Kikwete atavua magamba mangapi?


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), sasa kinatafuta mlango wa kutokea baada ya kushindwa kutekeleza kwa vitendo mradi wake wa kujivua gamba.

Ukweli wa kama kimeshindwa kujivua gamba uko wazi, kinachokosekana sasa ni ujasiri wa kukiri hadharani kuwa kimeshindwa.

Tangu kushindwa kutekeleza mradi huo, kumekuwa na kauli tofauti zinazotafuta kupunguza makali ya aibu ya kushindwa kutoka kwa viongozi wakuu wa chama hicho.

Kwa mfano, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita, Wilson Mukama, katibu mkuu wa chama hicho, amenukuliwa akisema, “Sharti chama kijisafishe ili kurejesha hadhi ya chama mbele ya umma.”

Hata hivyo, Mukama ameshindwa kujibu hatua gani zitachuliwa iwapo wahusika wataendelea kugoma kuondoka. Badala yake amesema, CCM hakiongozwi na maoni ya wananchi bali wanachama.

Lakini baadaye amesikika akisema, “Iwapo watuhumiwa wa ufisadi hawatakubali kuondoka kwa hiari yao” ndani ya chama chake, utaratibu madhubuti wa “kuwavua kwa nguvu magamba kabla ya mwezi Machi mwaka kesho” umewekwa.

Amesema zoezi la kuvua magamba liliahirishwa ili kupisha mchakato wa kuunda tume ya udhibiti wa nidhamu na maadili katika ngazi ya taifa; pamoja na uundwaji wa kamati za nidhamu na maadili kwenye ngazi za mikoa, wilaya, kata na matawi.

Amesema watuhumiwa watapewa nafasi ya kujitetea dhidi ya ushahidi utakaotolewa dhidi yao ili kudumisha “haki ya asili” (Natural justice). Haifahamiki mpaka sasa ni kwa nini CCM iamue kutumia njia ya kimahakama ndani ya chama wakati mahakama zipo wazi kuhukumu wanaothibitika kuwa ni mafisadi.

Ingawa Mukama hataji majina ya wanaotakiwa “kuvuliwa magamba” kwa nguvu, lakini wanaofahamika kwa mujibu wa John Chiligati, naibu katibu mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara na Nape Nnauye, ni Edward Lowassa na Andrew Chenge.

Hata hivyo, jopo lililokuwa linajadiliana na hatua ya CCM kuonekana imeshindwa kujivua gamba, walikubaliana kuwa uchaguzi wa msema wa “kujivua gamba” inapotosha maana nzima ya kuondokana na ufisadi ndani ya chama hicho. Walisema wakati hatua ya kujivua gamba kwa kiumbe nyoka ni ya asili, isiyohitaji nguvu kutoka nje, hatua ya CCM kuondokana na ufisadi inahitaji msukumo wa dhati kutoka ndani na nje ya CCM.

Mmoja alihoji, kama ushahidi upo wazi kwa nini CCM ichukue nafasi ya mahakama?

Sasa swali ambalo wengi wanajiuliza ni hili: Iwapo CCM kimeshindwa kutumia mkutano wa NEC kumalizana na mafisadi, badala yake imeamua suala hilo lirejeshwe kwenye vikao vya nidhamu na maadili; upanuliwe wigo wa watuhumiwa na kuongezwe tuhuma mpya kwa baadhi ya watuhumiwa, nani aweza kuamini sasa kwamba kweli gamba linalotajwa linaweza kuvuliwa?

Hii ni kwa sababu, kuruhusu suala hilo kupelekwa kwenye vikao vya nidhamu na kufungua wigo wa watuhumiwa, kutalifanya jambo hili kuwa gumu zaidi kutekelezeka.

Mathalani, ndani ya vikao vya maadili na nidhamu Lowassa aweza kuja na ushahidi mwanana wa kuthibitisha jinsi Rais Jakaya Kikwete alivyoshiriki katika kuhakikisha Richmond inapewa mkataba.

Anaweza kueleza jinsi Dowans walivyorithi mkataba wa Richmond na namna Rostam Aziz alivyoruhusiwa na mkuu wa nchi kuingilia mchakato wa zabuni kwa maslahi binafsi.

Je, Mukama yuko tayari kuruhusu hilo kutokea? Kama ndiyo, atafanya nini iwapo Kikwete atatajwa na kuthibitika kuwa ni mmoja wa watuhumiwa wakubwa kwenye ufisadi wa Richmond?

Chama chake kitakuwa wapi? Nani ataweza kukiamini ikiwa mwenyekiti ni miongoni mwa “magamba?” Lililo wazi ni hili: Iwapo Mukama atatenda kama anavyosema, utakuwa ni muujiza mkubwa ikiwa Rais Kikwete hatatajwa kama mhusika mkuu wa kashfa nyingi kubwa ambazo zimekuwa zinakisambaratisha chama hicho mbele ya wananchi.

Kabla ya Mukama kuja na kiini macho cha sasa, wenzake ndani ya chama hicho – Nape Nnauye, katibu mwenezi na John Chiligati, naibu katibu mkuu, Tanzania Bara, walitangaza hadharani mwisho wa wanaowaita mafisadi ndani ya chama chao ni siku 90 baada ya mkutano wa NEC wa Aprili kumalizika.

Hatimaye siku 90 zikaisha. Mukama akaibuka na kukana chama chake kutoa siku 90 kwa mafisadi. Akasema ni hadi NEC ijayo ambayo hufanyika kila baada ya miezi minne. Hatimaye miezi minne ikafika bila gamba kuvuka.

Azimio la kuvuana magamba kwa nguvu kabla ya Machi 2012, imekuja baada ya siku 90 zilitolewa na chama hicho kwa watuhumiwa hao kuondoka wenyewe kwenye uongozi wa juu wa chama kuisha bila wahusika kutekeleza agizo hilo .

Aidha, kauli ya Mukama imekuja miezi saba baada ya Nape kuhubiri kwa sauti kali, “Kinachosubiriwa sasa ni suala la utekelezaji tu; NEC imetoa siku 90 kwa mafisadi kuondoka” katika chama.

Nape alijiapiza kuwa barua za kujulisha mafisadi kuondoka katika chama tayari zimeandaliwa na zimekabidhiwa.

Siku 90 zilipokwisha, Mukama akaja na hadithi nyingine. Akasema, “…hakuna mahali popote katika maazimio ya NEC panapotaja siku 90.” Anapoyasema haya Mukama anasahau kuwa Nape Nnauye na Chiligati ndiyo waliohubiri siku 90.

Lakini yeye alisema, “Kama ni muda basi ni pale mwenyekiti wetu aliposema NEC ijayo. NEC hukutana kila baada ya miezi minne na kwa hiyo kama ni siku, basi ni 120 na siyo 90.”

Hadthi ya siku 120 nayo ikaisha. Miezi saba ikaingia bila wanaotakiwa kuondoka kuitikia wito wa kutoka.

Kwa hakika vituko vya ni vingi. Ni Mukama huyuhuyu anayesema ataondosha mafisadi kwa nguvu kwenye chama chake, anayedaiwa kuogopa kusaini barua zilizotaka kwenda kwa watuhumiwa akidai wakati NEC inapitisha jambo hilo, yeye alikuwa bado hajateuliwa.

Baada ya Mukama kuogopa kusaini barua hiyo, zikapelekwa kwa Pius Msekwa ambaye naye alishindwa kuweka saini. Zihahamishiwa kwa rais Kikwete, mbapo kama ilivyokuwa kwa wasaidizi wake hao wawili, naye aliigoma kuisaini.

Wapo wanaodai hadi leo barua hizo zinaendelea kuozea kwenye makabati ya ikulu na iwapo watasahau kuziondoa, kuna uwezekano mkubwa zikaonekana na rais ajaye na hivyo umma kufahamu kilichomo kwenye barua hizo.

Wakati wa mnyukano huo wa barua ukiendelea, watuhumiwa wakaeleza hawawezi kujiuzulu hadi watakapokabidhiwa barua zao. Bila shaka walifahamu udhaifu wa Kikwete katika kusimamia kile ambacho ameshiriki kukipitisha.

Hatua ya CCM kujivua gamba ilitangazwa na mwenyekiti wa CCM katika sherehe za maadhimisho ya 34 tangu kuzaliwa kwa CCM. Hii ilisababishwa na kupungua kwa kura za CCM katika uchaguzi uliopita ukilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2005.

Kura za Rais Kikwete licha ya kutiliwa mashaka makubwa na waangalizi wa ndani na nje, zilipungua kwa asilimia 20 huku idadi ya wapiga kura ikiwa chini ya asilimia 50. Wadadisi wa mambo ya siasa hapa nchini wanadai Rais Kikwete alikurupuka kutamka hatua hii ya kujivua gamba nah ii inaweza kuwa ni sehemu ya kiwewe cha kipigo alichokipata katika uchaguzi huo.

Dalili za kushindwa kwa CCM kujivua gamba hapo zikazidi kunaonekana wazi. Hatimaye miezi minne ikakatika. Miezi saba baadaye, mkutano wa NEC ukafanyika, lakini ni mtuhumiwa mmoja tu aliyetii agizo la NEC na kujiondoa mwenyewe katika uongozi wa chama.

Watuhumiwa wengine wawili waligoma na dalili za woga wa kuwagusa ziko wazi kwa hatua ya hivi karibuni inayoonekana kusahau matamshi ya viongozi waandamizi yaliyotolewa Aprili mwaka huu.

Je, katika mazingira haya, nani atamwamini Mukama kuwa anaweza kufukuza mafisadi? Uko wapi ujasiri wa kutekeleza hayo, wakati hata barua tu, ameshindwa kuwakabidhi. Tusubiri tuone.

Lakini CCM ingeweza kuandika historia kama ingewafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi kuanzia wizi uliofanywa na makampuni ya Kagoda, Deep Green Finance Ltd, Meremeta, Richmond na mwingine, badala ya kuhubiri kuvuana magamba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: