Kikwete asaidie iwepo sera dhidi ya ufisadi


John Kibasso's picture

Na John Kibasso - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version

RAIS Kikwete Jumatano 09 Septemba, 2009, aliamsha hisia za wananchi kwa kutoa staili mpya ya kuwaruhusu kumweka kiti moto 'live' kwenye luninga na vituo vya redio hapa nchini.

Rais alikuwa akijibu maswali na maoni ya wananchi kwenye maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Haijapata kutokea barani Afrika kwa rais wa nchi kujitokeza ‘live’ na kukubali asulubiwe na wananchi kwa kumuuliza maswali ya papo kwa hapo. Viongozi wengi wanaogopa mvundo wa harufu ya utawala wao kuanikwa wazi.

Katika gazeti la Mwanahalisi Jumatano, Agosti 19 – 25, 2009, nilijaribu kutetea makala ya Salva Rweyemamu, aliyempinga mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alisema Rais Kikwete ameshindwa kazi.

Kwenye makala hayo niligusia nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, ambako Rais amefanikiwa kwa kipindi ambacho amekuwepo madarakani.

Utendaji kazi wake niliufananisha na staili ya marais wa zamani wa Marekani, John F. Kenedy na Bill Clinton. Ulinganisho wangu ulijikita kwenye uhuru, uwazi, utawala wa sheria na haki za wananchi.

Makala hii inalenga kutoa majibu kwa wasomaji, hususani wanazuoni, ambao wengi walijitokeza na kubeza mafanikio niliyoyaorodhesha, huku wakidai hayakuwa na takwimu za kutia nguvu hoja zangu.

Maeneo waliyoyagusa kwa kushutumu uongozi wa Kikwete, ni kushindwa kudhibiti mafisadi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumfunga mdomo spika na wabunge wenye msimamo mkali dhidi ya ufisadi, mikopo kwa wanafunzi vyuoni, migomo ya wafanyakazi, na shule za kata.

Rais yeyote ambaye ni fisadi, mzandiki, mbinafsi, mroho na mwenye kila aina ya uchafu ndani ya utawala wake, kamwe hawezi kujitosa ‘live’ ili wananchi wa kawaida wamuulize maswali yanayohusu utekelezaji wa shughuli zake.

Kwa weledi wa siasa na wachambuzi wa mambo, kitendo cha Rais wa nchi kukubali mwenyewe kuulizwa maswali kwa staili aliyotumia Rais Kikwete ni ujasiri na ni ishara ya uadilifu, upendo na imani aliyonayo kwa wananchi.

Ameonyesha umakini, utulivu na uelewa wa mambo yanavyokwenda nchini. Rais alitumia busara na kuvuta hisia za wengi ambao walidhani kuwa ukimya na upole wake vimesababisha raia na taasisi kufikia malumbano yasiyokuwa na tija kwa taifa.

Majibu na ufafanuzi aliotoa inatosha kutoa mwanga kwa wale waliokuwa wanabeza mfumo wa utekelezaji wa majukumu yake.

Katika anga za siasa, Rais alithubutu kuwatoa wasiwasi wale waliodhani kwamba chama chake kina hisa na mafisadi. Alitoa kauli hadharani kuwa hayuko tayari kuwazuia wabunge kuikosoa serikali na kuwahimiza waendelee kupiga vita ufisadi ndani ya Bunge.

Naamini uhuru aliotoa kwa wabunge ni ishara ya kuwaonya wale ambao bado wanatamani ufisadi. Tamko la rais mara zote ni agizo kwa watendaji serikalini.

Nilifurahishwa na maelezo ya Rais kuhusu uchumi na pato la mtu binafsi. Rais alisema bado walikuwa wakiandaa miundombinu ya kuwanyanyua wananchi katika pato binafsi. Programu ya kilimo kwanza ndiyo suluhisho kwa kuongeza pato la wananchi.

Weledi wa historia wanafahamu kuwa kiongozi hodari na shupavu ni yule anayeingia kwenye kumbukumbu kwa aina ya kitu au mfumo alioubuni, ambao umeleta tija kwa jamii. Kwa mfano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alibuni utaratibu wa kuunganisha Watanzania kwa kutumia Kiswahili. Hili peke yake ni ubunifu ambao hautasahaulika.

Hata Richard Aldolf Hitler wa Ujerumani, historia inaonyesha kwamba pamoja na udhalimu wake, bado alibuni magari aina ya Volkswagen, ambayo yalikuwa ni rahisi na bei nafuu.

Historia haitamwacha Rais Kikwete kwa kubuni mbinu ya kujenga shule za sekondari za kata kwa muda mfupi na kujipambanua "live" kwa kuulizwa maswali ya papo kwa hapo. Unajua wengine wanaweza kukuuliza hata swali la matusi au wasomi wakauliza swali la taaluma kwa makusudi ya kukudhalilisha.

Ningependa kumshauri Rais Kikwete kuwa angekubali kuitisha kikao cha pamoja na vyama vyote vyenye usajili, chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ili watoe mwongozo au sera ya kitaifa, kupiga vita ufisadi bila kujali itikadi ya chama.

Ushauri wangu wa pili, ambao nauona ndicho kikwazo kwa viongozi wa kitaifa, hususani wa chama tawala kuogopa kushughulikia mafisadi, ni msigano wa katiba ya chama na ile ya nchi. Kwa muono wangu viongozi wote wakubali kuwapa uhuru viongozi kama madiwani, wabunge, spika na Rais watekeleze majukumu yao bila kuingiliwa na masharti ya vyama vyao.

Kipengele cha "kuvuliwa uanachama" kisitumike pindi kiongozi akiwa bado anatumikia taifa.

Viongozi wa chama kitaifa wawe na kinga ya kutowajibishwa na vyama vyao wakati wakitekeleza majukumu. Kinga itasaidia kuacha woga.

Katiba ya nchi, ibara ya 100, inampa kinga mbunge kutoshitakiwa wakati akichangia muswada bungeni. Kinga kama hii pia ingefaa kutumika kwa viongozi wa vyama kitaifa.

Kuhusu ubinafsishaji, ni muhimu Rais akashauriwa ili autolee mwongozo. Ubinafsishaji uliweka mashirika ya umma mikononi mwa wawekezaji, ili kuongeza uzalishaji na tija. Serikali ingefanya tathmini ya viwanda na mashirika yaliyobinafsishwa ili kutambua ufanisi na upungufu uliopo.

Kuna mashirika yaliyofanikiwa kujiendesha kwa ufanisi baada ya kubinafsishwa. Mfumo uliotumika kubinafsisha benki National Microfinance (NMB) na CRDB pia ungetumika katika kubinafsisha mashirika makubwa kama Shirika la Umeme (TANESCO), Shirika la Bima (NIC), Shirika la Ndege (ATC) na Shirika la Reli (TRC).

Mfumo wa kuuza hisa kwa wananchi ndio mzuri kwani umedhihirika kuwa unatoa changamoto kwao kumiliki uchumi wa nchi. Serikali ingekubali kubinafsisha TANESCO, NIC, ATC na TRC kwa mtindo huo.

Kwa TRC serikali ingetengua mkataba. Wafanyakazi wapewe asilimia 10 ya hisa kama sehemu ya "mkono wa heri." Hakuna atakayethubutu kuhujumu shirika.

Ushauri wangu mwingine ni kwa viongozi wa vyama vyote, kujenga tabia ya kuyapa kipaumbele majukumu ya kitaifa bila kujali itikadi. Kuendelea kubeza hata yale mazuri yanayofanywa na serikali siyo ustaarabu.

Makala hii imeandaliwa na John M. Kibasso, mpenzi wa gazeti hili, aliyewahi kuwa mbunge wa CCM jimbo la Temeke, Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu namba 0713 – 399004
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: