Kikwete amevunja sheria yake


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 April 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kujihalalisha kwa fedha badala ya sera.

Sasa kinahaha kutafuta mabilioni ya shilingi, siyo kwa ushindani, bali kwa shabaha ya kuzamisha vyama vingine.

Ilikuwa Ijumaa wiki iliyopita, CCM ilipozindua mpango wa kuchangisha Sh. 40 bilioni kwa ajili ya kile ilichoita “kampeni za uchaguzi mkuu.”

Lakini ni majuzi tu Rais Kikwete alisaini sheria ya matumizi ya fedha katika uchaguzi. Pamoja na kudhibiti matumizi ya fedha haramu, sheria hiyo ilikuwa na saaha nyingine kubwa.

Roho ya sheria ambayo Kikwete alisaini kwa mbwembwe, ingawa tayari imebainika kuwa itarejeshwa bungeni, ni hii hapa:

Sheria inalenga kupata “viongozi bila hila na jeuri ya fedha…” Maneno mengine katika sheria hii ni muhimu lakini haya tunayonukuu hapa ndiyo muhimu zaidi.

Sasa CCM imeamua kuchangisha fedha; kwa njia ya simu na kwa kukusanya kutoka kwa walionazo. Ukumbwa wa kiwango cha fedha kinachochangishwa, hakika ni wa kutatanisha.

Shilingi 40 bilioni (na zaidi) ni kiwango cha hila katika mazingira ya Tanzania, pale kinapotumika tu kwa kampeni za uchaguzi wa chama kimoja.

Kiasi hicho cha fedha ni cha jeuri ya aina yake katika jamii ambamo umasikini ni sehemu ya maisha.

Ni wazi basi kwamba viongozi watakaopatikana kwa hila na jeuri ya fedha, wataishi kwa hila na jeuri ya fedha juu ya vichwa vya masikini ambao watazuiwa kukohoa.

Kwa CCM kuamua kuchangisha mabilioni hayo ya shilingi kwa matumizi katika uchaguzi, chama hiki kimebwaga moyo wa sheria inayokataza hila na jeuri ya fedha.

Kimefanya hivyo makusudi. Kwanza kinataka kutishia vyama vingine kuwa “kiko juu” na hakina mshindani katika kuwa na fedha nyingi.

Pili, kinatoa ishara kwa wafanyabiashara wakubwa nchini kwamba wakati wa kukichangia ndio huu na mchango sharti uwe mkubwa kuliko siku zote.

Wafanyabiashara hawa wanajua vema kwa nini huwa wanachangishwa na wao kukubali kuchangia, kama hawana manufaa na “kelele za siasa.”

Tatu, CCM ina mtaji mkubwa wa michango. Ni mwenyekiti wake aliyesamehe watuhumiwa wa ufisadi waliodaiwa kuchota mabilioni ya shilingi kutoka benki Kuu (BoT).

Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete hakutaja majina na watuhumiwa, kiasi walichodaiwa kuiba, kiasi walichorejesha na kiasi hicho kiko wapi.

Ahadi yake ya kutowashitaki iwapo watarejesha fedha, ni mtaji mkubwa. Watuhumiwa hao ambao tayari wamethibitika kuwa mafisadi kwa kuwa wamekiri, wanatarajia kuchanga kiasi gani kwa njia ya shukrani?

Nne, kuna wananchi mitaani ambao, katika vibanda vyao vya matembe, ajira zao zisizosalama, uchuuzi wao unaopigwa vita kila siku na matarajio ya kuvaa kijani kila uchaguzi, watachanga Sh. 300 au 500.

Huwezi kubishana na hawa. Ndio waendelezaji wa kauli za kuwa “damu-damu” na CCM. Wakati mwingine husema wana damu ya kijani. Nao watachanga.

Chama Cha Mapinduzi kinataka kitu kutoka kwa kila mtu; ili kipate fedha na hivyo kupata viongozi kwa hila na jeuri ya fedha.

Na siyo kweli kwamba CCM itapata Sh. 40 bilioni tu. Kwa mkakati wake huu, itapata mabilioni mengi zaidi; labda mara mbili au mara tatu ya kiwango kinachotajwa hadharani.

Tutasikia kelele kwamba kitu muhimu ni kuripoti umepata kiasi gani cha fedha na umezitumiaje katika uchaguzi. Hizi ni kauli za “danganya toto.”

Kwa ubabe wa CCM na serikali yake; ule wa kukataa kutaja mafisadi waliothibitika; kukataa kusema waliiba kiasi gani na wamerudisha kiasi gani; na hatimaye kukaidi kuwapeleka mahakamani; nani atawalazimisha kutamka wamekusanya kiasi gani kwa mfumo wao wenyewe?

Kwa ukaidi na ubabe wa CCM na serikali yake; ule wa kuweka viongozi wa siasa katika sheria ya matumizi ya fedha wakilenga kudhibiti upinzani ndani na nje ya chama chao; nani atalazimisha chama na serikali yake kuwa waadilifu?

Katikati ya ahadi na mbinu za kukusanya mabilioni ya shilingi, ziko wapi mbwembwe za rais wakati wa kutia saini sheria ya kuzuia matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi?

Uko wapi utukufu wa waliomsindikiza rais kusaini sheria ya kuzuia matumizi ya fedha haramu katika uchaguzi? Kwa maandalizi haya, CCM na serikali yake “hawajafuta” sheria aliyosaini rais?

Sheria yenyewe ina matundu. Hakuna kipengele chochote katika sheria hii ambacho kinazuia mafisadi kuchangia chama.

Hatujaona, katika kanuni zinazojadiliwa, kipengele chochote kinachowazuia mafisadi kuingiza fedha katika kampeni za vyama vya siasa.

Kama vifungu hivi havimo na kama ukusanyaji fedha uko chini ya chama chenyewe ambako uwazi ni hadhithi za alinacha, basi mafisadi waliosetiriwa na kunusurishwa mahakama, wamepata fursa ya kutoa asante.

Tayari ubabe wa CCM na serikali yake umeanza kudhihirika. Kwa mfano, wadau walipendekeza na kukubaliana kuwa kiwango cha juu cha fedha kwa mgombea ubunge kwa upande wa Zanzibar, kiwe Sh. 10 milioni.

Lakini CCM imepenyeza pendekezo ambalo tayari linaonekana kukubaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kwamba mgombea ubunge Zanzibar atumie Sh. 40 milioni.

Uamuzi wa Tendwa na CCM yake, haukujali ukubwa wa majimbo ya Zanzibar kama sheria inavyoagiza; wala idadi ya wapiga kura.

Majimbo mengi ya Zanzibar ni madogo; yenye wapigakura wachache; pengine chini ya 10,000 na kijiografia ni madogo.

Mahali pengine, viwango vilivyopenyezwa na CCM na kukubaliwa na Tendwa kwa majimbo ya Zanzibar, ni vikubwa kuliko vile vya Bara.

Kwa staili hii, hata Tendwa mwenyewe amepoteza sifa ya uadilifu na ile ya kuwa msajili wa vyama vya siasa kwa sababu ya kukumbatia matakwa ya chama kimoja dhidi ya vingine.

Na hii, inaufanya mchakato mzima wa kutunga sheria hadi kuisaini kuonekana hauna maana na hauzingatii maslahi ya taifa.

Watanzania wengi wataendelea kujiuliza, kama Kikwete ana uwezo wa kuchangisha mabilioni yote hayo kwa uchaguzi wa kumwongezea miaka mitano ikulu, anashindwa nini kuchangisha mabilioni ya kuleta maisha bora aliyoahidi.

Itakuwa vigumu kutetea Kikwete kwamba fedha anazokusanya hazitatumika kununua kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: