Kikwete anaona wasichoona wengi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version
Kikwete na Mkewe wakibembea

PICHA inayojitokeza mara nyingi zaidi katika mtandao wa kompyuta ukurasa wa ziara za Rais Jakaya Kikwete ni ile inayomwonyesha akiwa amekaa katika kigari cha bembea (skyline) kwa ajili ya utalii katika nchi za milima kama Jamaica.

Kwenye bembea hiyo, Kikwete yuko na mkewe Salma pamoja na Waziri wa Utalii wa Jamaica, Edmund Bartlett (kulia) na mwenyekiti wa Hifadhi ya asili ya milima, Horace Clarke.

Picha hiyo alipigwa na kutumwa nchini kumwonyesha alipokuwa anabembea ili kuona vivutio mbalimbali vya utali katika mkoa wa St. Ann, Jamaica.

Ziara hiyo ni kati ya ziara lukuki alizofanya katika muda wa miaka mitano na kutumia mabilioni ya shilingi; kwanza ilidaiwa kwa ajili ya kujitambulisha, baadaye ilidaiwa mikutano muhimu na kutafuta wawekezaji.

Katika mikutano ya kampeni akiomba kupewa ridhaa ya kuendelea kukaa Ikulu, mgombea huyo wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) anadai kwamba, kama asingekwenda nje watu wangekufa njaa.

Wana CCM ambao kufurahia wakilishwa ghiliba, uongo na kauli zozote bila kupima walilipuka kwa shangwe.

Watanzania wengine wamemshtukia mgombea huyo wa CCM na wanajiuliza, hivi kweli wananchi wangekufa njaa asingebembea kwenye skyline Jamaica?

Ndiyo maana Kikwete anapata shida katika kampeni zake. Anapowaambia watu waone shule, zahanati alizojenga wao wanamwambia ni michango yao iliyojenga zahanati na shule; siyo serikali yake.

Anapowaambia waone barabara alizojenga nchi nzima wao wanamwambia hiyo ni miradi iliyoanza enzi za awamu ya tatu.

Wananchi hawaoni hicho anachoita ni mafanikio ya uongozi wake. Wanaona ghiliba ya mabango yasemayo “Watoto wote ni wetu” wakati kuna wanavyuo 60,000 wananyimwa haki yao ya kupiga kura.

Lakini ni kweli kwamba watoto wote ni wa CCM? Maana wanaposema “watoto wote ni wetu” katika kipindi hiki cha kampeni ina maana ni wa CCM. Vipi Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vinginevyo, navyo vina watoto wao?

Kwa hiyo CCM haioni kuwa “watoto wote ni wa taifa” ila wao?

Anaposema ziara zake za nje zina manufaa kiuchumi wao wanamwambia wanaona matumizi ya mabilioni ya shilingi kwa shughuli ambazo zingefanywa na mabalozi au waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa au wasaidizi wake ambao misafara yao ni midogo.

Watanzania wanaona alivyoshindwa kuwalipa wazee wa Afrika Mashariki huku akitenga Sh. 1.7trilioni (stimulus parkage) za kulipa makampuni yanayofikiriwa kupata hasara wakati wa mdororo wa uchumi duniani.

Wananchi wanaona alivyoshindwa kupunguza umaskini wa wafanyakazi aliotishia kuwatwanga virungu endapo wangeandamana kudai nyongeza, madaraja na maslahi mazuri Mei mwaka huu.

Wasomi wanaona alivyoshindwa kujibu maswali nchini Uingereza. Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwaona waandishi wote nchini uchwara hivyo akawa anakwenda jijini London, Uingereza ambako alihojiwa na kujieleza kwa raha.

Mkapa hakuwahi kushindwa kujibu swali ila siku moja alikumbana na mwandishi ‘aliyepinda’ Tim Sebastian wa kipindi cha Hardtalk katika BBC. We!

Oktoba 4, 2007 Kikwete aliruka kwa pipa hadi London, ambako alihojiwa na gazeti la Financial Times kuhusu raslimali na umaskini wa nchi. Mambo yalikuwa hivi.

FT: Kutokana na namna ulivyojieleza kuna utajiri mwingi Tanzania. Mna maeneo makubwa ya kilimo, utajiri wa madini, lakini kwa nini hainufaiki na utajiri huu? Kitu gani unadhani kinakwamisha?

JK: Kwa kweli hata mimi sijui. Hili ndilo swali ambalo nimekuwa nikijiuliza kila siku, kwamba ni kitu gani ambacho hatujafanya? Nafikiri tumekuwa tukiongoza barani Afrika katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini. Lakini bado tunafanyia kazi (kuvutia uwekezaji katika sekta nyingine). Labda ujumbe bado haujafika sawasawa nyumbani.

Alibandikwa maswali mengine:

FT: Je, unaona uwezekano wa siku moja chama tawala kukabidhi madaraka kwa chama cha upinzani ambacho kitaibuka mshindi?

JK: Siku hiyo inaweza kuja. Lakini sioni uwezekano huo hivi karibuni. Tuna nguvu sana; bado ni maarufu; nafikiri tunafanya mambo kwa uhakika.

Oktoba 31 Watanzania watapigia kura ahadi ya elimu bure na afya bure, siyo viwanja vya ndege na picha ya bembea ya Jamaica.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: