Kikwete ana nini?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete alipoanguka Jangwani

RAIS Jakaya Kikwete ameanguka mara tatu na zimetolewa sababu tatu tofauti zinazodaiwa kuchangia hali hiyo, MwanaHALISI limebaini.

Mara ya kwanza alianguka mwaka 2005 wakati wa kufunga kampeni za chama chake - Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mara ya pili ni wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Kanisa la Inland Church mjini Mwanza.

Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete alianguka wakati anazindua kampeni za uchaguzi mkuu kwenye viwanja vya Jangwani.

Aliondoka bila kuwanadi wagombea ubunge wa mkoa wa Dar es Salaam. Hata hivyo, alijitahidi kurejea jukwaani ili kunadi sera za chama chake, lakini alilazimika kukatisha hotuba yake na kuondoka.

Safari zote hizo, zimetolewa sababu tofauti na zinazokanganya.

Saa chache baada ya tukio hilo lililosababisha hali ya simanzi, hofu na vilio vya wapenzi na wanachama wa chama hicho, mwenyekiti wa kampeni za CCM, Abdulrahman Kinana alisema afya ya Rais Kikwete ni salama.

Alisema rais “anasumbuliwa na tatizo dogo la sukari” linalotokana na kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini mwake. Hadi sasa, Kinana hajasema rais ameanza lini kusumbuliwa na ugonjwa huo.

Akiongea kwa upole, Kinana alisema, “Alilazimika kukatisha hotuba yake kutokana na ushauri wa madaktari wake na wametuhakikishia kuwa kila kitu kipo sawa.”

Taarifa ya Kinana juu ya afya ya rais inatofautiana kwa kiwango kikubwa na ile iliyotolewa na madaktari wake, Oktoba mwaka jana mara baada ya rais kuishiwa nguvu na kuanguka mjini Mwanza.

Alipoanguka jukwaani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Oktoba mwaka jana, Rais Kikwete aliwaambia waandishi wa habari tatizo lilikuwa ni “uchovu uliosababishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila ya kupumzika.”

Kikwete alisema kwamba madaktari wake walikuwa wamemshauri apumzike na asiende Mwanza kuhudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Kanisa la African Inland Church (AIC), lakini alikaidi na kilichomkuta ni matokeo ya kutofuata ushauri wa wataalamu.

Katika tukio hilo, lililotokea wakati akihutubia halaiki ya waumini na viongozi wa AIC kwenye uwanja wa CCM Kirumba, madaktari walisema rais amekuwa akikabiliwa na “tatizo moja tu” la kuwa na damu nyingi mwilini.

“Matokeo ya uchunguzi wetu yameonyesha kuwa Mhe. Rais yuko salama. Hana maradhi ya damu au kisukari, wala ukimwi, au ya wingi wa mafuta (cholesterol), ama ya kiwango cha madini, au ya tezi la kibofu, wala ya tezi la shingo, au ya ini, au ya homoni mbalimbali zilizoko mwilini,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Dk. Peter Mfisi.

Alisema, “Afya ya mheshimiwa Rais ipo sawa, isipokuwa tu matatizo madogo yanayohusiana na hali ya kuwa na damu nyingi mwilini mwake.”

Aliongeza, “Pia rais ana maumivu kidogo shingoni ambayo huenda yalitokana na tukio lililomtokezea ujanani kwenye michezo au mafunzo ya kijeshi.”

Dk. Mfisi alisema, “Matokeo ya uchunguzi wetu yameonyesha kuwa Mhe. Rais yuko salama. Hana maradhi ya damu au kisukari, wala ukimwi, au ya wingi wa mafuta (cholesterol), ama ya kiwango cha madini, au ya tezi la kibofu, wala ya tezi la shingo, au ya ini, au ya homoni mbalimbali zilizoko mwilini.”

Alisema matatizo hayo hayasababishi hofu juu ya hali ya afya ya rais.
Dk. Mfisi alitangaza kwamba rais atapunguziwa ratiba ya kazi zake ili tukio kama hilo lisitokee tena.

Chini ya mwaka mmoja, Rais Kikwete anaanguka tena jukwaani na kuzua taswira mbaya kwa wana-CCM waliokusanyika Jangwani, lakini pia kwa umma wa Watanzania.

Taarifa hiyo ilizima kabisa fununu kwamba Rais Kikwete alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari. Vilevile, taarifa hiyo ni tofauti na tukio la kuanguka kwake mara ya kwanza mwaka 2005.

Katika tukio hilo, alianguka wakati akihutubia mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi za CCM katika viwanja vya Jangwani na kuzua hali ya hofu miongoni mwa wanachama wa chama hicho.

Taarifa iliyotolewa baadaye ilisema alianguka kwa sababu ya uchovu wa kampeni. “Mimi mzima wa afya, si mnaniona? Ulikuwa uchovu tu wa kampeni, lakini niko salama,” alisema Kikwete.

Kwa hiyo mwaka 2005 alianguka kwa sababu ya uchovu; mwaka 2009 kwa sababu ya damu nyingi mwilini na mwaka 2010 kwa sababu ya kushuka kiwango cha sukari mwilini, mapigo ya moyo na kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Japokuwa taarifa hizo zinatofautiana ni uthibitisho kwamba, tatizo la Rais Kikwete kuanguka linazidi kukua na kuchukua sura tofauti.

Mwaka 2005 Kikwete hakuweza kurejea jukwani, alichukuliwa moja kwa moja kwenda mapumziko; mwaka jana alipumzishwa kwa muda akarudi tena, lakini safari hii, alipojaribu kurudi kuendelea na hotuba yake alimudu dakika tano tu, akakatisha hotuba na kuondoka.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu wala daktari wa rais, Mfisi, hawakupatikana kuzungumzia hali ya sasa ya rais ingawa amemudu kuendelea na ratiba yake ya kampeni mkoani Mwanza.

Salva alipigiwa simu muda mrefu ikawa haipatikani. Baadaye iliita na kupokewa. Lakini wakati mwandishi anajitambulisha na kuanza kueleza shida yake, Salva alisema apigiwe “baadaye kidogo.”

Muda mfupi baadaye, mwandishi wa MwanaHALISI alimtumia ujumbe wa simu Salva kumweleza umuhimu wa kupatikana taarifa ya daktari kuhusu hali ya afya ya Rais Kikwete.

Gazeti limepokea ujumbe wa simu kutoka kwa wasomaji wake kadhaa wakizungumzia suala la afya ya rais. Mmojawapo ni Adinani Livamba anayehoji:

“Napata mshangao kuona mkuu wa nchi akiendelea kuanguka kila mara. Matukio haya yasifanyiwe mzaha na siyo kusema ‘ilikuwa ni Ramadhani’ kwani wakulima wangapi hufanya kazi juani wakiwa na swaumu zao? Rais achunguzwe kiundani kuhusu afya yake,” anasema Livamba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: