Kikwete atishia wenzake


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 January 2009

Printer-friendly version
Wapanga kuhama chama
Aliyotabiri Mkapa yaja
Rais Jakaya Kikwete

BAADHI ya viongozi na wanachama mashuhuri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana mpango wa kuanzisha chama cha siasa ili kuweka upinzani mkali kwa Rais Jakaya Kikwete ifikapo 2010, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa mikakati ya viongozi na wanachama hao, ambayo gazeti hili limepata, chama hicho kinapaswa kuwa kimeanzishwa katika miezi sita ijayo.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi, rais aliyeko madarakani anaruhusiwa kugombea kwa mara ya pili iwapo anapitishwa na chama chake. CCM ina utamaduni wa kumpitisha rais wake kwa kipindi cha pili.

Sababu kuu ambayo imeelezwa kuwa chanzo cha kuundwa kwa chama cha “waasi” ndani ya CCM ni kile kilichoitwa “kudhalilishwa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu” wa chama hicho.

Njia tatu zimetajwa kutumika katika kuanzisha chama hicho. Kwanza, kutafuta uwezekano wa kuanzisha chama moja kwa moja. Pili,  kujiunga au kununua moja ya vyama vya upinzani vilivyopo ambavyo vimelegalega lakini vina mizizi hasa Tanzania Bara.

Njia ya tatu ni kwamba iwapo njia mbili za kwanza zitashindikana, basi wapenyeze wafuasi wao katika kura za maoni za CCM na kuwagharimia ili waweze kushinda.

Mazingira yanayojitokeza katika hili ni kama yale aliyotabiri rais mstaafu Benjamin Mkapa, mwishoni mwa wiki, kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 “utakuwa mgumu na unaweza kuliingiza taifa katika machafuko.”

Mkapa ametaja siasa za majungu, chuki, fitina, ukabila na udini kuwa mambo yaliyozuka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na ambayo yatazua ugumu iwapo viongozi hawatajiepusha navyo.

Miaka miwili na nusu ya utawala wa Rais Kikwete imekuwa ya kimya lakini katika kipindi kuelekea mwaka wa tatu, Kikwete amecharuka na kukamata watuhumiwa wa ufisadi wakiwemo waliokuwa mawaziri katika serikali ya Mkapa.

Taarifa zinasema baadhi ya viongozi wanaotaka kuanzisha chama ni miongoni mwa watuhumiwa wa ufisadi na ambao wanadai kudhalilishwa na utawala wa Kikwete.

Kauli ya Mkapa inaonyesha ama anaelewa kinachoendelea kuhusu mkakati wa chama kipya au analilia waliokuwa wasaidizi wake ambao wamekumbwa na zahma sasa.

Miongoni mwa madai ambayo watuhumiwa wamekuwa wakitoa ni “kuonewa, kufanyiwa fitina na chuki.”

MwanaHALISI imepewa orodha ya wanachama na viongozi ambao wanatajwa katika mkakati wa kuanzisha chama kipya kwa masharti kwamba wasitajwe kwa sasa.

Mmoja wao alimwambia mwandishi wa habari hizi, “Nami nimesikia mpango huo, lakini mimi simo kwani mabao yangu siyo magumu.”

Alisema wale ambao “mambo yao ni magumu kama unavyosema, ndio wanaoweza kujenga mawazo ya kukimbia… Mimi niko kijijini huku nafanya kazi za chama.”

Mwingine kwenye orodha hiyo ambaye alihojiwa alisema, “Ninavyojua mimi hakuna wabunge wa CCM wanaoweza kuanzisha chama. Hii si kazi ndogo. Kwanza wakianzisha chama sasa hivi watapoteza ubunge na mafao yao.”

Alipoulizwa juu ya uwezekano wa kujiunga au kununua chama cha upinzani kilichopo alisema, “labda hilo. Hilo linawezekana.”

Kiongozi wa chama cha NCCR-Mageuzi ambacho kimetajwa kuwa kinaweza kuhamiwa au kununuliwa, amekana kuwa na taarifa zozote juu ya mpango huo.

Sam Ruhuza, Katibu Mkuu wa chama hicho alimwambia mwandishi wa habari hizi “Mimi sijasikia lolote juu ya hilo.”

Alipoulizwa huenda hajui kwa akuwa amekuwa kiongozi katika uchaguzi wa mwezi uliopita, alisema “Ni kweli mimi ni mpya kwenye nafasi hii lakini nimekuwa kwenye chama kwa muda mrefu.”

“Kama mpango huo upo ningeujua, kwa kuwa ni mimi niliyepo ofisini na mwenyekiti wangu yuko nchini Uholanzi kwa masomo,” alisema Ruhuza.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, wanaotaka kuanzisha chama wamelenga kutumia magazeti yaliyopo au kuanzisha mapya ili kuendesha kampeni kubwa ya ushawishi.

Mmoja wa wamiliki wa magazeti aliyemo katika mpango huo alipoulizwa juu ya mpango wa gazeti lake kutumika, hakijibu bali alikata simu.

Kumekuwa na taarifa nyingi za kuanzishwa kwa magazeti mengi kuelekea uchaguzi wa 2010 na kwamba ofisi ya Msajili wa Magazeti (MAELEZO) imejaa maombi ambayo hayajashughulikiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Maelezo, Raphael Hokororo amethibitisha kuwepo maombi mengi ya kuanzisha magazeti.

Hata hivyo amesema maombi yote yanashughulikiwa. Hakuna agizo lolote la kusita kusajili magazeti.

“Maombi yapo tunayashughulikia. Hakuna agizo la kusitisha usajili. Kwa hiyo hata mwenye magazeti mia akileta maombi mapya na ametimiza vigezo, tutamsajili,” amesema Hokororo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: