Kikwete ana Katiba yake kichwani?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

TUME ya kushughulikia mchakato wa katiba mpya imekwishaapishwa na itaanza kazi zake Mei Mosi mwaka huu.

Akitoa nasaha zake kwa tume baada ya kuiapisha, Rais Jakaya Kikwete alisema maneno yanayoashiria kuwa, ama tayari ana chapisho la katiba kichwani mwake au anatekeleza kazi asiyoipenda.

Maneno hayo yalihusu Muungano na hatima yake. Alisema na kuelekeza kuwa watu hawataulizwa iwapo wanautaka Muungano; bali ni Muungano wa namna gani na jinsi ya kuuboresha.

Watanzania basi, hawana njia, isipokuwa kujifunza kuishi na Muungano hata kama hawautaki; lakini fursa ya kutengeneza katiba mpya haitasaidia kuondoa Muungano hata kama Watanzania hawautaki.

Msimamo huu, hata kama una uzalendo ndani yake, utadhoofisha Muungano. Maneno ya rais yanatokana na sheria ya kuunda tume ya Katiba inayoagiza kuwa Muungano ni moja ya mambo yasiyohojiwa.

Kwa hiyo tume ya katiba itafanya kazi ya kukusanya maoni ya kuuboresha pamoja na maoni ya mfumo gani wa Muungano. Pamoja na kwamba kujenga Muungano ni jambo jema, maneno ya nasaha ya Rais Kikwete yametia doa mchakato huu kabla haujaanza.

Ikumbukwe basi kuwa Rais Kikwete alitoa ahadi huko nyuma kwa baadhi ya makundi yaliyokwenda ikulu kuonana naye, kuhusiana na jambo hili, kuwa sheria inayounda tume hii bado inafanyiwa marekebisho na itaendelea kufanyiwa marekebisho wakati tume inaendelea kufanya kazi.

Alirudia ahadi hii hata wakati anasaini muswada huo ili iwe sheria rasmi. Hakuishia hapo; bali hata katika hotuba yake kwa wana CCM katika sherehe za miaka 35 alirudia ahadi kuwa sheria hiyo inaendelea kuboreshwa ili kutupatia katiba nzuri.

Hii ina maana kuwa, nasaha za Rais kwa tume kuhusu Muungano zaweza kubadilika kwa sababu kadhaa, ikiwamo haja ya kuwapa watu uhuru kuamua hatima nzima ya Muungano.

Fursa ya kuamua masuala haya, hasa Muungano, inatakiwa sana. Kwanza, Wazanzibari tayari wameanza safari ya kueleza hatima ya Muungano pale walipofanya marekebisho ya katiba yao na kutamka kuwa Zanzibar ni nchi.

Aidha, walionyesha msimamo wao pale walipochana hadharani muswada wa marekebisho ya kuunda tume ya katiba mpya.

Mwenye akili angeelewa hapa kuwa kujaribu kulazimisha Muungano kwa tamko la kidola, ni kuuvunja Muungano unaojaribu kuulinda. Muungano unaolindwa na dola hautakaa ujengwe katika mioyo ya Watanzania.

Watanganyika nao wanahoji inakuwaje Wanzanzibar waingie katika tume ya kujadili katiba inayozungumzia masuala ya Tanzania bara wakati wao hawakukaribishwa wakati wa kufanya marekebisho ya katika ya Zanzibar?

Hoja ya kwamba hii ni katiba ya Muungano haijitoshelezi kwa sababu, Watanganyika hawana jukwaa la kwao la kuandaa kile wanachotaka kiingie katika masuala ya Muungano.

Sheria ya kuunda tume ya katiba mpya ilipigiwa kelele na watu wengi, na kwa sehemu kubwa, kelele zilijengwa katika dhana ya kuwa tume hii inaonekana kuwa tume ya rais badala ya kuwa tume huru inayoweza kutuletea katiba mpya.

Hata kabla tume haijaanza kazi, imeanza kupokea amri na maelekezo ya nini kifanyike. Maelekezo ya rais kwa tume yamo kwenye adidu za rejea; hivyo haikuwa busara kwa rais kutoa maelekezo hayo hadharani kwani kitendo hicho kimejenga fikra kuwa tume itapokea amri kutoka kwake kwa kila hatua.

Wakati tunasubiri tume hiyo ianze kazi, zimeanza kusikika tetesi za ajabu zinazoweza kutishia upatikanaji wa katiba mpya inayoakisi mawazo ya Watanzania wote.

Tetesi kuwa chama tawala kimesambaza waraka kwa watendaji wa serikali ili kuhakikisha maslahi fulani ya chama hicho yanalindwa katika utoaji maoni, ni za hatari sana.

Kama tetesi hizi ni za kweli, basi ni hujuma kwa mchakato mzima maana kwanza, hakuna maslahi ya kudumu ya chama chochote katika taifa hili; na pili, hakuna chama chenye hodhi ya kura zitakazopitisha katiba mpya kabla haijatumika.

Yeyote anaweza kuhoji, ikiwa hali ni hii, kwa nini Bwana Kondo unakuwa na wasiwasi?

Wasiwasi wangu unatokana na ukweli kuwa katiba mpya inapaswa iwe ni matokeo ya mchakato mzuri na wazi.

Hata kama mawazo ya Watanzania yamebadilika sana na yanaweza kuyashinda mawazo ya kikiritimba yanayoenezwa na watawala wetu na chama chao, bado siyo sawa kujaribu kuingilia mchakato muhimu kwa fikra za kutaka kulinda maslahi ya kundi fulani.

Sheria inampa rais uhuru wa kuteua mtu yeyote kutoka makundi mbalimbali ilimradi alipendekezwa na kundi lake. Na kwa namna ya kipekee, rais aliamua kuteua watu hao, wengi wao wakiwa wamependekezwa kwa, ama nafasi ya tatu au hata ya nne.

Lakini kitu kimoja ambacho hakionekani wazi katika uteuzi wa rais, ni kigezo cha “mwanya wa kizazi” (generation gap). Mwanya wa kizazi ni dhana ya kuhakikisha tume hiyo inakuwa na wajumbe wa umri na fikra tofauti, yaani vijana, watu wazima na wazee.

Hata katika tasnia moja, wazee, watu wazima na vijana wana muono tofauti; lakini usioathiri tasnia yenyewe kwa njia mbaya.

Ukiiangalia tume nzima imejaa kizazi cha “Mwalimu” na awamu iliyofuata. Pamoja na kwamba hii si kejeli, lakini inaweza kuathiri utendaji wa tume yenyewe hata kama sekretariati inaweza kuwa na uwezo wa kuchukua mawazo kwa haraka na weredi mkubwa.

Katiba inayoundwa itatumiwa na kizazi cha vijana kuliko inavyoweza kuwaathiri walio wazee tayari.

Ulinganifu na umakini uliotumika kuhakikisha tofauti za kiitikadi, dini, bara za visiwani, jinsia na tasnia, ungetumika pia kuangalia “mwanya wa kizazi.” Hili lingesaidia utendaji wa tume hii.

Hata unapoangalia utendaji wa bunge letu kwa sasa, unaweza kuona tofauti kubwa iliyopo katika kizazi kilichopita na kilichopo.

Tutakumbuka kuwa pamoja na wabunge wa CCM kuzomea wabunge wa CHADEMA waliposusa na kutoka nje ya bunge wakati wa kujadili muswada wa sheria ya katiba mpya, ni mawazo yao na hekima ya rais ndivyo vilivyookoa mchakato huu usigubikwe na ghasia.

Ni ajabu kuwa hata baadhi ya wabunge wa CCM waliozomea wakati ule, waligeuka na kupongeza jitihada za CHADEMA pale sheria hiyo iliporudishwa bungeni kufanyia marekebisho makubwa.

Kumbe ndiyo maana wenye hekima wanasema, “Ujana si ujambazi na uzee si uzembe.” Vizazi  vinahitajiana katika suala nyeti kama hili. Kukosekana kwa vijana na fikra za kizazi hiki, kunanifanya nijaribiwe kufikiri kuwa mteuzi (rais), tayari ana katiba yake kichwani.

Kwa kuwa suala la katiba mpya halikuwamo katika ilani ya CCM, ni sahihi kuwaza kuwa Rais Kikwete anafanya kazi hii pasipo utashi binafsi wala utashi wa chama chake.

Hii inaweza kuwa kasoro kubwa katika mchakato mzima. Waswahili husema, waweza kumlazimisha punda kwenda mtoni, lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji yale.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: