Kikwete ametuacha njia panda


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 07 April 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Rais Jakaya Kikwete

HOTUBA ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa 1 Aprili 2009, haiwezi kupita bila kujadiliwa. Sababu zipo nyingi. Lakini kubwa ni kwamba hotuba ya rais ni kichocheo cha mijadala.

Katika hotuba yake Rais Kikwete alizungumzia mambo makubwa matatu. Mwenendo wa mvua na hali ya chakula nchini, hali ya upatikanaji na uzalishaji wa umeme, na mkutano wa nchi ishirini tajiri duniani.”

Kuhusu Mwenendo wa mvua na hali ya chakula nchini. Haya ya mvua, ukame na matatizo ya chakula siyo mageni nchini. Ni mambo yanayojulikana kwa karibu miaka 50 sasa.

Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambayo haistahili na haina sababu ya wananchi wake kuishi na wasiwasi wa chakula.

Sababu ya kuwa na njaa katika taifa hili ni moja tu, uzembe! Njaa ya Tanzania haitokani na ukosefu wa maji, bali ukosefu wa mipango thabiti na hatua madhubuti za kubadilisha kilimo kiwe cha kisasa zaidi.

Zingatia mambo mawili tu. Kwanza tunazungukwa na mito mingi na maziwa makubwa na madogo. Hilo peke yake linatupa jibu moja la haraka kuwa hatuna tatizo la maji.

Lakini jambo la kushangaza ni kuwa karibu miaka 50 baadaye Tanzania haina mradi mkubwa wa umwagiliaji maji wa kuzalisha mazao ya chakula.

Ripoti ya mpango wa kilimo cha umwagiliaji ya mwaka 2002 unaonesha kuna hekari 29.4 milioni zinazoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji. Kati ya hizo 2.3 milioni zina uwezo mkubwa, 4.8 uwezo wa kati na 22.3 uwezo mdogo.

Hadi Juni mwaka jana, hekari 290,000 tu ndizo zilizokuwa zimeendelezwa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Kwa maneno mengine, kama tukichukulia kiasi kilichoendelezwa ni sehemu ya zile milioni 2.3 zenye uwezo mkubwa, basi utaona kuwa kilichoendelezwa ni asilimia 12.6.

Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miaka 48 baada ya uhuru hata robo hatujafikia, badala yake tunaendelea kuangalia angani kusubiri mvua. Kama kiasi hicho ni kutoka katika jumla ya hekari zote za milioni 29.4 basi tulichoendeleza ni asilimia 0.98 ya uwezo wetu wote wa umwagiliaji.

Pili, mikoa minne ambayo tunaiita ndiyo wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Rukwa kwa karibu miaka 50 imekuwa ikiilisha nchi kwa kiasi kikubwa kwa kutumia jembe la mkono.

Kwa maneno mengine, tunapokuwa na mvua za kutosha, mbolea na udhibiti mzuri wa wadudu waharibifu, mikoa hii inaweza kuzalisha asilimia 100 na zaidi ya mahitaji ya taifa. Sasa kama tungeweza kuondokana na jembe la mkono ambalo linatumia nguvu kazi kubwa na muda mwingi, kilimo chetu kingekuaje?

Hivyo, matatizo ya chakula nchini hayatokani na ukame, mvua pungufu au uuzaji wa nafaka nje ya nchi. Ni shauri ya uongozi mbovu, sera zilizobakia vitabuni, na tabia ya kuvuta muda bila ya kuona uharaka na umuhimu wa kufanya mambo kwa mfumo wa dharula.

Ni vema rais Kikwete akafahamu kwamba mapinduzi ya kilimo hayawezi kuja kwa miujuza. Yanaweza kupatikana kwa kuwepo dhamira na mipango yake kutekelezwa, badala ya kuifungia katika makabati na kutafunwa na panya.

Hali ya upatikanaji na uzalishaji wa umeme.

Rais alisema tatizo kubwa la upungufu wa umeme ambao umesababisha mgao katika maeneo ya Dar es Salaam na wilaya za jirani, ni kuharibika kwa mashine.

Lakini Kikwete anajua kwamba tatizo halijatokana na kuhabarika kwa mashine mbili au tatu! Tatizo ni sera mbovu ya nishati ambayo imeshindwa kuzalisha umeme wa ziada wakati uwezo wa kufanya hivyo upo, fedha zipo na watu wa wapo!

Kwamba, hatujathubutu kuwa na miradi ya uhakika na mipango ya makusudi ya kukomesha tatizo la uhaba wa nishati hiyo. Ndiyo maana rais anasema, “Kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo ni dalili kuwa baada ya muda si mrefu hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa mbaya hata kama mitambo yote ya sasa itakuwa inafanya kazi kwa ukamilifu.”

Anasema, kwa sasa mahitaji yanaongezeka kwa asilimia 10– 15 kwa mwaka. Hili ni ongezeko kubwa sana ambalo linahitaji kusiwepo kukwama kokote.

Yaani, tatizo wanalijua kuwa huko mbeleni litatokea tatizo la upungufu wa umeme. Taarifa hizo zimesemwa bungeni kwa miaka zaidi ya 20. Lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Ni katika hilo ndipo rais akaelezea suala la kampuni ya kufua umeme ya Dowans Holding Tanzania Limited., kwamba “…kwa nia ya kupunguza makali ya mgawo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likaona waombe ruhusa ya kununua mitambo ya Dowans ambayo wakati huo ilikuwa inatangazwa kuuzwa.”

Kama hiyo haitoshi, rais akapongeza viongozi wa Tanesco kwa kile alichoita, “uamuzi wao wa busara wa kuachana na nia ya kununua mitambo ya Dowans.”

Hakika, uamuzi wa kutonunua mitambo hiyo haukuwa wa Tanesco. Ulikuwa wa wanaharakati na wazalendo wa nchi hii waliotawanyika kote duniani. Wale waliojitoa kuzuia serikali kuzawadia kampuni ya kitapeli, kampuni ambayo haikuwa na mkataba na serikali, lakini tayari imekwapuliwa fedha za umma.

Kutokana na hali hiyo, rais hakutenda vema kutoa pongezi kwa Tanesco. Waliostahili pongezi walikuwa ni wananchi.

Hapa pia hatukusikia mipango madhubuti wa kuondokana na tatizo la upungufu wa nishati. Hatukusikia mpango usiohusisha viraka vya majenereta ya kila mwaka na vibwawa vidogo vidogo. Hatukusikia mipango ya kufua umeme kupitia bwawa la mto Rufiji ambalo lina uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha na mwingine hata kuuza nje.

Na kama tungekuwa ni watu wenye kuthubutu kweli, Tanzania ingeweza kuanzisha mpango wa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa nguvu za Kinyuklia.

Tuna uwezo na mazingira yetu ya kisiasa ni ya utulivu mkubwa wa kutosha kabisa kuanzisha mradi kama huu ambao umeme wake unaweza kutosha katika eneo lote la Afrika Mashariki kwa muda mrefu ujao.

Tukiamua kutumia nguvu hizo za kiatomiki tunajiweka katika mazingira ya kutokutegemea mvua kabisa katika kuzalisha umeme. Kwanini miaka karibu hamsini baadaye mpango kama huo unaonekana ni mwiko?

Jingine ambalo naamini lingeweza kufanyika ni kubadilisha sheria ili TANESCO isinunue umeme kutoka kwa makampuni ya kuzalisha umeme.

Sheria itamke kwamba makampuni binafsi yazalishe umeme na wauze wenyewe kwa wateja; wakitaka kutumia miundombinu ya TANESCO ambayo imegharimiwa na Watanzania, basi makampuni hayo yalipe Tanesco “Capacity Charge.”

Hili la Dowans kwa hakika halijafikia kikomo chake kama rais anavyotaka tuamini. Kwa kadiri ya kwamba mnunuzi pekee wa mitambo hiyo ni Tanesco au kampuni nyingine ambayo yaweza kuiuzia Tanesco umeme kuna kila dalili mitambo hii haiendi kokote.

Njia pekee ya kumaliza mjadala huu ni kwa kuiondoa mitambo hiyo pale Ubungo. Kuifungua na kuipeleka uwanja wa ndege ili kina Al-Adawi na marafiki zake waichukue na kuirudisha Costa Rica. Vinginevyo, litamalizwa kwa serikali kuitaifisha kwa sababu za kisheria.

Na zaidi ya yote mjadala huu utaisha vipi wakati bado tunawadai mabilioni na zaidi ya yote wao wamefungua kesi ya kudai zaidi ya 100 bilioni katika mahakama ya kimataifa kule Paris, Ufaransa?

Mjadala hauwezi kwisha kwa sababu rais kasema. Unaweza kufungwa iwapo Dowans watang’oa mitambo yao na kuondoka. Unaweza kufungwa iwapo watendaji wa serikali watatimiza wajibu wao wa kushinda kesi iliyofunguliwa na Dowans.

Tayari kuna taarifa kuwa baada ya ununuzi mitambo kugonga mwamba baadhi ya watendaji wa serikali wanakula njama na “wamiliki wa Dowans,” ili serikali ishindwe katika kesi iliyofunguliwa na kampuni hiyo. Lengo ni kukomoa serikali na kuhakikisha Dowans wanalipwa fedha zao na kuondoka na mitambo yao.

Lakini kubwa zaidi na ambalo Mwendesha Mshitaka Mkuu wa Serikali (DPP) na wasimamizi wa sheria zetu wangeamua kufuatilia ni ukweli kuwa kampuni ya Dowans kama ilivyokuwa kwa Richmond ni kampuni iliyoingia kwa ulaghai nchini.

Ilijitaja kuwa wabia wake wakubwa ni makampuni ya Portek Indonesia na Dowans Holdings SA. Ukweli ambao hata rais Kikwete anaujua ni kuwa kampuni ya Portek haina hisa kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited na kampuni ya Dowans Holdings ni kampuni ya kitapeli iliyoanzishwa kwa lengo la kuweza kuingia Tanzania.

Kampuni hii haina ofisi, simu, wala mtu aliyeiandikisha huko Costa Rica. Kwa ufupi, kama wazazi wa Dowans ya Tanzania hawakuzaliwa, haiwezekeni mtoto Dowans akawepo.

Hii inatuachia uchaguzi mmoja tu, kutaifisha mitambo ya Dowans. Ukiangalia kwa karibu mchakato wa jinsi Dowans ilivyopata mkataba na jinsi ulaghai uliotumika, jinsi Sheria ya Manunuzi ya Umma ilivyokiukwa, utaweza kubaini mara moja kwamba serikali ikiamua mitambo ya Dowans haiwezi kuondoka nchini. Ni mitambo ya kutaifisha moja kwa moja.

Kuhusu Mkutano wa G20: Rais alielezea kwa kirefu historia ya matatizo ya kiuchumi na jinsi gani Tanzania na Afrika kwa ujumla hazihusiki katika matatizo ya mataifa hayo makubwa lakini athari za mmomonyoko wa kiuchumi unaziona.

Inasikitisha kuwa katika mambo matano ambayo rais Kikwete alisema yametokana na mkutano wao na IMF/WB na ambayo aliyapeleka kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown yafikishwe kwa G20 hakuna hata moja ambalo linahusu serikali yake inafanya nini kukabiliana na tatizo hilo.

Swali ambalo ninabakiwa nalo ni serikali ina mpango gani wa kuhakikisha matatizo ya kiuchumi ya dunia hayaleti madhara makubwa nchini?

Je, serikali inampango gani wa kuandaa mfuko wa kuchochea uchumi (stimulus package) wa kwetu sisi wenyewe. Je ni jinsi gani tunaweza kuongeza ulaji wa ndani, ubora wa bidhaa, uzalishaji wa kisasa ili hatimaye tuweze kuchochea ajira, mauzo na ulaji wa ndani?

Je kuna mpango gani wa kuchochea utalii wa ndani wakati hao wa nje wanaanza kudorora? Kwanini serikali isitangaze kitu kama punguzo kubwa la bei za kutembelea mbuga zetu na kutangaza hata kwa wageni punguzo hilo na kufanya kuja Tanzania kwa wingi hasa kipindi hiki cha majira ya joto?

Je serikali ina mpango gani wa kusaidia viwanda binafsi vya ndani vimepata madhara kama mabepari Wamarekani na Waingereza wananvyofanya kusaidia viwanda vyao? Serikali inajua mpaka sasa ni sekta gani zimeeanza kuathirika?

Nimeamua kuchambua hotuba hiyo kwa kuwa hotuba ya rais inatakiwa kuwa kichochea cha mijadala. Ni katika kuzungumza kama taifa ndivyo tunavyofikia na kupata hoja bora na njia bora za kufanya mambo. Tukiacha kulumbana na kubishana kwa hoja, ndipo Watawala watakuwa wanatuhutubia na kutuburuza.

Tusikubali!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: