Kikwete amtosa Warioba


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version
Jaji Warioba

CCM Trust ni moja ya makampuni manne yanayounda kampuni ya Mwananchi Trust Limited yenye hisa katika kampuni ya Mwananchi Gold Limited (MGL) ya Dar es Salaam.

CCM imekana pia kumiliki Mwananchi Trust ambayo ni mbia katika Mwananchi Gold Limited. Warioba ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya MGL.

Gazeti hili lina taarifa kwamba CCM imekana kumiliki makampuni hayo mawili – Mwananchi Trust na CCM Trust na imeanika orodha ndefu ya makampuni yake.

Wachunguzi wa mambo wanasema hatua hiyo inamweka pabaya Warioba kwani amekuwa akidai kampuni hiyo inamilikiwa na chama tawala.

Taarifa kutoka serikalini zinasema baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa CCM tayari wamehojiwa na vyombo vya dola nchini kuhusiana na umiliki wa CCM Trust, Mwananchi Trust na kampuni mwavuli ya Mwananchi Gold Limited.

Kupatikana kwa taarifa za hatua hiyo ya CCM kumekuja takriban wiki mbili tangu Warioba atuhumu Rais Jakaya Kikwete kuingilia mkondo wa mahakama, hasa katika kesi zinazohusu ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

MwanaHALISI limegundua kuwa waraka wa CCM unaokana kampuni ya Warioba ulijadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, tarehe 2 na 3 Mei mwaka huu.

Waraka huo wenye kurasa 22 unaitwa, “Mkakati wa Chama Cha Mapinduzi kujiimarisha kiuchumi mwaka 2009 – 2012” na kampuni ya CCM Trust haionyeshwi kuwa mali ya CCM.

Kikao cha CC kilichojadili mkakati wa CCM kilifanyika Ikulu, Dar es Salaam, chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete.

Tarehe 13 Januari mwaka huu, Jaji Warioba alinukuliwa na waandishi wa habari ofisini kwake Masaki, Dar es Salaam, akisema kuwa Kampuni ya Mwananchi Trust inamilikiwa na CCM na kwamba ina hisa 15.

Mwananchi Trust ina hisa katika Mwananchi Gold Limited ambayo anaongoza Warioba na ambayo imekuwa ikituhumiwa kutumia vibaya mabilioni ya shilingi kutoka BoT. Fedha hizo zililenga “kusaidia wachimbaji wadogo” wa dhahabu nchini.

Kwa mujibu wa nyaraka za Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA), wenye hisa katika Mwananchi Gold Limited ni BoT yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lenye hisa 375 na Chimera Company Limited, ya anayetajwa kuwa “raia” wa Italia, yenye hisa 500.

Taarifa zinaonyesha kuwa kampuni ya CCM Trust inamilikiwa na Jaji Warioba na Yusuf Mushi. Pamoja na kuwa mwenyekiti wa bodi MGL, Warioba pia ana hisa katika kampuni hiyo.

Hisa za Warioba katika MGL zinapitia kampuni ya familia yake inayoitwa Umoja Entertainment Limited (UEL).

Nayo kampuni ya Mwananchi Trust inabeba hisa za Vulfrida Mahalu kupitia kampuni ya VMB Ltd.; Yusuf Mushi kupitia kampuni ya Y.M. Limited na CCM Trust.

Warioba alipoombwa na gazeti hili kufafanua juu ya CCM kukana kampuni ya Mwananchi Trust na CCM Trust alisema, “No comment” (Sina la kusema). Aliendelea kusema, “Ninyi andikeni wanayosema, lakini kwangu mimi, no comment.”

Awali Warioba alimwambia mwandishi kuwa madai juu ya makampuni hayo aliishayajibu mara nyingi na kuuliza, “Kuna nini?”

Hadi sasa Rais Kikwete hajasema lolote juu ya Warioba na makampuni husika; bali wiki mbili zilizopoita, rais alisema kesi tatu kubwa za ufisadi zitafikishwa mahakamani. Haijulikani iwapo katika hizo kuna inayomhusu Warioba.

MwanaHALISI liliwasiliana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba juu ya suala hilo; naye alisema si Mwananchi Trust wala CCM Trust kuwa ni mali ya chama hicho.

“Hiyo CCM Trust si kampuni yetu. Hatuifahamu na wala haimo katika orodha ya makampuni ya CCM,” alisema Makamba.

Alipoulizwa kama kampuni ya CCM Trust haina uhusiano na chama chake, iweje hawajachukua hatua ya kuwashitaki waliotumia jina hilo kwa vile wanaweza kuingiza chama katika migogoro, Makamba alisema, “Hayo mengine ya baadaye. Kwa sasa nakueleza hivyo. Hii si kampuni yetu.”

Katika kukana kumiliki makampuni hayo, CCM imetoa kwa wajumbe wa CC, orodha ya kile ilichoita “makampuni yake yote” inayomiliki.

Makampuni hayo ni Shirika la Uchumi na Kilimo (SUKITA), ambalo lilisajiliwa 15 Machi 1978 kwa ajili ya kufanya biashara mbalimbali.

Kampuni nyingineni ni Uhuru Publications Company Limited (UPL) ambayo ilisajiliwa 9 Desemba 1991. CCM inamiliki asilimia 100 ya hisa za Modern Newspaper Printers (MNP) iliyosajiliwa1995. Ni kampuni tanzu ya UPL.

Nyingine ni Tanzania Trading and Investment Limited (TANTI) iliyosajiliwa 1992 kwa lengo la kufanya biashara ndani na nje ya nchi. Ilifanya kazi tangu 1992 hadi 1998 ilipositisha shughuli zake kutokana na madeni.

Waraka unataja kampuni nyingine ya uwakala wa mafuta kuwa ni Jitegemee Trading Company Limited iliyosajiliwa mwaka 1997.

Kampuni ya Jitegemee Trading Company imeweza kununua hisa zenye thamani ya Sh. 5 milioni kwenye makampuni ya bia na sigara na inapata gawio kila mwaka.

Nyingine ni National Marketing Company Limited. Ilisajiliwa tarehe 6 Mei 1999 kwa madhumuni ya kufanya shughuli za uzalishaji mali na biashara. Kampuni inafanya biashara na kukiingizia chama mapato Tanzania Zanzibar.

Kampuni ya Tanzania Green Company Limited ilisajiliwa mwaka 2003 kwa lengo kuzalisha na kuendesha miradi ya biashara; ilipoanzishwa ilikuwa na mpango wa kuanzisha miradi zaidi ya 10. Hata hivyo, hakuna hata mradi mmoja ulioanzishwa hadi sasa.

Kamati Kuu ilijulishwa kuwa CCM inamiliki kampuni ya People’s Media Communication Company Limited ambayo inamiliki Radio Uhuru. Ilisajiliwa 22 Septemba 2004.

Makampuni mengine ni Kinara Exporters and Importers Company iliyosajiwa mwaka 1998; Jitegemee Tours and Company Limited iliyosajiliwa mwaka 2005; Gaming Management Company Limited iliyosajiliwa mwaka 2003; Amico Holding Company Limited ya mwaka 2001 na Jitegemee Mining and Constructions Company Limited iliyoundwa mwaka 2003 kwa ajili ya ujenzi.

MwanaHALISI liliripoti, miezi minne iliyopita, kuwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), ilikuwa tayari imewasilisha jalada la uchunguzi kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua za mwisho.

Tuhuma zinazomkabili Warioba zipo katika maeneo mawili. Kwanza, ni iwapo fedha zilizotoka BoT zilipitia mkondo sahihi na halali; na pili, kama fedha hizo zilitumiwa kama ilivyotarajiwa.

Bali kwa muda mrefu sasa, Warioba amekuwa akirudia kauli ileile: “…Taarifa kwamba mimi nimetafuna fedha za mradi wa Mwananchi Gold Company Ltd., si za kweli, sijatumia vibaya fedha za kampuni hiyo.”

Amesema, “Fedha zote tulizolipwa na BoT, ambayo ilitoa mkopo kwa mradi huo, zipo kwenye maandishi na ushahidi upo wazi, ila nashangazwa sana, sijui ni kwa sababu za kisiasa mradi huu unapigwa vita?”

Warioba amekuwa akiilaumu serikali kwa kupiga vita MGL kwa kuitoza kodi ya asilimia tatu, wakati ipo kwa mujibu wa sheria ya EPZ, inayotaka kampuni za aina hiyo zisilipe kodi.

Wakati serikali imekuwa ikiibana kampuni hiyo kwa kodi, imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kwa miaka mitano kwa kampuni za kigeni ambazo zipo nchini kwa ajili ya kuwekeza, Warioba amekuwa akisisitiza.

 

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: