahojiano na TBC1, Lowassa alijitanua na kusema wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi sharti wajiuzulu kama yeye alivyofanya.

Wachunguzi wa mambo ya siasa za Tanzania wanasema hii ni njia mpya ya Lowassa kuanza kumkoromea Kikwete, baada ya kimya cha miaka mitatu na nusu tangu ajiuzulu.

Kama kwamba kikao hicho kilikuwa kimeitishwa rasmi kumkandamiza Kikwete, nyaraka kadhaa zilizowasilishwa zilionyesha mshololo wa matatizo ambayo Kikwete na chama chake wanakabiliana nayo miaka minne kabla ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.

Nyaraka zinaonyesha serikali ya Kikwete imeshindwa kutekeleza kile ilichoita, “Mpango wa dharula wa kuongeza nishati ya umeme (MW 572) katika gridi ya taifa ifikapo Desemba mwaka huu.

Mpango huo wa serikali uliowasilishwa bungeni, 13 Agosti 2011, ulieleza kuwa kati ya megawati hizo, MW 150 zilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano kati yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Mgawanyo wa megawati hizo ulionyesha kungeingizwa megawati 50 kwa kila mwezi, kati ya Septemba na Desemba 2011.

Hadi sasa hakuna hata megawati moja ya umeme iliyozalishwa na NSSF.

Taarifa kutoka serikalini na NSSF zinasema ujumbe uliotumwa nchini Marekani kuona mitambo iliyotajwa kuwapo haikukuta mitambo yoyote, badala yake walikutana na kile kilichoitwa, “Richmomnd nyingine.”

Inaelezwa baada ya timu hiyo ya wataalamu kushindwa kupata mitambo ya kuzalisha umeme nchini Marekani, waliamua kwenda nchini Ufaransa ambako nako wameambulia patupu.

“Ni kweli, hadi sasa hakuna umeme ulioingizwa na NSSF. Fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa. Hili ni jambo la hatari kwa mustakabali wa Tanesco, serikali na NSSF yenyewe,” ameeleza John Mnyika, mbunge wa Ubungo na waziri kivuli wa nishati na madini.

Mnyika alikuwa akijibu swali la mwandishi wa MwanaHALISI iwapo anafahamu kinachoendelea katika utekelezaji wa mradi huo.

Hivi sasa serikali inatumia karibu Sh. 2 bilioni kila siku kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme; jambo ambalo wachambuzi wa mambo ya uchumi wanasema, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno kwa uchumi wa nchi.

Katika kipindi cha miezi minne ya Agosti hadi Desemba 2011, serikali imetumia kiasi cha Sh. 523 bilioni kununulia mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme.

Akiwasilisha mada ya hali ya siasa na mahusiano ya jamii, Makamba ananukuliwa akisema athari za mgawo wa umeme ni kubwa kwa uchumi na chama chake.

“Athari za mgawo wa umeme kwa uchumi ni kubwa. Vilevile, tatizo hili lina athari kubwa kisiasa kwa CCM kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zake mara kwa mara za kumaliza tatizo hilo” nchini.

Tayari serikali imekubali kudhamini Tanesco kupata mkopo wa Sh. 408 bilioni kutoka mabenki binafsi ya biashara nchini, jambo litakalosababisha moja kwa moja mzigo mkubwa kwa wananchi.

Habari zinasema Tanesco wamewasilisha tayari ombi la kutaka kupandisha bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 185 (zaidi ya mara tatu) ya bei ya sasa, jambo ambalo litawafanya maisha ya wananchi kuwa magumu zaidi.

Januari 2011, Tanesco walipandisha umeme kwa asilimia 18.5 tu, lakini kupanda huko kulisababisha mfumuko mkubwa wa bei.

Mbali na tatizo la ukosefu wa nishati ya umeme na kushindwa kwa chama kutekeleza ahadi zake, Rais Kikwete anakabiliwa na migawanyiko ndani ya chama chake inayotokana na vita vya urais mwaka 2015 na mnyukano utakaoibuka kwenye mabadiliko ya katiba ya CCM yanayolenga kuwaengua baadhi ya wabunge kwenye ujumbe wa NEC.

Kwa mujibu wa waraka Na. 8 uliowasilishwa katika kikao hicho cha NEC na katibu mkuu Wilson Mukama, CCM imeazimia kupitisha mabadiliko ya katiba yanayoondoa wajumbe wa NEC kwenye ngazi ya mikoa na kupeleka wilayani.

Katika kupitisha mapendekezo hayo, NEC imetaka kutumia Ibara ya 107 (18) ya katiba ya chama hicho inayosema, “Kusimamia, kwa maslahi ya CCM, utumiaji wa kifungu chochote cha katiba ya CCM au kuruhusu kifungu kutumika kabla ya kuingizwa ndani ya katiba… Hata hivyo, uamuzi huo sharti baadaye ufikishwe mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho.”

Wachambuzi wa mambo wanasema mpango huo unalenga kuwaengua baadhi ya makada ambao ni wabunge na unaweza kuleta matatizo makubwa huko mbele, hasa iwapo itatokea wahusika kushawishi wajumbe wa mkutano mkuu kukataa mapendekezo hayo.

“Unajua mkutano mkuu wa chama ndiyo chombo cha mwisho. Mkutano mkuu ndiyo wenye mamlaka ya mwisho ya kukubali au kukataa pendekezo lililofanywa na vikao vya chini. Hivyo, ikiwa mpango huu unalenga kutuengua sisi, nakuambia kijana tutakwenda kwenye mkutano mkuu kupinga mapendekezo haya,” anaeleza mmoja wa wabunge kwa sharti la kutotajwa gazetini.

MwanaHALISI halikuweza kufahamu mara moja iwapo mabadiliko hayo ya kutaka wajumbe wa NEC kupatikana wilayani yalipita kama yalivyopendekezwa au kulikuwa na mabadiliko yoyote.

Utaratibu wa kupata wajumbe wa NEC kwenye wilaya unaelezwa katika ukurasa wa tatu wa waraka wa Mukama. Pamoja na mambo mengine, unalenga kupatikana kwa viongozi wanaotoka moja kwa moja kwenye wilaya hizo.

Waraka unasema watakaoruhusiwa kugombea ni wale tu, wenye makazi ya kudumu kwenye wilaya hizo.

Misukosuko yote hii inamkabili Kikwete ambaye mapema mwaka kesho anatarajiwa kuomba kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama ambacho wachunguzi wanasema, kinaweza kukabidhi njiti kwa upinzani mwaka 2015.

0
Your rating: None Average: 2.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: