Kikwete awaliza Maaskofu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version

MAASKOFU na waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wamesikitishwa na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutoshiriki kikamilifu katika sherehe za Jubilei ya miaka 100 ya kanisa hilo katika Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, imefahamika.

Rais alialikwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Kanisa katika Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, zilizofanyika mjini Bukoba, Jumapili iliyopita.

Taarifa zinasema licha ya rais kuwasili akiwa “amechelewa” na kukuta shughuli zimeanza, aliondoka mara moja baada ya kusoma hotuba yake kwenye mkusanyiko mkubwa wa maaskofu wa kanisa hilo na waamini wake.

“Rais aliondoka bila kupata chakula cha pamoja na wenyeji wake,” ameeleza mtoa taarifa wa kanisa hilo kwa sauti ya unyonge.

“Ni kinyume na matarajio ya viongozi wa Kikristo. Rais Kikwete hakuhudhuhuria ilivyopasa, ibada ya pamoja ya kuadhimisha miaka 100 ya kanisa letu, wala kula chakula kilichoandaliwa kwa ajili yake na wageni wengine kutoka duniani kote,” ameeleza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa kanisa hilo.

Badala yake, rais alifika eneo hilo la wazi ambako ibada ilikuwa ikifanyika, wakati ibada ikiwa imemalizika na aliondoka bila kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa rasmi kwa ajili yake.

Inaelezwa kwamba Kikwete alitarajiwa kufika kwenye shughuli hiyo saa mbili asubuhi ili kuwa na waamini wakati wa kuanza ibada ya pamoja, lakini taarifa zinasema alifika majira ya saa tano.

Wakati huo, ibada ilikuwa imekwisha na ilikuwa zamu ya wageni waalikwa kutoa salamu.

Baada ya kuwasili, taarifa zinasema Rais Kikwete alikwenda moja kwa moja jukwaani ambako walikuwa wameketi maaskofu.

Katika sehemu hiyo, rais aliketi pamoja na mkuu wa mkoa wa Kagera, Mohammed Babu ambaye alikuwa amekaa mkono wa kulia wa rais na kushoto kwake alikaa Askofu wa Bukoba, Elisa Buberwa na mkuu wa Kanisa la KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa.

Taarifa nyingine zimesema mapema Jumapili asubuhi, Rais Kikwete alikuwa amewasiliana na viongozi wa kanisa na kueleza kuwa asingehudhuria ibada ya pamoja, kutokana na uchovu aliokuwa nao.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na maaskofu mbalimbali na wawakilishi wa majimbo rafiki kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Hakika rais amesikitisha wengi. Kwanza, alichelewa kufika, lakini pili hakula chakula cha pamoja kilichoandaliwa kwa ajili yake,” amesema kiongozi mmoja wa madhehebu hayo aliyehudhuria sherehe hizo.

Amesema, “Viongozi na waamini wamekichukulia kitendo hicho kuwa cha kutowathamini. Badala ya kuja saa mbili asubuhi, anafika saa tano na kuondoka kabla ya sherehe kuingia katika sehemu muhimu ya kupata chakula pamoja,” ameeleza muumini huyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waandaji wa sherehe hizo, rais aliondoka mahali hapo mara baada ya kumaliza kusoma hotuba yake akitarajiwa kurejea tena baadaye kuungana na wenyeji wake kwa ajili ya chakula cha pamoja.

Imeelezwa kuwa rais alipomaliza kusoma hotuba yake aliondoka pamoja na mkuu wa mkoa kwenda ikulu ndogo, na ilitarajiwa arejee muda mfupi baadaye kwa ajili ya kupata chakula.

Hata hivyo, muda kidogo ilipatikana taarifa kwamba hatarejea.

“Kwa msononeko, maaskofu wakalazimika kula chakula bila mgeni wao maalum. Ukweli ni kwamba hili limesononoesha wengi,” ameeleza msaidizi wa mmoja wa maaskofu.

Akizungumza taratibu, msaidizi huyo wa askofu alisema “…hata Askofu Mkuu wa Kanisa la Bukoba, Elisa Buberwa ameonekana kusikitishwa na kustushwa na tukio hilo.”

MwanaHALISI lilishindwa kumpata Askofu Buberwa kwa maelezo kwamba hakuwa kazini siku nzima Jumatatu, kutokana na uchovu wa shughuli za sherehe na kwamba alikuwa anajisikia maumivu mwilini.

Naye, Katibu wa Askofu, Godwin Lwezaura, hakupatikana kueleza kilichotokea. Alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.

Baadaye katibu muhtasi wa askofu alisema Lwezaura alikuwa safarini mkoani humo katika visiwa vya Bumbiire na Goziba. Alimtaka mwandishi amtafuta Jumanne (jana).

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Askofu na Katibu Mkuu wa KKKT, zinasema kwamba Rais Kikwete aliwasili Bukoba siku ya Jumamosi, majira ya saa moja usiku badala ya saa saba mchana kama iliyokuwa imepangwa.

Malalamiko haya mapya ya waamini wa madhehebu ya Kilutheri yamekuja miezi miwili tangu Rais Kikwete akutane na viongozi wa dini katika semina ya siku moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Malasusa, alipoulizwa kuhusu tukio hilo la rais, alisema yeye alikuwa kama rais – wote walikuwa wageni waalikwa.

Alisema kwa taarifa sahihi, mwandishi amtafute askofu wa Bukoba ambaye alikuwa mwenyeji wao.

Akizungumza katika kilele cha sherehe hizo baada ya kuwasili, Rais Kikwete alitaka viongozi wa madhehebu ya kidini kukemea wanasiasa wanaoweza kutafuta madaraka kupitia mlango wa dini.

Alitaka kanisa kuwafundisha waamini wao kuwakataa wanasiasa hao kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kwa maelezo kwamba wanaweza kuingiza nchi katika maangamizi.

Alisema, “Tusiwaendekeze. Mchezo wao ni mauti yetu. Tukiruhusu ubaguzi huu, ndiyo mauti yetu. Ni lazima tujihadhari na viongozi hawa waoga, wasiojiamini na wanaopenda madaraka kwa gharama yoyote,” alisisitiza.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: