Kikwete ana kundi; anaogopa kila kundi


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetimiza miaka 34 na kufanya maadhimisho ya kitaifa mjini Dodoma wiki iliyopita huku idadi ya waliojitokeza katika uwanja wa maadhimisho, ikiwa ndogo sana. Hali hii ilimshutua hata Rais Jakaya Kikwete.

Alipomuuliza mwenyeji wake kuhusu hali hii, William Kusilla, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, alidai ni kwa vile maadhimisho yameangukia Jumamosi.

Aidha, ilionekana wazi wana CCM walikuwa wamezama katika kutafakari nini kifanyike ili kuepusha chama chao kuangamia.

Nayo hotuba ya Rais Kikwete ilikosa msisimuko uliozoeleka katika siku kama hii na hapakuwa na mwitikio wa kusisimua; huku rais akidhihirisha kutokuwa na uhakika na alichokuwa akisema.

Hebu tujadili suala la makundi ndani ya CCM. Hakuna mwenye idadi kamili ya makundi haya wala anayekiri waziwazi kuwa ni mwanachama wa kundi fulani. Mengi hayana vikao rasmi vyenye ajenda, taarifa na mwenyekiti anayefahamika.

Ili kuitendea haki mada hii, niyaangalie kwa kina makundi makubwa ndani ya CCM kwa sasa. Makundi hayo yanajulikana kama kundi la Samwel Sitta, Edward Lowassa na lile la Kikwete.

Makundi haya yana sifa kuu mbili: Kwanza, yanaogopana. Pili, yanaheshimiana. Sifa hizi zinamuweka Kikwete katika nafasi ngumu ya kufanya uamuzi wowote dhidi ya wahusika.

Watendaji ndani ya sekretariati ya CCM na ndani ya ikulu wanatamani Kikwete alishughulikie vikali kundi la Sitta. Kwa upande wake, Kikwete hawezi kulishughulikia kundi hili na bado akabaki na chama chake kikiwa salama.

Hii ni kwa sababu, kundi la Sitta linakubalika sana kwa wananchi walio wengi na hasa vijana na linabeba ajenda ambayo CCM iliipuuza kwa miaka mingi – ajenda ya vita dhidi ya ufisadi.

Kwa kupuuza ajenda hiyo, CCM ilijipuuza yenyewe. Ajenda ya kupinga ufisadi inafahamika kwa walio wengi kuwa si ya CCM kama chama, bali ni ajenda ya upinzani inayoungwa mkono na kundi la akina Sitta.

Kwa bahati mbaya hata baadhi ya mahasimu wa Sitta na wenzake, wamechangia ieleweke hivyo pale walipoanza kuwakejeri wahusika kwa kuwaita majina ya “makamanda wa ufisadi, au mitume kumi na wawili.

CCM isiyopinga ufisadi kwa kauli na vitendo haina tija na hakuna anayehiitaji.

Kwa bahati mbaya, siku za nyuma, Kikwete aliwahi kula njama za kuwashughulikia akina Sitta lakini akashindwa. Aliwaahidi mahasimu wa akina Sitta kuwa atawaruhusu ndani ya vikao ili wawasurubu na hatimaye kuwafukuza kwenye chama.

Pamoja na wingi wao, mahasimu hao walishindwa na mpaka sasa wanamlaumu Kikwete kwa kutoongoza mkakati huo vizuri wakati yeye anawakejeri kwa kusema aliwapa nafasi wakashindwa wenyewe.

Kwa hali hii, ni sahihi kuamini kuwa mfupa uliomshinda Kikwete miaka miwili iliyopita, hawezi kuuvunja sasa wakati meno yake yameanza kuwa butu.

Kundi la pili ni akina Lowassa. Hili ni kundi kubwa na hata Kikwete mwenyewe aliwahi kuwa mwanachama wa kundi hili mpaka miaka miwili iliyopita.

Anawajua vema nguvu yao na udhaifu wao. Nao wanamjua nguvu yake na udhaifu wake. Mmoja wa wanakundi hili aliwahi kuniambia kuwa, Kikwete hawezi kufanya maamuzi magumu mpaka asaidiwe na kundi hili.

Alitoa kejeri kuwa ili Kikwete afanye maamuzi magumu inabidi apigiliwe misumari kwenye kiti na kufungwa kamba ngumu ili tetemeko la kutamka uamuzi mgumu lisimwangushe chini.

Siku za karibuni baadhi ya watu makini katika siasa za taifa wamesema wazi kuwa Kikwete bila Lowassa amepwaya sana, wakimaanisha kuwa Lowassa alimsaidia sana katika kufanya maamuzi magumu na kuyasimamia.

Kwa maana nyingine, Lowassa na kundi lake wana wafuasi wengi ndani ya CCM kama walivyo na maadui wasioweza kupuuzwa. Hali hii inamuweka Kikwete katika kona ngumu ya kulishughulikia kundi hili bila kusababisha tetemeko kubwa ndani ya chama na serikali.

Ni wazi akifanya hivyo atakipasua chama katika mapande makubwa mawili yenye tofauti kubwa za kiitikadi na mtizamo. Kwa mazoea mabaya ya CCM, hakuna atayemshukuru Kikwete kwa kukipasua chama, maana wengi watamzodoa kuwa anawanufaisha wapinzani.

Tishio la kupasua chama endapo ataligusa kundi la Lowassa ni sawa na tishio ambalo Kikwete mwenyewe alilitumia kumtishia mtangulizi wake, Benjamin Mkapa katika kipindi cha mchakato wa kugombea urais mwaka 2005.

Pamoja na ujuzi wa Kikwete wa kutumia karata hiyo, ujuzi huo ukitumika dhidi yake na kundi la Lowassa, utamwacha taabani ndani ya chama na serikali.

Kundi la tatu ni la kwake mwenyewe. Hili ni kundi maslahi linalowaleta pamoja baadhi ya mawaziri, makada wa chama wenye nafasi na wasio nafasi, lakini wanaishi kwa kutegemea fadhila za rais.

Wengine ni wale wanaoishi kwa matumaini ya kuwa anaweza kufanya mabadiliko yoyote ndani ya serikali na chama na akaweza kuwapa ulaji. Siku za karibuni kundi hili limeongezeka kwa kasi sana likivutwa na ‘hisia’ za udini na kudai linamsaidia kwa sababu anasakamwa na watu wanaoongozwa na ajenda ya udini.

Uzuri wa kundi hili ni kuwa halina kiongozi maalum maana ni kundi linalomwangalia zaidi Kikwete na kumzunguka tu sawa na wakuu wengi wa nchi ambao hujikuta wamezungukwa na watu wanaowaambia mambo wanayotaka kuyasikia.

Ubaya wa kundi hili ni kumpotezea fursa Kikwete ya kufanya mabadiliko ya maana ndani ya chama na serikali kwa kumjaza hofu ya maadui wasiokuwepo.

Habari za karibuni kutoka kundi hili baada ya uchaguzi mkuu, zinaeleza kuwa kundi hili limeanza kukata tamaa na Kikwete kwa sababu licha ya kulisikiliza kwa muda mrefu lakini hafuati kwa makini yale wanayomshauri.

Na yeye Kikwete hawezi kulivunja kundi hili kwa sababu hakuliunda. Ni kundi linalojiunda na kumzunguka kwa sababu yeye ni rais.

Mpaka hapa ni wazi kuwa Kikwete hana kundi la kuvunja bali kuzidi kuyaimarisha makundi kwa hatua yoyote atakayoichukua. Akigusa kundi lolote kama tulivyoona, hawezi kufanikiwa kulisambaratisha, bali kundi hilo litakiyumbisha chama na hatimaye kuimarika zaidi.

Akiamua kukaa kimya na kuyaacha kama yalivyo, hiyo pia itazidi kuyaimarisha makundi kama yanavyoendelea kuimarika. Je, afanye nini? Anawezaje kukitenga chama chake kiwe mbali na serikali anayoiongoza?

Anawezaje kuwaelimisha wananchi waelewe kuwa madhambi ya chama si madhambi ya serikali? Au madhambi ya watendaji binafsi si madhambi ya chama wala ya serikali?

Kwa wenye hekima na akili, wanakiri wazi kuwa ndoa kati ya chama na serikali ilikuwa ni ndoa batili na ndicho chanzo cha mambo kwenda mrama ndani ya chama na serikali.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: