Kikwete amlinda Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 January 2010

Printer-friendly version
Amuweka pabaya Mwinyi

RAIS Jakaya Kikwete ameelemewa. Ameagiza itafutwe suluhu na watuhumiwa wa ufisadi, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zinasema rais ameagiza Kamati ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kutafuta suluhu kati na baina ya watuhumiwa na wale ambao wanawatuhumu.

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kuwa Kamati ya Mwinyi imependekeza, katika ripoti yake, kuvuliwa nafasi za uongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), vigogo wanne watuhumiwa wa ufisadi.

Waliotajwa ni Edward Lowassa, Rostam Aziz, Nazir Karamagi na Andrew Chenge.

Taarifa za ndani ya serikali na CCM zinasema mara baada ya Rais Kikwete kupokea ripoti ya Kamati ya Mwinyi hivi karibuni na kusoma mapendekezo yake, alibaini kuwa baadhi ya mapendekezo ya kamati “hayatekelezeki.”

Pendekezo moja ambalo Kikwete ameona ni gumu ni lile linalotaka achukue hatua ya kuwavua uongozi baadhi ya maswahiba wake “ili kukinusuru chama na mgawanyiko kabla ya uchaguzi mkuu.”

Rais Kikwete amenukuliwa akiwaeleza wajumbe wa kamati hiyo, “Nendeni mkayamalize. Huu ni mwaka wa uchaguzi. Hatuwezi kuendelea na haya; yaishe kabla ya uchaguzi mkuu.”

Mkutano wa Rais na wajumbe wa Kamati ya Mwinyi ulifanyika ikulu, Dar es Salaam wiki iliyopita.

Gazeti hili liliripoti wiki iliyopita kuwa Ripoti ya Mwinyi imevuja na ilikuwa mikononi mwa watuhumiwa.

Lilisema kutokana na hali hiyo, ripoti ya Mwinyi ingepata upinzani mkali katika NEC kutokana na watuhumiwa kuwa na ushawishi mpana.

Hata kabla hoja ya suluhu haijatoka, kulikuwa na taarifa kwamba watuhumiwa, baada ya kupata taarifa, walikuwa wamemaliza mzunguko katika mikoa ya kanda ya Ziwa Viktoria wakitembelea wajumbe wa NEC.

Tayari mwenyekiti wa kamati ameanza jitihada za kukutana na kujaribu kupatanisha Lowassa na Spika wa Bunge, Samwel Sitta.

Aidha, mjumbe mmoja wa kamati ameripotiwa kwenda kwa Lowassa na “kumtaka maoni juu ya kumaliza mgogoro.” Jitihada hizo hazijazaa matunda yoyote.

Tangu tuhuma dhidi ya akina Lowassa zipambe moto ndani ya bunge, watuhumiwa wamekuwa wakidai kuwa Spika Sitta ndiye anayechangia wao kusakamwa.

Taarifa zinasema ni kutokana na hali hiyo, Kamati ya Mwinyi ilitaka kuwakutanisha Lowassa na Sitta kwa madai kwamba “watamaliza tofauti zao.”

Hata hivyo, taarifa zinasema wapinga ufisadi walioko upande wa Sitta wameng’ang’ania kuwa hakuna ugomvi kati ya Sitta na Lowassa.

“Kilichopo ni kwamba kuna mafisadi na wapinga ufisadi. Hili haliwezi kufanywa suala la binafsi. Spika Sitta hana lolote la kupatana na Lowassa,” mmoja wao ameliambia gazeti hili.

Miongoni mwa wanaopinga ufisadi ambao walikuwa wakimsubiri Sitta atoke kwa rais ili wajue msimamo wake, walikuwa ni pamoja na wabunge na mawaziri.

Taarifa nyingine ambazo hazikuweza kuthibitishwa haraka zinasema Sitta, baada ya kupewa taarifa za kupatanishwa na Lowassa, alikwenda moja kwa moja kumwona rais kutaka kujua iwapo hiyo ilikuwa amri yake.

Mtoa taarifa ameeleza kuwa Rais Kikwete alikana kuagiza suluhu kati ya Sitta na Lowassa lakini ameripotiwa kuagiza kamati itafute “njia zozote ili mambo haya yaishe kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi.”

Juhudi za kuwapata Sitta na Mwinyi ili kutoa maelezo kuhusu hili, hazikuzaa matunda.

Hatua ya sasa ya rais inaiongezea mzigo Kamati ya Mwinyi. Hadidu zake za rejea za awali zilihusu kutafuta chanzo cha mivutano na migogoro kati ya bunge na serikali na kati ya serikali na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Hadidu zilitaka pia kamati ipendekeze jinsi ya kuondoa mivutano na migogoro hiyo. Sasa Kamati imetwisha mzigo wa “kutafuta suluhu.

Kamati ya Mwinyi iliundwa na Kamati Kuu ya CCM, Septemba mwaka jana. Wajumbe wake wengine wawili ni Abdulrahman Kinana na Pius Msekwa.

Kamati imewatuhumu Lowassa, Rostam na Karamagi kujenga makundi yenye shabaha ya kujisafisha ambayo yamedhoofisha chama na serikali.

Watatu hawa wanatuhumiwa katika kashfa ya mradi wa kufua umeme wa dharura wa Richmond.

Kwa upande wake, Chenge ametuhumiwa kuaibisha chama kutokana na tuhuma nzito za ufisadi zinazomkabili.

Hatua ya rais kuzungumzia suluhu, imeelezwa na wachunguzi wa mambo ya siasa kuwa ni “kukimbia kuchukua maamuzi magumu.”

Kwa njia hii, wamesema rais atakuwa anakiumiza chama kuliko kama angeamua kutosa watuhumiwa wa ufisadi.

Mbunge mmoja, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, amesema kwamba kwa utaratibu huu, “jambo hili linaweza lisimalizike hadi baada ya uchaguzi mkuu.”

“Lakini sharti tukubaliane kuwa jambo hili ni hatari kwa mustakabali wa chama chetu,” alisema.

Amesema suluhu yoyote ile itakuza mgogoro, kudhoofisha chama na kuwapa jeuri watuhumiwa wa ufisadi wanaoona chama “kinawaogopa.”

Tayari kundi linalotaka “mafisadi watoswe” limehusishwa na usajili wa chama kipya CCJ – Chama Cha Jamii. Tayari chama hicho kimepewa usajili wa muda.

Alhamisi iliyopita, siku moja baada ya gazeti hili kuandika kuwa baadhi ya vigogo ndani ya CCM wameanzisha chama kipya, CCJ kiliwasilisha maombi ya usajili jijini Dar es Salaam kwa kutumia watu ambao siyo maarufu kisiasa au kiharakati.

Akizungumza na MwanaHALISI juzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alisema hakuna cha kushangaza katika CCJ kuomba usajili na kwamba kuna maombi mengine ya vyama vingine.

Alipotakiwa kutoa majina ya wadhanini wa chama hicho, Tendwa alisema, “Baada ya miezi sita, kila kitu kitakuwa wazi. Wadhamini watajulikana kwa sababu sisi (Ofisi ya Msajili) ndiyo tutakaowahakiki. Kila kitu kitakuwa wazi tu. Kuweni na subira,” alisema.

Kwa mujibu wa Tendwa, fomu za chama hicho zinaonyesha Mwenyekiti wa muda ni Richard Kiyabo na Katibu Mkuu ni Renatus Muhabi.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: