Kikwete ameanza kumwaga damu


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

HATIMAYE yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu yametimia. Mkoani Arusha serikali imeua watu wake kwa risasi za moto.

Dhambi kama hii, kubwa na ya mwisho, kwa kawaida hufanywa na serikali dhalimu, serikali inayojali raia wake.

Inasikitisha! Mikono yenu sasa imetapakaa damu; damu ya watu wenu wenyewe! Kwa ujinga wa mtu mmoja, nchi sasa imetiwa doa jeusi katika macho ya kimataifa. Na kwa ujinga wa mtu huyo serikali sasa imejipandikizia chuki nzito katika mioyo ya watu wake.

Baba, idadi ya wanaokuchukia sasa imeongezeka maana hata wenye haki na wote walio wema wameungana nao. Baraka za Mwenyezi mungu zitapatikana vipi?

Nakuahidi sitakuacha. Nitakuwa nawe hata katika siku zako za shida kwakuwa wewe ndiye baba na u-mwema. Utawala wa kishetani hukosa radhi ya Mungu. Mungu anajua kuwa maisha ya Watanzania yako mikononi mwako na wewe ndiye utatoa hesabu kwa kila utakayempoteza!

Waliotenda unyama huu, hukumu ya Mwenyezi Mungu iko juu ya vichwa vyao. Mungu wa Ibrahim Mungu wa Yakobo atawaonyesha hasira yake wao na watoto wao hapa hapa duniani.

Josephine Mushumbusi simfahamu, lakini  nilimwona katika picha, mwili wake ukiwa umetapakaa damu yake iliyokuwa inachuruzika toka kichwani. Wanyama hawa walimpiga mjamzito huyu mpaka wakampasua kichwa.

Kwa uchungu mkubwa alilia akisema, “Nipigeni! Niueni! Nitakufa kwa ajili ya kutetea wananchi wengi walio maskini na wanyonge. Kama nchi imefikia hivi hali si nzuri…mnanipiga kiasi hiki wakati nimeisha waambia nina ujauzito….hakuna neno. Damu mlioimwaga haitaenda bure.

“Lazima matunda yake yatapatikana kwani wananchi watapata haki zao. Hata huyo dereva mnayemtoa sadaka  damu yake haitaenda bure.”

Katika mateso makali kama haya mama huyu hakujililia yeye bali maskini na wanyonge. Mungu atambariki. Kilio hiki alilia Mahlangu, mpigania uhuru wa Afrika Kusini alipokuwa anawekwa katika kitanzi tayari kwa kunyongwa na utawala katili wa Makaburu.

Alisema, “Damu  itakayomwagika itazirutubisha mbegu za mti utakaochipua na kuleta uhuru wa kweli.”

Kristu Yesu akiwa katika magumu aliwaambia wale wanawake waliokuwa wanamlilia, “Msinililie mimi, jililieni wenyewe na watoto wenu.”  Waliowema huwazia wengine kwanza, mimi baadaye. Watawala wetu wamepofuliwa na umimi kwanza.

Waliowatuma kutenda unyama huu walibaki katika makasri yao wakiangalia katika televisheni vijana wao wakifanya kazi waliyowatuma. Mungu apishe mbali!

Katika ukurasa wa 60 kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Ala kumbe! Kila zama na watu wake. Walikuwapo wafalme waliokuwa na mamlaka na majeshi yenye nguvu kupindukia. Watawala walioitawala dunia kwa upanga wa moto. Leo wako wapi? Hawako tena. Wamekwishapita.

“Walikuwepo masultani waliofanya kila aina ya ufirauni, wao wakiuita starehe! Je, leo wako wapi? Hawako tena! Wamekwishapita.

“Walikuwepo majemedari nduli walioua raia na askari kwa maelfu kwa utashi tu na ujivuni. Lakini je, leo wako wapi? Hawako tena!

Wamekwishapita. Na sisi tunapita!” Wako wapi akina Mobutu Seseseko, Iddi Amin na wenzake? Wote nyama ya udongo! Mpumbavu hudhani yeye ataishi milele!

Baba utuambie, unatulizaje ghasia kwa kumvua mwanamke suruali aliyoivaa? Tumwombe Mwenyezi Mungu atufundishe kufanya ibada. Laana imeingia katika nchi yetu watu wa Mungu wanaangamia.

Mwana mwema kaniandikia, “Mwalimu mkuu sali kwa kuwa wewe Mungu wako huwa anakusikia.” Kama hivyo ndivyo, Mwenyezi Mungu ashushe uso wake wa huruma juu ya ‘Yatima hawa wa Nyerere ambao leo wanauawa kwa risasi.

Mwana mwema Maturo aliniandikia, “Arusha imekuwa Kenya ndogo. Siyo tena raia ni polisi wanakimbia raia. Ningefurahi Rais Jakaya Kikwete na na katibu mkuu, Yusuf Makamba wangekuwa Arusha maana ndio waliosababisha. Kama kuongoza halmashauri wanatumia nguvu hivi na nchi itakuwaje?”

Rais wangu, tusome ukurasa wa 8 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Maandamano yalijumulisha watoto, vijana, wazee, akinamama, na hata vilema na ulemavu wao. Waliendelea mbele na kukata kushoto kuingia katika barabara iendayo moja kwa moja.

Hapo ndipo…lahaula! Walikutana na askari wengi wa kutuliza ghasia waliojisheheneza silaha nzitonzito. Basi bila onyo wala hadhari yoyote, na kwa nguvu kubwa ajabu, askari wale wa kutuliza ghasia walianza kutuliza ghasia ambayo kwa kweli haikuwepo.

Walifyatua risasi za moto. Walifyatua risasi za mpira. Walifyatua mabomu ya machozi, walitumia virungu na silaha nyingine nyingi dhidi ya  ule umati. Kwa kufanya hivyo, askari wa kutuliza ghasia wakawa wameanzisha ghasia kubwa.

Ilikuwa tafrani kubwa patashika nguo kuchanika. “Traa tra….. traa…” bunduki zilifyatuliwa ovyo. Mabomu ya machozi yalilipuliwa na virungu kutembezwa ovyo.

Waliopoteza maisha yao  waliyapoteza. Waliojeruhiwa walijeruhiwa. Watu walikimbia hovyo kusalimisha maisha yao. Umati ulitawanyika na kusambaa huku na huko.

Moshi wa risasi na ule wa kiwandani ulizagaa hovyo hewani. Patashika yake ilikuwa kubwa na matokeo yake yalimtoa machozi kila aliyekumbuka baadaye. Aliyesimuliwa alishindwa kuelewa ni kwa kiasi gani binadamu anaweza kuwa mkatili kwa binadamu mwenzake.

Askari wa kutuliza ghasia walianzisha ghasia ambazo mwisho wake ulikuwa  vifo, majeruhi, mateso na vilio vingi vya wale waliokuwa wakizitoa  roho zao. Huo ndio ukawa mwisho wa maandamano ya amani.

Edward Lowassa alishauri wana wema wa Arusha wakae pamoja kama ndugu walipatie ufumbuzi  jambo lililowasibu, lakini mwana wa shetani akampuuza. Sasa wana wa nchi hii wanauawa kama nguruwe.

Rais wangu tuambie askari wa serikali walipowafikia waandamanaji walikuta ghasia gani? Walianzaje kutuliza ghasia ambazo hazikuwapo? Malaika wa Mungu watoto wadogo nao walifanya ghasia gani? Wasafiri kituoni walileta ghasia gani? Wote waliadhibiwa. Kosa lao shetani peke yake anajua.

Baba waache Watanzania katika neema uliyowakuta nayo na Mungu atakubariki. Wameanza kuwa sugu na shuruba za polisi. Watakapoyakumbuka maneno ya  Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere risasi za kuua mlizonazo hazitawatosha Watanzania wote. Mtaua wangapi?

Wako watakaobaki kwa ajili ya kuwahukumu wahusika. Kwelikweli nawaambieni mwisho wao utakuwa mchungu kuliko shubiri. Nao hawatachagua baba, mama, wala mtoto. Ole! wao watu hawa, kwa maana ingelikuwa bora kwao kama wasingezaliwa!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: