Kikwete anasubiri sauti ya Mungu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

WAPO baadhi ya maofisa wanaojaza fomu za safari na tiketi kama sheria inavyotaka katika kuonyesha wamesafiri ili walipwe nauli na posho za safari. Kumbe hawajasafiri.

Wapo maofisa wanaojaza fomu na kuambatanisha risiti kuonyesha wamenunua vifaa fulani wakati ukweli hawajanunua.

Na wapo maofisa wanaojaza fomu na kuambatanisha mikataba feki kuonyesha miradi fulani ya maendeleo imetekelezwa wakati ukweli wamekula fedha na kazi ikawashinda.

Mbinu za kuiba fedha za umma hufanyika kisheria, na ikitokea Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) akaamini vitabu bila ya kukagua miradi husika ili kujua thamani ya fedha anaweza kubariki wizi huo.

Wizi huo hufanyika kwa ushirikiano wa wahasibu, wakaguzi wa ndani na maofisa waidhinishaji wa malipo. Katika ngazi ya kitaifa mwanasheria mkuu na mkuu wa nchi huhusika kikamilifu.

Hii ndiyo sababu sakata la ufisadi kupitia kampuni ya Richmond/Dowans limewatia kabari mwanasheria mkuu wa serikali na mkuu wa nchi. Sakata la ununuzi wa rada lilikaba shingo ya aliyekuwa mwanasheria mkuu, Andrew Chenge.

Mikataba inayotesa wananchi ya IPTL, TICTS, TRL, Songas hata ukwapuaji wa fedha za EPA kupitia Kagoda Agriculture, Deep Green Finance, ina baraka za wakuu wa nchi. Wabunge wanasema Ben Mpaka alijilipa kiinua mgongo kwa kujibinafsishia mgodi wa Kiwira mkoani Mbeya.

Hivi umejiuliza kwa nini mwanasheria mkuu, Rais Jakaya Kikwete na kikundi kidogo cha mawaziri ndio wamebaki kutetetea ufisadi kupitia Dowans? CCM nao wameingia kichwa kichwa Dowans ilipwe.

Huo ndio ushirika wa kifisadi ulioruhusu Richmond; ukafinyanga mkataba kuipa Dowans ulaji. Ushirika huo ukatengeneza majina feki ya wamiliki halafu ukampa mamlaka ya kisheria Rostam Aziz wakati hakuna mahali anapotajwa kuwa na hisa zozote Dowans.

Rostam anaidhinishwa ashtaki, asimamie na kudai fidia duniani kote isipokuwa Costa Rica. Haya ni mamlaka makubwa anayopaswa kupata mmiliki. Katika wamiliki serikali inasema hayumo. Kituko!

Kama serikali ilikuwa inajua Rostam anatembea na mamlaka hayo tangu Novemba 28, 2005, kwa nini iliendelea kudanganya kwa kutaja watu wa kufikirika? Kwa nini haikueleza kuwa pamoja na kuwepo majina hayo Rostam ndiye mwenye mamlaka?

Tahadhari

Ingawa watumishi wa Mungu wanasema Rais Kikwete ni chaguo la Mungu, watumishi haohao wanasema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu.

Kama hivyo ndivyo, katika sakata hili la Dowans, Rais Kikwete atabaki kusikilizwa na Mungu kama chaguo lake au Mungu atasikia sauti ya wengi kwa vile ni yake? Je, Mungu atalinda serikali ya kifisadi au atalinda umma unaopinga ufisadi? Rais Kikwete ajue wakati wa kuachwa mpweke umewadia maana Mungu hawezi kuacha kondoo wake watafunwe na mafisi-adi.

Tujiulize, kwa nini katika mazingira magumu kama haya, Rais bado anakubali kudharauliwa na kukejeliwa kwa sababu ya Dowans?

Kwa nini, hata baada ya wananchi kutahadharisha wazi kwamba wataandamana kupinga malipo kwa Dowans bado rais ameng’ang’ana na Dowans?

Kwa nini, hata baada ya wabunge wa CCM kupinga malipo ya kifisadi kwa Dowans, CCM, mwanasheria mkuu, kikundi kidogo cha mawaziri akiwemo Mtoto wa Mkulima, aliyepoteza ushawishi, wanashupalia Dowans ilipwe? Kwa nini kikundi hiki hakitaki baraza lote la mawaziri lijadili wizi huu?

Mtoto wa Mkulima amezuia wabunge watunga sheria kujadili Dowans bungeni akidai ni suala la kisheria; hivi kazi ya wabunge ni kupiga porojo za kisiasa?

Ushauri

Wakati umefika Rais Kikwete, atoke hadharani atamke wazi, kwamba pamoja na tozo feki waliyopewa Dowans huko nje, serikali yake haitalipa. Kinyume chake, kuna kila dalili atakuwa amechagua kusikia sauti ya Mungu kupitia nguvu ya umma kwa maandamano ya kumpinga yeye na serikali yake.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: