Kikwete amtelekeza Sitta


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 18 August 2009

Printer-friendly version
Aruhusu 'mafisadi' kumsulubu
Mpasuko mkubwa CCM waja
RAIS Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ameshindwa kulinda hadhi ya Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta katika vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.

Akiwa mwenyekiti wa chama hicho, Kikwete aliwaacha wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kumtuhumu Sitta kuwa aanatumia bunge kujeruhi chama na serikali yake.

Alikuwa mbunge wa kuteuliwa na rais, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyemkana na kumsulubu kwa kauli kali akisema "…Sitta ametwaa madaraka vibaya kwa kuahidi wabunge kuboresha maslahi yao."

"…Huyu Sitta amepata madaraka kwa rungu la ulaghai. Alihadaa wabunge kwamba wakimchagua ataboresha maslahi yao.," Ngombale alinukuliwa na mtoa habari akisema ndani ya kikao cha NEC.

Aliongeza kuwa Sitta "Amechapisha hata kitabu, tena nje ya nchi kinachoitwa, 'Bunge lenye meno.' Haya ni meno dhidi ya serikali ya CCM," amenukuliwa na akisema.

Ngombale aliongea kwa kudhamiria. Alisema "Sitta anahutubia sana Bunge kuliko mbunge mwenyewe. Anapenda wabunge wa upinzani kuliko wa CCM. Tabia yake hii, ameipandikiza hata kwa naibu spika na wenyeviti wake wa Bunge," Ngombale alinukuliwa aking'aka.

Lakini pamoja na tuhuma nyingi na nzito, wote walioongoza genge la "Kummaliza Sitta" kwa kumtoa uspika na hata kumfukuza kwenye chama, waliishia kunywea.

Naye Sitta, baada ya kusikiliza tuhuma, shutuma, kejeli, lakini na busara za rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Waziri Kiongozi wa Zanzibar Shamsi Vuai Nahodha, alipoza munkari wa wajumbe kwa njia ambayo mwanasiasa yeyote mzoefu angefanya.

Sitta alisema, "Kufanya kosa si kosa; kosa ni kurudia kosa." Hapo ndipo baadhi ya mahasimu wake walitazamana huku wakishindwa kucheka au kuendelea kununa.

Mtoa habari aliliambia MwanaHALISI kuwa hata wakati wa kutoka ukumbini, baadhi ya wajumbe walikuwa wakijiuliza, "Kwa kosa anasema nini? Kwamba angeasi na kuhama chama au kweli amekiri tuhuma alizotwishwa?"

Awali katika kikao cha Kamati Kuu cha Jumamosi na Jumapili, Sitta anaripotiwa kugeuka mbogo na kueleza kwa undani kile alichosema kinachosumbua serikali.

Mtoa taarifa alimnukuu Sitta akisema wakati "mtandao wa Kikwete" ulipokuwa unaomba ridhaa kwa wananchi, wao (akiiwemo yeye) hawakupanga kutumia nafasi hiyo kutafuta utajiri.

"Kama tunataka kuiba na kulea ufisadi, basi sawa. Lakini ni muhimu twende kwenye mkutano mkuu ili kubadilisha katiba ya chama chetu. Tukawaambie wanachama wetu, kwamba CCM imebadilika kutoka chama cha kutetea wanyonge na kuwa chama cha kulea mafisadi," alisema mtoa taarifa akimnukuu Sitta.

Kauli ya Sitta iliamsha munkari wa baadhi ya wajumbe waliokuwa wamebeba hoja kuu ya kumfukuza Sitta na wabunge wenzake waliotajwa kuwa 11ambao wanapiga vita ufisadi.

Katika kikao cha NEC ambacho kiliendelea hadi usiku wa Jumatatu, Asha Bakari Makame, makamu mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), alisema Sitta anapasua chama na kwamba ndicho chanzo cha matatizo.

Asha alisema kwa sauti ya kufoka, kuwa Sitta aondoke na "kubakisha hapa kadi yetu."

Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, akijibu hoja ya upatanishi, alinukuliwa na mtoa taarifa akisema kwamba hakuna upatanishi unaoweza kufanyika.

Alisema mgogoro uliomo ndani ya chama unatokana na makundi mawili; moja linalopinga ufisadi na lile linalounga mkono ufisadi.

"Ugomvi huu utaisha pale ufisadi utakapomalizika. Zaidi ya hapo, hakuna kinachoweza kuzungumzwa na kumaliza ugomvi wetu," alisema Mwakyembe.

Kwa mujibu wa taarifa, baadhi ya wajumbe watetezi wa Sitta walipokuwa wakiongea, zilikuwa zikisikika sauti za kuzomea, jambo ambalo lilimfanya mwenyekiti Kikwete kuingilia kati.

Kwa mfano, mbunge wa Igunga, Rostam Aziz alinukuliwa akisema, "Sikujua kama huyu ana akili ndogo kiasi hiki." Ilikuwa ni wakati mjumbe mwingine, Injinia Stella Manyanya alipokuwa akitetea Spika Sitta.

Manyanya alinukuliwa akisema, "Sitta ni mmoja wa viongozi wa kupigiwa mfano nchini."

Mtoa taarifa anasema baada ya Rostam kushambulia Manyanya, Nape Nnauye, aliyesikia kauli ya Rostam, alijibu kwa kusema, "Wewe usiyeelewa kinachosemwa, ndiyo mwenye akili ndogo."

Akizungumza katika siku ya kwanza ya kikao cha NEC, Nape alisema jina la Rais Kikwete linatumiwa vibaya na baadhi ya wasaidizi wake. Alisema baadhi yao wamo katika mkutano ule na kwamba rais angewakana hadharani.

Alitoa mfano wa sakata la Daniel ole Porokwa, Katibu Msaidizi wilaya ya Hanang, aliyefukuzwa kazi na Katibu Mkuu Yusuph Makamba kwa kisingizo cha "agizo kutoka kwa mwenyekiti Kikwete."

Hoja ya ufisadi iliyotajwa na Mwakyembe ilikuwa imeibuka mapema katika Kamati Kuu pale mjumbe Abdulrahman Kinana aliposimama upande wa Sitta na kusema, huku akitoa macho kuwa "Tuhuma za ufisadi zinazokabili baadhi ya viongozi ndizo zinaangamiza CCM."

Katika hali ambayo haikutegemewa, Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Ngenda Kirumbi alimbeza Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginard Mengi, akisema kwanza si mwanachama wa CCM.

"Huyu Mengi si mwana-CCM. Namshangaa dada yangu Chilolo (Diana Chilolo mjumbe wa NEC), kusema kuwa Mengi ni mwanachama safi. Huyu Mengi ni mtu tu. Mimi nimekwenda hadi kwa balozi wa shina na katika tawi linalodaiwa kuwa Mengi ni mwanachama. Hajasajiliwa huko. Uanachama wake ni feki. Mimi siujui," alisema Kirumbi huku akimtolea macho Chilolo.

Miezi michache iliyopita Mengi alifanya ziara mkoani Singida na kwenye mkutano, Chilolo alimtaja kuwa mwanachama mzuri wa CCM. Kwenye mkutano, Mengi alichanga Sh. 100 milioni kwa ajili ya Saccos ya akinamama.

Sitta amebaki na nafasi yake ya spika na amebaki na kadi yake. Wachunguzi wa mambo wanasema inawezekana hazikuchukuliwa hatua dhidi yake kwa vile walihofia angechukua uamuzi mkali wa kuhama chama ambao ungekiumiza.

Mjadala wa kumsulubu Sitta ulitokana na mada iliyowasilishwa ndani ya vikao ambayo ilihusu hali ya kisiasa nchini, ndani ya CCM na nje ya chama hicho.

Naye mwenyekiti Kikwete,pamoja na kusema kuwa anampongeza Sitta kwa ujasiri wake, alionyesha wasiwasi wake jinsi spika anavyoendesha shughuli zake.

Alisema mambo ya ufisadi wanayojadili sharti iwe kwenye vikao vya chama na siyo bungeni; kwani yakipelekwa bungeni wanakuwa wameifanyia kazi kambi ya upinzani.

Kamati Kuu imeunda kamati ndogo ya watu watatu – Ali Hassan Mwinyi, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana kutafuta mahusiano kati ya bunge na kamati ya wabunge ya CCM.

Ukiacha mpambano huo kati ya Sitta na kundi zima la CCM, kitendo cha Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kutohudhiria vikao hivyo kuanzia CC hadi NEC, nacho kilizua maswali mengi miongoni mwa wajumbe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: