Kikwete awaangukia maaskofu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 April 2010

Printer-friendly version
Awatuma Malecela, Msekwa kuteta
Wenyewe wazidi kutoa maelekezo
Rais Jakaya Kikwete

MISIMAMO mikali ya makanisa nchini imetikisa serikali na kufanya Rais Jakaya Kikwete kuomba huruma, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinasema misimamo ya madhehebu ya kidini ina uwezekano wa kupenya hadi kwa wananchi na kuhatarisha uhai wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Katika hali isiyo ya kawaida, taarifa hizo zinaeleza, Rais Kikwete ametuma ujumbe mzito wa viongozi waandamizi wa chama chake kwenda kuangukia viongozi wa kidini.

Kikao cha Kamati Kuu (CC) kilifanyika tarehe 28 mwezi uliopita, ikulu Dar es Salaam.

Kwa muda wa miaka minne sasa, madhehebu ya kikristo yamekuwa yakituhumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya vitendo vya ufisadi nchini.

Karibu madhehebu makuu ya kikristo, yakiwemo Katoliki, Lutherani, Anglikana na Pentekoste, yamekuwa yakitoa matamko mazito juu ya mwenendo wa serikali.

Ilifikia mahali Kanisa Katoliki likatoa, mwaka jana, Mwongozo wa kuelekeza waumini wake na wananchi kwa ujumla jinsi ya kupata viongozi bora.

Mwongozo huo ambao ulilalamikiwa na viongozi wengi wa kisiasa kwa kuwa ulitoa changamoto ya kupata viongozi mbadala, ulitetewa kwa nguvu zote na Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Polycarp Kadinali Pengo.

Pengo alisema, “Hakuna mwenye mamlaka ya kuzuia viongozi wa dini kufikia waamini wao” na kwamba hawatarajii kufundishwa jinsi ya kufanya kazi yao.

Akiongea kwa sauti ya ukali kwenye mazishi ya Mhashamu Askofu Anthony Mayala, Agosti mwaka jana, Pengo alisema hatua ya serikali kutaka nyaraka za kanisa kushirikisha serikali, inalenga kuyavua makanisa uwezo wa kusimamia mamlaka ya Mungu.

Hotuba ya Pengo ilitolewa mbele ya Rais Jakaya Kikwete, rais mstaafu Benjamin Mkapa na viongozi wengine wa CCM na serikali ambao hawakuwa na muda wa kujibu.

Akitumia staili ya kuongea ya MacAnthony katika kitabu cha Shakespeare cha Kaizari, Pengo alisema, “Ndugu zangu nimekuja kumzika Askofu, sikuja kuleta mambo ya ugomvi…”

Tangu hapo serikali imepata mashambulizi kutoka kila kona kuhusu inavyoendesha shughuli zake na hasa mwelekeo wake kuhusu watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Taarifa za kuaminika zinasema viongozi wa CCM waliotumwa kukutana na viongozi wa kidini, ni aliyewahi kuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais, John Malecela na makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa.

Wakati Msekwa ametumwa kukutana na Kardinali Polycarp Pengo, Malecela ameagizwa kukutana na kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikana, Valentine Mokiwa.

Habari zinasema, Kikwete amelazimika kuchukua hatua hiyo ya kutuma vigogo waandamizi wa chama chake baada ya kuona kuwa matamko na misimamo ya viongozi wa kidini, vinaweza kukivuruga chama chake katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

“Unajua haya mambo ya maaskofu si madogo. Maaskofu wanaonekana kama wameanza uasi. Wametoka kule walikokuwa na sasa wanazungumza mambo ya uongozi hadharani,” ameeleza mjumbe mmoja wa CC ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini.

Alisema, “Hata nchini Kenya mambo yalianza hivihivi. Maaskofu walipiga kelele kwa uchungu kukemea watawala kwa kukumbatia watuhumiwa wakuu wa ufisadi. Hatimaye, Daniel arap Moi alianguka. Hivyo Kikwete ameona vema atafute njia ya kunyamazisha viongozi hawa.”

Hata anguko la Mwai Kibaki, kama siyo kwa ufisadi katika uchaguzi wa 2007, lilitokana na kauli za viongozi wa dini waliokemea utawala mbaya na ufisadi ndani ya serikali yake.

MwanaHALISI limefahamishwa na mtoa taarifa wake, kwamba wakati Kikwete akitoa maagizo hayo alikuwa anaonyesha upole na unyenyekevu.

Hata hivyo, Kikwete ameelezwa kuwa mbogo pale Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba alipotaka kupewa kazi ya kukutana na viongozi wa madhehebu.

Taarifa za ndani ya CC zinasema awali Makamba alimuomba rais Kikwete kumpa kazi ya kuzungumza na viongozi wa dini kwa maelezo kwamba anafahamiana nao vizuri.

Huku wajumbe wakiwa bado wanatazamana na kutafakari, ghafla Kikwete aliingilia kati na kupinga ombi la Makamba.

Kikwete amenukuliwa akimwambia Makamba, katika hali ya ukali, kuwa wamwagize yeye akaongee nini wakati amezoea kutukana na kushambulia tu.

Hata hivyo, haikuwezekana kuthibitisha iwapo Msekwa na Malecela tayari wameanza kufanya kazi waliyopewa.

Uamuzi wa Kikwete wa kutaka kutafuta suluhu na viongozi wa kidini, umekuja wiki moja baada ya viongozi wa madhehebu ya kikristo kukutana Dar es Salaam katika kile kinachoitwa, “Kongamano la kupigia debe uadilifu.”

Kongamano la viongozi wa kanisa ambalo lilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na kuhudhuriwa na maaskofu kutoka CCT na TEC, lilifanyika kati ya 14 na 16 Machi mwaka huu.

Kikao cha CC kilichofanyika ikulu, Dar es Salaam, hakikuwa katika ratiba ya kawaida ya vikao vya chama hicho. “Kile hakikuwa cha kawaida. Kilikuwa cha dharula,” kimeeleza chanzo cha taarifa.

Hata hivyo, haijulikani kama kuitishwa kwa kikao hicho cha CC ghafla kulitokana na mkutano wa madhehebu ya kidini wa kupigia debe uadilifu.

Kikao cha CC kimefanyika miezi tisa tangu kanisa kujibu serikali kuwa haliwezi kutafuta ushauri kwake kila linapotaka kuwasiliana na waamini wake.

Katibu Mkuu wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Dk. Leonard Mtaita alikiri kufanyika kwa mkutano wa viongozi wa madhehebu ya kikristo uliofanyika Dar es Salaam na kujadili, pamoja na mambo mengine, “maadili ya viongozi.”

Hata hivyo, Mchungaji Mtaita amesema hajihusisha zaidi na undani wa kilichojadiliwa na maazimio ya mkutano kwa kuwa wakati mkutano unafanyika alikuwa nchini Sudan.

Naye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Mchungaji Askofu Thadeus Ruaichi amekiri kufanyika kwa mkutano huo wa kidini na kusema kuwa wameanza kutekeleza kile wanachokihubiri.

Mchungaji Jesica Mkichu, aliyeshiriki mkutano huo amesema, “Hata yaliyohubiriwa kwenye sherehe za Pasaka ni sehemu ya waliyofundishwa kwenye mkutano huo wa kidini.”

Karibu viongozi wote wa madhehebu ya kikristo waliohubiri wakati wa Pasaka, walikemea rushwa katika uchaguzi kutaka wananchi kuacha kuchagua wala rushwa ambao, walisema wanasababisha nchi kuendelea kuwa masikini.

Miongoni mwa maazimio ya mkutano wa viongozi wa dini ni kuelimisha waamini wao na wananchi kwa ujumla, kuchagua viongozi waadilifu.

Maazimio mengine, ni kutaka waamini wachague mgombea mcha mungu, “hata kama anatoka katika dini ya jiwe; anayependa nchi yake, si kwa maneno bali ni kwa vitendo.”

Sifa nyingine ya mgombea urais anayetakiwa ni kuwa mzalendo wa kweli na aliyetayari kulinda maslahi ya taifa na kuacha kubeba watuhumiwa wa ufisadi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: