Kikwete amtosa Chenge kujinusuru


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 April 2008

Printer-friendly version
Pinda alishinikiza 'asulubiwe!'
Wabunge waliteta kumfukuza
Andrew Chenge

SIRI ya kumtosa bilionea Andrew Chenge ni "kunusuru hadhi ya serikali inayotota" katika kipindi cha kilio cha wananchi dhidi ya ufisadi, MwanaHALISI limeelezwa.

Tayari imefahamika pia kuwa shinikizo la Chenge kujiuzulu limetokana na woga wa serikali ya Rais Kikwete kuja kushinikizwa na Bunge kumfukuza mwansheria mkuu huyo wa zamani.

Taarifa za ndani ya Bunge zinasema baadhi ya wabunge walikuwa wamejipanga kupeleka hoja binafsi, au kushinikiza kupitia kwa waziri mkuu, ili Chenge ajiuzulu.

Taarifa za Ikulu Dar es Salaam zinasema Rais Kikwete alikuwa tayari ana mawasiliano na Waziri Mkuu Mizengo Pinda juu ya "umuhimu" wa Chenge kujiuzulu.

Imeelezwa kwamba Pinda aliishamweleza rais kwamba "ni vema mtu wako akaondoka, akakupunguzia mzigo."

Kauli hiyo inaendana na taarifa za awali kwamba Pinda alishasema hadharani kuwa yeye hakuomba kuwa waziri mkuu na kwa hiyo hatakubali kubeba mtu wa "kumchafulia."

Hayo yanathibitishwa na kauli ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, aliyesema juzi kuwa rais alikuwa tayari anatarajia uamuzi wa Chenge kujiuzulu.

Chenge aliyekuwa Waziri wa Miundombinu alijiuzulu wadhifa wake Jumapili. Anakuwa waziri wa nne kujiuzulu katika mazingira yanayohusisha ufisadi ulioghubika taifa kwa takribani miaka kumi sasa.

Chenge anakabiliwa na tuhuma nyingi na nzito za kuwa na akaunti za benki katika nchi za nje ambazo MwanaHALISI hadi sasa limegundua kuna zaidi ya Sh. 25 bilioni ambazo upatikanaji wake unatiliwa mashaka.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwa hali yoyote ile Chenge atakuwa hakutaja, katika fomu za wabunge za kutaja mali zao, utajiri wake ulioibuliwa na kuanikwa hadharani na vyombo vya habari.

Kama hivyo ndivyo, ukiukwaji wa maadili ulioambatana na utajiri wenye utata, unamwondolea Chenge uadilifu wote na unaweza kumgharimu hata ubunge wake.

Mwishoni mwa wiki iliyopita baadhi ya mabalozi wa Umoja wa Ulaya, Finland na Uholanzi walitembelea bungeni Dodoma ambapo, pamoja na mambo mengine, walikuwa wakifuatilia taarifa za ufisadi na hatua ambazo serikali inachukua kuukabili.

Kiongozi mmoja wa wa ngazi ya juu katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameliambia MwanaHALISI kuwa chama chake hakiko tayari kumlinda Chenge na hivyo kuhatarisha sifa yake mbele ya wanachama na wananchi kwa ujumla.

Amesema, "Chama kipo tayari hata kupoteza jimbo lake kwa maana ya kuchukuliwa na upinzani, lakini kisipakwe matope kwa ajili ya mtu mmoja."

Jimbo la Chenge, Bariadi Magharibi, lilipokonywa kwa United Democratic Party (UDP) ambacho mbunge wake alikuwa Isaack Cheyo.

Mawaziri wengine waliojiuzulu ni Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu, Dk. Ibrahim aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki na Nazir Karamagi aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Wote hawa walikumbwa na kashfa ya upendeleo kwa kampuni feki ya Richmond iliyoingia mkataba na serikali kuzalisha umeme wa dharura wa megawati 100. Ilishindwa kufanya hivyo kwa kutokuwa na uwezo kifedha na kiufundi.

Chenge ambaye alikuwa ameanza kuitwa "bwana vijisenti" kutokana na kauli yake kuwa mabilioni yaliyokutwa kwenye akaunti yake Ulaya yalikuwa vijisenti tu, ameondoka kimyakimya baada ya kuwasiliana na rais wake.

Rweyemamu, akiongea katika kipindi cha BBC juzi Jumatatu asubuhi, alisema kitendo cha Chenge kujiuzulu kinaonyesha kile alichoita "ukomavu wa kisiasa na mfano wa kuigwa wa umakini wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete."

Wki mbili zilizopita Kikosi Maalum cha Upelelezi wa Ufisadi Sugu cha Uingereza, kilinukuliwa na gazeti moja la Uingereza, The Guardian, kikisema Chenge ana zaidi ya Sh. 1.2 bilioni kwenye akaunti binafsi iliyoko kisiwa cha Jersy.

Hata hivyo taarifa za uhakika zilizochapishwa na MwanaHALISI zinasema akaunti hiyo ya Jersy ina Euro 3 milioni, sawa na Sh. 6 bilioni. Ni kutoka kwenye akaunti hii zilichotwa dola 600,000 kwenda kwenye akaunti ya "bosi" wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa shughuli ambayo haijafahamika.

Katika akaunti ya Uswisi, Chenge anamiliki dola 467,000 sawa na nusu bilioni, fedha ambazo zilichotwa kwenye akaunti ya kampuni ya TANGOLD iliyopo tawi la NBC Limited makao makuu.

Akiwa Mkurugenzi wa TANGOLD na mwidhinishaji malipo, Chenge anasimamia pia mabilioni katika akaunti mbili za kampuni hiyo zilizoko NBC Limited makao makuu.

Akaunti moja ya fedha za kigeni Na. 011105011782 ina akiba ya dola 12,997,950.84 sawa na Sh. 15 bilioni. Katika akaunti nyingine ya fedha za ndani, Na. 011103024852 ya tawi hilohilo, kuna Sh. 1,379,359,367.37.

Kwenye akaunti yake ya fedha za Tanzania katika NBC Limited, makao makuu, Chenge anamiliki Sh. 25,794,805.89 hadi 11 Aprili mwaka huu.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwa kadri Chenge alivyokuwa amekataa kujiuzulu, hatua hiyo aliyochukua siku tatu baada ya kung'akia waandishi wa habari wakati akitoka ziarani China, itakuwa imeshinikizwa na ikulu.

"Baada ya siri zake kuanikwa na yeye kushindwa kijitetea; na papo hapo kuonekana kuwa mzigo kwa utawala, wakubwa zake wameonelea wamtose ili kuepuka maswali mengi na magumu yanayohusu kwa nini anaendelea kukumbatiwa," ameeleza mmoja wa wachunguzi.

Kuondoka kwa Chenge kunafungua mlango wa mawaziri wengine, naibu mawaziri na watendaji wakuu wa serikali waliohusika na kashfa za ufisadi kujiondoa kazini kabla ya kulazimishwa.

"Haileti maana yoyote kwa waziri kujiuzulu lakini Katibu Mkuu na wakurugenzi wakabaki kazini," kimeeleza chanzo cha habari.

Hata hivyo imefahamika kuwa naibu mawaziri wawili huenda wakajiuzulu nafasi zao au kuondolewa wakati wowote kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili.

MwanaHALISI haikuweza kupata majina ya mawaziri hao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: