Kikwete ang'ang'ania 'zigo' la Richmond


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 July 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

RAIS Jakaya Kikwete amejitwisha upya "zigo" ambalo tayari lilishafika ufukweni. Jumamosi iliyopita, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima alitangaza uamuzi wa serikali wa "kuwabeba" viongozi wawili waandamizi waliokuwa wanatuhumiwa katika sakata la kampuni ya Richmond Development Company (LLC).

Viongozi hao ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.

Naibu waziri alisema wanaondolewa tuhuma kutokana na "kukosekana kwa ushahidi." Malima alikuwa akiwasilisha taarifa ya bajeti yake, pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge, kuhusu mkataba wenye utata kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond.

Bunge lilimtuhumu Hoseah kushindwa kuwajibika wakati wa uchunguzi uliofanywa na taasisi yake juu ya mkataba kati ya serikali na Richmond.

Serikali inakiri kwamba Hoseah hakutenda kazi zake inavyotakiwa. Kwamba kabla ya kutoa taarifa yake kwa umma, hakujiridhisha kama kweli kampuni ya Richmond ilisajiliwa nchini au hapana.

Hata hivyo, serikali inasema haiwezi kumfikisha Hoseah mahakamani, wala haiwezi kumwajibisha kwa sababu hana kosa la jinai alilolitenda. Alisema Hoseah amepewa onyo kwa kutokuwa makini katika uchambuzi wa taarifa zinazowasilishwa kwake.

Serikali imesema sheria ya TAKUKURU ya wakati ule ilikuwa na mapungufu katika kubaini viashiria vya rushwa kwenye mchakato wa zabuni. TAKUKURU iliwahi kutoa taarifa kuwa Richmond haikuwa katika kashfa yoyote ya rushwa.

Kutokana na hali hiyo, tangu hapo watu wengi walisema hawana tena imani na taasisi hiyo, hasa baada ya Bunge kuanika ukweli juu ya "sakata" la Richmond.

Bunge litakumbuka kauli ya Hoseah baada ya kuamua kuchunguza mkataba wa Richmond, pale alipokaririwa akisema kuwa bunge halina mamlaka ya kufanya kazi ya uchunguzi bali taasisi yake.

Mwingine ambaye serikali imemkingia kifua, ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika. Kama Hoseah, serikali imesema Mwanyika hana jinai aliyoitenda na wala hakuna sababu ya kumwajibisha.

Mwanyika anatuhumiwa kushindwa kuishauri serikali katika mkataba wa Richmond. Wala Mwanyika mwenyewe hakujihangaisha kutafuta taarifa juu ya uhalali wa kampuni ndani na nje ya nchi.

Inawezekana Mwanyika akawa hakuhusika. Inawezekana pia kuwa hakuchukua hata chembe ya pesa ili kufanikisha mkataba. Lakini kule kushindwa kwa ofisi yake kushauri vizuri serikali, hadi serikali ikalazimika kuingia mkenge kwa kuingia mkataba wa ajabu kama ule, kulitosha kumweka pembeni.

Tuhuma zilikuwa kwamba akiwa mwanasheria mkuu wa serikali Mwanyika alishindwa kuwajibika. Aliingiza serikali katika hasara ya mabilioni ya shilingi na amechangia kuzorotesha uchumi wa nchi kwa kuipa kazi ya kufua umeme kampuni ambayo haikuwa na uwezo.

Kutokana na hali hiyo, wachunguzi wa mambo ya utawala wanasema hatua ya rais Kikwete kukubali Hoseah na Mwanyika kuendelea na nyadhifa zao, inazima matarajio ya wengi; na kwa undani yaweza kuonekana inatia doa utawala bora.

Ilitarajiwa kwamba hata kama Hoseah na Mwanyika hawakupatikana na jinai, lakini rais angewawajibisha kutokana na uzembe uliodhihiri. Ni wazi kwamba hatua ya Rais Kikwete ya kuwabakisha wahusika katika nafasi zao, itazidi kuibua minong'ono na malumbano mengine mengi huko tuendako.

Kwanza, wako watakaodai kuwa rais ameshindwa kuwachukulia hatua Mwanyika na Hoseah kwa sababu wao hawakuwa waamuzi katika hili. Walikuwa wanafanya kazi ya kubariki kile kilichoamuliwa kutoka juu.

Tayari mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Lipumba, ametupa kombora, kwamba mhusika mkuu katika sakata hili ni Rais Kikwete mwenyewe. Ameibuka na kauli kwamba katika hili la Richmond, Lowassa amesulubiwa kwa "makosa ambayo hakutenda."

Pili, wapo watakaodai kuwa labda Rais Kikwete alikuwa amepanga kumfukuza kazi Lowassa, ndiyo maana haraka alikubali kujiuzulu kwake.

Hata Lowassa mwenyewe amewahi kunukuliwa akilalamika, "…Nimeonewa sana, nimefedheheshwa sana katika hili. Mimi naona tatizo ni uwaziri mkuu…"

Hapa haraka wananchi wanaweza kudhani kuwa labda hakuhitajika tena katika nafasi hiyo. Ndiyo maana baada ya yeye kuondoka, serikali imeamua kuendelea kuwakumbatia kina Hoseah na Mwanyika.

Na kwa jinsi muda unavyozidi kutokomea kuelekea uchaguzi mkuu, sioni dalili za Rais Kikwete kuweza kukabiliana na madai haya, hasa katika wakati huu ambapo umaarufu wake kwa wananchi umeshuka ikilinganishwa na wakati anaingia ikulu.

Wananchi wengi wanamuona rais kama taasisi isiyokuwa na meno; hawezi kutekeleza kile alichoahidi. Hoja hii inapata nguvu hasa katika hili, kwamba hata baada ya bunge kumaliza kazi, rais ameshindwa kuwaondoa wahusika.

Je, rais anaelekea wapi? Sitaki kuwa mtabiri, lakini kwa inavyoonekana, serikali itakuwa imejiingiza katika zogo jingine na bunge na wananchi kwa jumla.

Inawezekana waliomshauri Rais Kikwete kumuacha Hoseah na Mwanyika katika nafasi zao hawakuyaona haya. Tusubiri tuone!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: