Kikwete amepasua jipu la udini


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 07 September 2011

Printer-friendly version

IDADI kubwa ya wasomaji wanapata mawazo mbadala juu ya mwelekeo wa nchi, zaidi kupitia kwenye magazeti yanayofanya uchunguzi kuibua uozo, wizi, ubadhirifu au ufujaji wa mali na raslimali za nchi na ukiukwaji wa sheria za nchi na utawala bora.

Wasomaji wachache sana tena wenye nafasi na wakiwa ofisini hupata fursa ya kusoma kinachoandikwa kwenye ‘social media’ yaani mitandao jamii kama intaneti, twitter na facebook.

Humo, hasa kwenye intaneti, kuna mijadala mikali na yenye sura tofauti na mingine iliyojaa chuki ya wazi kati ya Wakristo na Waislamu.

Mjadala mojawapo mzito unahusu uamuzi wa serikali kukubali kurejesha shule zilizokuwa zinamilikiwa na Wakristo lakini ikawakatalia Waislamu. Mjadala huu wa muda mrefu, umehaishwa wiki iliyopita na mgeni rasmi Rais Jakaya Kikwete katika Baraza la Id el Fitr mjini Dodoma aliposema kuwa serikali haitarejesha shule zilizokuwa zinamilikiwa na Waislamu.

Aidha, katika Baraza hilo, Rais Kikwete alisema serikali inawaruhusu Waislamu waanzishe Mahakama ya Kadhi na waendeshe wao wenyewe.

Jambo jingine zito ambalo Rais Kikwete alisema, tena kwa ujasiri mkubwa tofauti na siku za nyuma, ni pale alipokemea waziwazi na kuonya waumini wa dini moja kukashfu dini nyingine.

Haya ni masuala ya msingi yanayowagawa waumini wa dini mbili hizi kubwa nchini. Hapa Rais Kikwete ni kama amepasua jipu, ameacha ‘aliyepeasuliwa’ akiwa na maumivu ya kuuguza kidonda.

Hotuba hiyo ilipokewa kwa mtazamo tofauti. Maaskofu wamempongeza Rais kwa kuchana pazia la udini linalotenganisha Watanzania kwa dini, lakini Waislamu wameponda na kupitia Shura ya Maimam wametishia kufanya maandamano nchi nzima.

Kwa hiyo, msimamo huu wa Rais Kikwete au serikali yake kuhusu mambo haya umeibua hasira za Waislamu. Wanadai kwenye mitandao ya jamii ametumbukia katika mkumbo ule ule wa kupendelea mfumo Kristo.

Msimamo wa serikali kuhusu Mahakama ya Kadhi ni huo. Lakini serikali inaweza kupitia upya uamuzi juu ya urejeshwaji wa shule kwa madhehebu ya dini kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima.

Wale wenye umri nusu karne kama mimi au waliozaliwa kabla ya uhuru, wanajua kuwa mashirika mengi ya dini yalikuwa yanamiliki shule za msingi, sekondari na vyuo nchini.

Aidha, waliosoma enzi za ukoloni wanajua ilivyokuwa vigumu kwa mtu mweusi kusoma shule za Wazungu au Wahindi. Vilevile wanajua masharti ya kusoma kwenye shule za seminari. Mazingira hayo ndiyo yalichochea, baada ya uhuru, serikali ya TANU kutaifisha shule zote za kidini ili kila mtoto apate fursa ya kusoma bila kujali dini wala rangi.

Shule zote zilizokuwa zinamilikiwa na wamisionari au Wahindi na taasisi za Kiislamu zilichukuliwa na serikali.

Miaka ya 1980, baada ya Vita dhidi ya Idd Amin Dada wa Uganda, uendeshaji wa shule ilianza kuwa mgumu na waathirika wakubwa walikuwa walimu na shule zao.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, serikali iliporuhusu mashirika ya dini kujenga shule na taasisi za elimu ya juu, madhehebu ya dini ya Kikristo yalianza kuomba kurejeshewa baadhi ya shule zilizokuwa zimetaifishwa huku yakionesha jinsi yatakavyoziendeleza.

Serikali iliridhia kurejesha shule tatu tu tena miaka ya hivi karibuni tu. Kanisa Katoliki lilirejeshewa shule ya msingi na sekondari ya Forodhani; Kanika la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) lilirejeshewa shule ya sekondari ya Magamba ambayo imeboreshwa na kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Sebastian Kulowa (SEKUco) mwaka 2007.

Kanisa la Anglikan lilirejeshewa shule ya sekondari ya Mazengo ambayo imegeuzwa kuwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (SJUT) 2007. Vyuo hivi vinamilikiwa na madhehebu ya Kikristo lakini vinachukua wanafunzi wa dini zote.

Uendeshwaji wa shule kwa Wakristo zilizogeuzwa vyuo vikuu ungekuwa msingi wa kuweka urari kwamba shule zilizoombwa na Waislamu ambazo kihistoria zilijengwa na kumilikiwa na taasisi za Kiislam na zikataifishwa mwaka 1967 warejeshewe. Kwa nini suala hilo litumiwe kuibua migogoro kati ya Wakristo na Waislamu?

Tatizo jingine kwa serikali, kama ilivyo mahakamani, mtu anaweza kukosea taratibu za kuwasilisha maombi tu, kesi au maombi yake yakatupwa hata kama ana haki. Kama Waislamu wamekosea taratibu za kuomba basi waelekezwe namna ya kuwasilisha maombi na mikakati ya kuziendeleza. Kuwanyima kwa kigezo cha kuchelewa kuomba kiangaliwe upya ili kisitumike kuwakosesha haki.

Hata hivyo, ieleweke si madhehebu yote ya Kikristo yaliyoomba yaliyorejeshewa shule na yale yaliyofanikiwa hayakurejeshewa shule zote. Je, itakuwaje Wakristo wakiomba  kurejeshewa shule zote?

Jambo jingine la msingi ni kuwa Wakristo hawakutaka kuganda kwenye shule za zamani tu, wamejenga mpya na wamefungua vyuo vikuu vingi na hospitali. Taasisi na dini nyingine ziige.

Kanisa la Kibaptisti linamiliki Chuo Kikuu cha Mount Meru (MMU); Wasabato waligeuza chuo cha theolojia kuwa Chuo Kikuu cha Arusha (UoA); Kanisa la Moravian linamiliki Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU).

Hata kama serikali isingewarejeshea shule ya sekondari ya Magamba kuanzisha SEKUco, KKKT imejenga na kutumia majengo yake kuanzisha vyuo vikuu kadhaa. Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Tiba cha Kilimanjaro (Kilimanjaro Christian Medical College – KCMC) 1997; Chuo Kikuu cha Makumira (MUCo) 1997 Arusha; Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo) 1997; Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCo) 2004; Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano cha mjini Moshi (SMMUCo) 2007 Moshi.

KKKT ina mpango wa kufungua vyuo vikuu vingine vitatu kikiwemo Joseph Kibira (JoKUco) cha Bukoba, Kagera.

Kanisa Katoliki linamiliki Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) 1998;Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Bugando (BUCHS) 2003 Mwanza; Chuo Kikuu cha Elimu Mwenge (MWUCE) 2005 Moshi; Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) 2005 Iringa.

Serikali ya awamu ya tatu, kwa nia thabiti iliamua kwa makusudi kuchukua majengo ya Chuo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Morogoro na kuwapa Waislam. Hapo ndipo kipo Chuo Kikuu cha Kiislam Tanzania. Tusonge mbele.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: