Kikwete amliza Lowassa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly version
Asema mkataba hauna maslahi
Aelekea kuunga mkono Nape
Edward Lowassa

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete amesema mkataba wa mradi wa ujenzi wa kitegauchumi cha Umoja wa Vijana (UV-CCM), una dosari nyingi na haukubaliki kama ulivyo, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za ikulu zinasema rais ameagiza utekelezaji wa mkataba usitishwe hadi dosari hizo zitakapoondolewa.

Katika mawasiliano rasmi na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, ya 3 Julai 2008, rais ameelekeza yafanyike mazungumzo baina ya Makamba, Mwenyekiti wa UV-CCM Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Isack Francis kuweka msingi wa kurekebisha mkataba huo.

Hatua ya Kikwete inalenga kuzuia UV-CCM kutumbukia katika mgogoro wa kisheria na kuweka mbele ?maslahi ya Umoja wa Vijana.?

Rais amesema mkataba umebainika kuwa na mapungufu mengi ya kisheria ambayo lazima yarekebishwe ?ili tusipoteze maslahi katika mradi huu.?

Barua ya Kikwete kwenda kwa Makamba, ambayo gazeti limeona nakala yake, inahusu mkataba wa ukarabati/upanuzi wa Jengo la Umoja wa Vijana na ujenzi kwenye viwanja Na. 108/2 vilivyoko Barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Nape Nnauye alisema tarehe 22 Julai mwaka huu kwamba Baraza la Wadhamini la umoja wao, chini ya Edward Lowassa liliingiza UV-CCM katika mkataba unaonuka ufisadi na usio na manufaa kwa umoja huo.

Alisema baraza la Lowassa halikuwa na madaraka ya kufikia maamuzi hayo kwa sababu ?Baraza Kuu la UV-CCM, lenye mamlaka ya uamuzi wa mwisho, lilikuwa halijaridhia mkataba huo.?

Kwa mwezi mmoja sasa kumekuwepo kutupiana lawama kati ya wajumbe wa Baraza Kuu la UV-CCM na Baraza la Wadhamini chini ya mwenyekiti wake Lowassa.

Wakati Baraza Kuu limesema halikuhusishwa katika suala la mkataba kati ya UV-CCM na mfanyabiashara Subhash Patel kwa ajili ya ujenzi wa mradi unaokadiriwa kufikia Sh. 40 bilioni, Makamba na Lowassa wamekuwa wakidai kuwa mkataba haujafikiwa wala kuwekwa saini.

Hata hivyo ujenzi unaendelea kwenye viwanja husika na tayari rais amesema mkataba hauna manufaa kwa umoja huo hadi utakapofanyiwa marekebisho.

Mara ya kwanza MwanaHALISI lilipoandika taarifa kuhusu mkataba wa UV-CCM, Lowassa alitishia kushitaki gazeti akisema ?limezidi? kumzulia uwongo. Hajaenda mahakamani.

Dosari ambazo zimemstua rais ni pamoja na ile ya kukiuka Sheria ya Ardhi. UV-CCM wameridhia asilimia ya miliki ya ardhi (kiwanja) kuhamishiwa kwa wabia kabla shughuli yoyote ya ujenzi kuanza.

Utaratibu ni kwamba kabla hatua hiyo haijachukuliwa, sharti Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali atoe kibali kwa ajili ya uhamisho wa aina hiyo.

Yote haya yalifanyika bila kumfahamisha rais; bila kupitishwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM na bila kupelekwa na kubarikiwa na Baraza Kuu la UV-CCM.

Mkataba wa ujenzi wa mradi huo ulioenda kwa kichwa kisomekacho: ?Development Agreement? ulisainiwa tarehe 2 Januari 2007 kati ya UV-CCM na makampuni mawili ya M.M. Integrated Steel Mills (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL).

Kasoro nyingine ambayo ilimstua rais ni uhamisho wa miliki ya ardhi kutokuwa na ukomo wa muda wa miliki. Mkataba unaacha eneo hilo kama kwamba uhamisho ni wa milele na milele.

Aidha, mkataba ambao rais ametilia mashaka na kukataa hadi utakaporekebishwa, hauonyeshi nafasi ya UV-CCM katika uendeshaji wa mradi pale ujenzi utakapokuwa umekamilika.

Lingine ambalo linaoenekana kuwa chanzo cha mitafaruku katika siku za usoni, ni uhusiano kati ya mbia mmoja ? MMISML na mwingine, ambaye hakika ni mkandarasi wa ujenzi ? ECCL.

Kinachostahili hapa ni kufafanuliwa kwa kina nafasi ya mbia na mkandarasi ili maslahi ya UV-CCM yasiingie kwenye mgogoro.

MwanaHALISI limesoma mkataba wa UV-CCM kwa makini na kugundua kuwa hauelezi kiasi cha uwekezaji kutoka kwa wabia ambacho kinaweza kutumika kueleza mgawo wa asilimia 25 ambazo inadaiwa UV-CCM watachukua.

Wataalam wa sheria wanasema ilibidi mkataba ueleze asilimia 25 ni sawa na eneo lipi la ardhi ya sasa au vitegauchumi vipya vinayotarajiwa kujengwa.

Mradi wa vijana, katika hali ambayo haiwezi kuelezeka kitaalam, hauna ufafanuzi wa matumizi na mapato hatua kwa hatua; jambo ambalo linaonyesha kutokuwa makini au kuashiria ghiliba katika mahusiano ya wabia.

Vilevile mkataba hauelezi iwapo ubia ni wa miliki ya pamoja au itaundwa kampuni tofauti ya kuendesha kitegauchumi.

Gazeti hili limeona barua ya Makamba ya 9 Julai 2008 inayopendekeza kikao kati yake na viongozi wa UV-CCM wiki moja mbele, lakini ujenzi bado unaendelea hadi sasa; takriban mwezi mmoja baada ya Rais Kikwete kuingilia kati.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Muleba Kusini Wilson Masilingi amekana kushiriki maamuzi yaliyoingiza UV-CCM katika mradi wenye utata.

Masilingi alikuwa akijibu swali kwa nini hakutoa ushauri kwa umoja huo wakati yeye ni mjumbe wa Baraza la Wadhamini.

?Sikiliza bwana, mimi sijui lolote. Sikushirikishwa katika hilo. Niliposikia kelele zinaanza, nikamwona Lukuvi (William, Mkuu wa Mkoa Dodoma) na kutaka tukutane na kujadili,? alisema Masilingi.

Alisema Lukuvi alimwambia kuwa yeye siyo mjumbe tena wa Baraza; ?kwamba niliishatolewa na nafasi yangu amechukua Karamagi (Nazir, Mbunge Bukoba Vijijini).?

Hata hivyo Masilingi amesema kinachomsikitisha ni kuona waliomweka (Baraza Kuu la UV-CCM) siyo waliomwondoa na hivyo vijana wanamwona kama alishiriki kutoa maamuzi.

?Sina barua ya kuniondoa. Walioniondoa hawakunipa hata barua ya kunishukuru. Kinachoniuma ni vijana kufikiri kuwa hata mimi ni mmoja wa walioandaa mkataba wenye utata,? alisema Masilingi.

Masilingi anasema alipokutana na Mwenyekiti wa UV-CCM Nchimbi, na kumuuliza mbona hakushirikishwa katika suala la mkataba huo, alimjibu kuwa anakwenda kuangalia kwenye orodha kama bado yupo, lakini akaongeza, ?nadhani ulikwisha badilishwa.?

Nchimbi alimkumbusha Masilingi kuwa wajumbe wa Baraza la Wadhamini wanabadilishwa baada ya miaka mitano, ?lakini nikashangaa, mbona wenzangu niliongia nao bado wamo?? alihoji Masilingi kwa kicheko.

Kuhusu mkataba wenyewe, Masilingi amesema, ?Katika dunia sijawahi kuona mkataba ovyo kama huu, usiokubalika katika misingi yoyote ya maadili.?

Masilinga anasema hati za kimila zinatambulika benki; itakuwaje hati rasmi za serikali za kiwanja kilichoko katikati ya jiji kama viwanja vya UV-CCM.

Anasema Umoja wa Vijana wangechukua hati yao; wakaenda benki kukopa; wakapata fedha na kumpa mkandarasi yeyote, hata Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwajengea na ?siyo kuingia katika mkataba wa kijinga kama huu.?

Masilingi, mmoja wa wanasheria wanaoaminika nchini, anasema ameona nakala ya mkataba na amejiridhisha kuwa kilichosainiwa na kuwezesha wabia kuanza ujenzi, ni mkataba halisi na si vinginevyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: