Kikwete aogopa ‘vyama vya msimu’


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Dk. Slaa: Tunafanya kazi ya kisiasa
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete, ambaye miezi mitatu iliyopita alisema vyama vya upinzani visichaguliwe kwa kuwa ni “vyama vya msimu,” sasa analalamika kuwa CHADEMA inataka kuangusha serikali yake.

Kauli ya Kikwete kabla ya uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka jana, ililenga kudhoofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilichokuwa kimekaba koo Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchi nzima.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, juzi Jumatatu, Rais Kikwete alionyesha kutishwa na wimbi la CHADEMA, hasa maandamano na mikutano yake mikubwa kuliko hata ile ya wakati wa kampeni.

Kikwete alisema, bila kumung’unya maneno, kuwa vitendo vya sasa vya CHADEMA vinachochea “…ghasia ati kwa nia ya kuiondoa serikali madarakani.”

Alisema hiyo “…ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Iweje leo, miezi mitatu (baada ya uchaguzi), kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yaleyale waliyoyasema kwenye kampeni. Siyo sawa hata kidogo.”

“Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,” alieleza.

Kauli ya rais ya kuhofia maandamano, inakuja siku nne tu baada ya CHADEMA kuanza ziara ya kushukuru wananchi kwa kuwapa kura na kueleza matatizo yanayokabili utawala na nchi kwa jumla.

Aidha, kauli ya rais inakuja wakati nchi za Kaskazini mwa Afrika zikikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi kwa njia ya maandamano na migomo.

Akijibu madai ya Rais Kikwete, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amesema, “Tunakwenda mikoani kufanya kazi za chama cha siasa, si kuangusha serikali.”

Dk. Slaa amesema, “Huku tuliko hata mende hajafa. Hatufanyi vurugu wala hatuhamasishi wananchi kupindua serikali. Tunachokifanya ni kueleza wananchi juu ya rushwa na ufisadi serikalini. Tunawaeleza jinsi uteuzi wa mawaziri na wakuu wa mikoa ulivyojaa upendeleo kwa kuweka watu hawa wasiostahili kama vile Steven Wassira na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dk. Johannes Balele.”

Anasema, “Tunakwenda kuwaeleza wananchi juu ya fedha zao zinavyotafunwa na jinsi viongozi wanavyotumia madaraka ya umma kujinufaisha binafsi.”

Anatoa mfano wa Dk. Balele ambaye anadai aliruhusu “dawa ya ukimwi iliyopigwa marufuku nchini Afrika Kusini kufanyiwa majaribio nchini, jambo ambalo limesababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha.”

“Siku zote tumekuwa tunamuuliza rais, Kagoda ni nani? Deep Green ni nani? Meremeta ni nani. Hakuna majibu. Tumemuuliza waziri mkuu bungeni, nani Meremeta, amesema ‘hata mkinikata shingo, sisemi,” ameeleza Dk. Slaa kwa simu kutoka Shinyanga.

“Sasa (rais) anataka sisi tufanye nini kama si kwenda kwa wenye mali zao na kuwaambia serikali imeiba fedha zenu? Kwamba Sh. 155 bilioni zimeibwa kupitia Meremeta, Sh. 50 bilioni kupitia Kagoda na mabilioni mengine mengi kupitia makampuni mengine ikiwamo Meremeta,” Dk. Slaa amefafanua.

Katika hotuba yake, rais alisema, katika nchi ya kidemokrasia na kwa wanademokrasia wa kweli, uchaguzi mmoja unapomalizika, “mnajiandaa kwa uchaguzi mwingine” na kwamba hilo linafanyika kupitia bunge na halmashauri za wilaya kupitia wabunge na madiwani wenu.

​Alisema, “Kuacha kufanya hivyo na badala yake kuamua kuzunguka nchi nzima na kuchochea ghasia kwa lengo la kuwaondoa walioshinda ili muingie nyie ni kinyume kabisa na misingi ya demokrasia.”

Rais Kikwete amesema “CHADEMA…wanataka kuipeleka nchi yetu pabaya kwa kukidhi uchu wao wa madaraka. Kwao sasa demokrasia haina maana, inaweza kusubiri. Wanataka kutumia mabavu.”

Amewaomba wananchi kukataa “…mambo yao. Tusiwafuate. Waambieni mchezo wao ni hatari na ni mauti yetu. Sisi katika serikali tutajitahidi kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa nchi yetu, watu wake na mali zao.”

​Akizungumzia hali ya uchumi, Rais Kikwete alikubali kuwa kuna hali ngumu ya maisha na kwamba serikali yake inajitahidi kukabiliana nayo. Alisema kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, bali “kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu.”

Akijaribu kuhalisha usugu wa matatizo, Kikwete alisema hata Mwalimu Nyerere aliongoza kwa miaka 23 lakini hakumaliza matatizo, Ali Hassan mwingi miaka 10 na Benjamini miaka 10 lakini hayakuisha na kwamba hata yeye hatayamaliza.

Hadi juzi Jumatatu, CHADEMA walikuwa wametembelea mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga. Watahitimisha ziara yao ya sasa mkoani Kagera.

Wakiwa mkoani Mara, viongozi wa CHADEMA walizuru nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Butiama na kupata fursa ya kuzungumza na Mama wa Taifa, Maria Nyerere.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: