Kikwete anashangaa nini?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ametema nyongo. Amesema hadharani kuwa amesikitishwa na wanachama wa Jumuiya ya Wazazi (WAZAZI) ya chama chake kugawanyika na kufikia hatua ya kupigana ngumi.

Hii ilikuwa kwenye kampeni za uchaguzi wa mwenyekiti wa WAZAZI. Vijana wa kambi mbili walizozana na kuchapana. Kikwete anasema, “Nyinyi wagombea acheni kuleta wahuni katika uchaguzi kama huu. Angalieni mlivotia aibu kwa chama chenu.”

Kikwete anasema jumuia nyingine za chama chake ziko shwari. Hapa ndipo tunataka kumkumbusha kiongozi huyu wa CCM.

Uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UV-CCM) ulijaa vituko vya kila aina. Walijenga kambi. Wakashambuliana kwa maneno na kutishiana. Wakafukuzana. Hizi ni “ngumi” kama za WAZAZI.

Uchaguzi wa Umoja wa Wanawake (UWT) ulikuwa vurumai tupu. Walitupiana mate. Wagombea uenyekiti walioneshana vidole na kushutumiana na kutuhumiana kutoa rushwa. Hizi ni “ngumi” kama za WAZAZI.

Jumuiya za CCM zimekuwa ngazi za kupandia kwenye utukufu wa kisiasa wa chama hicho, kwa wema au kwa hila. Haziwezi tena kusimamia hoja na ajenda muafaka za kitaifa na kuzitetea.

Kama baba kama mwana. Jumuiya za CCM zinatoa sura na taswira za chama hicho.

Ni CCM, wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma, Novemba mwaka juzi ambayo “ilimshangaza” Kikwete kwa kutopea katika rushwa. Naye alinukuliwa akisema:

“…Wakati wajumbe tuko hapa ndani, huko nje watu wanagawa fedha kwa watu ambao hata si wajumbe wa kupiga kura. Naambiwa eti wanataka washawishi wajumbe wawapigie kura watu wao.” Hizi ni ngumi za aina yake. Wapiganaji wamevaa glovu za rushwa.

Sura ya CCM haiishii kwenye uchaguzi ndani yake na jumuiya zake; hata wakati wa uchaguzi mkuu na chaguzi zinazohusisha vyama vingine.

Ghiliba katika uandikishaji wapiga kura; uwongo, ahadi za visivyotekelezeka, ununuzi wa shahada; matumizi ya vyombo vya ulinzi na usalama; na hatimaye ukwapuaji wa ushindi pale ambako CCM haikustahili, ni “ngumi” za kiwango cha juu.

Ni mtindo wa kifisadi nchi nzima ambao umekuwa njia ya maisha kwa baadhi kiasi kwamba asiyetaka kushiriki hapati huduma, hapati heshima. Asiyepokea wala kutoa rushwa anazomewa.

Tunasema Kikwete hana la kushangaa. Anachojaribu kushangaa ndiyo tabia na sasa hulka ya chama chake na utawala wake. Tujifunze nini kutoka kwa chama kikongwe – CCM?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: