Kikwete amekwishafanya uamuzi mgumu


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version

TUNAPOELEKEA uchaguzi mkuu ujao tukiwa "ndani ya kumi na mbili" hatuna budi kuangalia uongozi kwa mwanga mpya. Tukiendelea kuangalia uongozi kwa mwanga wa zamani basi tutajikuta tunarudia makosa yale yale tuliyoyafanya huko nyuma.

Zamani mgombea alikuwa anakuja huku akituringishia vyeti vyake vya elimu na wapi amesoma huku tukivutiwa na yule ambaye anaonekana kusoma “sana” na kumfikiria kuwa huyo atatufaa.

Katika mwanga huu wa zamani tulimkataa mtu ambaye ameishia darasa la saba na tukamkumbatia yule aliyefika Chuo Kikuu. Wakati mwingine tulimkataa kijana sana kwa kumkumbatia mzee au kinyume chake tukiamini kuwa vitu hivyo vinahusiana na uongozi.

Katika mwanga huu mpya, ambao nimeuita ndani ya miaka minne kuwa ni “mapambano ya kifikra,” Watanzania tunaitwa na historia, bahati, na mpango wa kimbingu, kuachana na fikra za zamani na kuanza kufikiri kwa namna mpya kabisa; namna mpya ya kuwapima viongozi wetu tunaowataka.

Uongozi ni uwezo. Uongozi siyo elimu, uzoefu au umri. Hivi vyote vinaweza kumsaidia kiongozi kuwa kiongozi mzuri. Lakini havimfanyi mtu kuwa kiongozi mzuri au hata kuwa kiongozi.

Hapa hatuna budi kusema wazi kuwa uongozi ni uwezo. Yaani, mtu ambaye anataka kutuongoza ni lazima awe ni yule mwenye uwezo wa kutufanya tuamini kuwa anaweza, ana maslahi yetu moyoni mwake na yuko tayari kusimamia maamuzi yake na kukubali matokeo ya maamuzi hayo.

Kiongozi mzuri siyo yule anayetuahidi nini atatufanyia bali yule ambaye yuko tayari kufanya yale ambayo sisi tunayataka kama wananchi.

Uwezo huu wa kiuongozi unamtofautisha mfuasi na kiongozi. Tangu utoto tumevutiwa na watu ambao wanatuonyesha uwezo wa kutushawishi kukubaliana nao. Kama ilikuwa twende tukacheze mpira au kucheza kombolela, kwenda kucheza “ready” au kwenda kuruka kamba; kutoroka darasani au kwenda kujisomea!

Wale waliotushawishi utotoni ni hawa tuliwafuata. Wale ambao walikuwa ni washawishi utaona hata baadaye ukubwani wamekuwa ni watu wa ushawishi vile vile na kuongoza wengine (katika mema au mabaya)!

Uwezo huonyeshwa katika maamuzi.

Mojawapo ya maneno ambayo tumeyasikia karibuni ni kuwa tunahitaji viongozi wanaoweza “kufanya maamuzi magumu.”

Tumeyasikia haya kwa sauti zaidi katika kongamano siku chache zilizopita, ambapo baadhi ya watumishi wakongwe wa nchi yetu walipaza sauti zao wakitaka Rais Kikwete kufanya “maamuzi magumu” na hivyo kuonyesha uongozi. Naomba kutofautiana nao.

Rais Kikwete hahitaji kufanya maamuzi magumu! Ameshayafanya, yanatosha. Si yeye ndiye aliyemteua Andrew Chenge licha ya Chenge huyohuyo kuandamwa na tuhuma za ufisadi katika suala la rada?

Ni Kikwete aliyeruhusu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samwel Sitta, kusulubiwa katika vikao vya chama kiasi cha kutishia utawala wetu wa kikatiba. Ni yeye aliyeliacha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) linunue dege lile bovu na kujiendesha kwa hasara huku akiendelea kulimwagia mabilioni ya fedha za walipa kodi.

Si yeye na serikali yake waliamua kuwaacha watoto wetu karibu 30 kwenye baridi la Ukraine na kuwalazimisha kuacha masomo ya chuo kikuu kwa kisingizio kuwa “serikali haina pesa” wakati leo hii wanatuma watu karibu sabini kwenda kwenye mkutano huko majuu wakati yeye na wenzake wakicheza kwenye bembea za Cuba? Wanataka Rais Kikwete afanye maamuzi gani magumu?

Ndugu zangu, uongozi siyo kufanya maamuzi magumu! Uongozi ni kufanya maamuzi bora! Tukitaka kiongozi yeyote ati afanye maamuzi magumu wakati mwingine tunampa ruhusa ya kufanya maamuzi magumu ya nani amridhishe.

Kama uamuzi ni kati ya kuwakamata wahusika wa Kagoda au kuifunua Meremeta na kuwawajibisha wote wahusika na kiongozi akaamua kutofanya lolote kati ya hayo akiamini kuwa huo ni “uamuzi mgumu” je tutamlaumu?

Uamuzi bora hutanguliwa na misimamo bora: Mojawapo ya mambo ambayo yanamtofautisha kiongozi bora na bora kiongozi ni misimamo aliyonayo. Vitu ambavyo vinanisumbua sana binafsi ninapoangalia watawala wetu ni kuwa misimamo wanayochukua ni ya kusikitisha. Bila ya mtu kujifunza kuchukua misimamo bora mtu huyo hawezi kuchukua maamuzi bora.

Kiongozi ni lazima awe na msimamo wa kuchukia rushwa ili aweze kuchukua maamuzi ya kupigana na rushwa; kiongozi ni lazima awe na msimamo wa kukataa uonevu ili achukue maamuzi ya kutokumuonea mtu. 

Misimamo bora hutanguliwa na fikra bora.

Hata hivyo, mtu hawezi vile vile kuchukua misimamo bora kama fikra zake na mtiririko wa fikra zake siyo bora. Mtu ambaye hajajifunza kufikiria na kujenga hoja na kuzipima kwa kina atajikuta anachukua misimamo mibovu.

Kama mtu anaamini kuwa “wazungu wako mbali” na kuwa “wazungu siyo mafisadi” mtu huyo anapoenda kujadiliana na wazungu hawezi kufikiria kuwa wanamuingiza mkenge!

Hivyo, ili mtu aweze kufikia misimamo bora ni lazima awe na fikra bora ili hatimaye aweze kuchukua maamuzi bora. Nje ya hapo utaona kuwa mtu mwenye fikra za uduni atakuwa na misimamo ya uduni (kama kwenye mikataba) na matokeo yake atachukua maamuzi ya mtu duni.

Ni kwa sababu hiyo, kama taifa na kama wananchi unapokuja uchaguzi huu mkuu ni lazima tuwapime viongozi wetu siyo kwa kile wanachosema bali kila wanachosimamia na hiki kinaonekana kwenye historia zao.

Kiongozi anayeibuka sasa hivi na misaada kwenye jimbo lake na ahadi kibao za nini atafanya ni kiongozi wa kuogopwa. Viongozi bora hawaanzi wakati wa uchaguzi. Ni wananchi wenzetu ambao tumekuwa nao wakituonyesha njia na kutushawishi katika mambo kadhaa hata bila ya wao kuwa na maslahi ya uchaguzi au kuchaguliwa. Hawa ndio viongozi ambao hutambulikana kwa fikra zao, misimamo yao na maamuzi yao bora.

Hawa ndio viongozi ambao ndani ya “hizi kumi na mbili” tunawahitaji ili kuweza kuanza kuushinda ufisadi na kuanza kujenga misingi ya taifa jipya la kisasa. Vinginevyo, tuwe tayari kupokea “bora viongozi”.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: