Kikwete: Ballali bado hajafa


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 03 June 2008

Printer-friendly version

TANGU zilipoibuka taarifa za kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dk. Daudi Ballali, Watanzania tumekuwa na maoni mchanganyiko kuhusu kifo hicho.

Hadi sasa, wapo wananchi wengi wanotilia shaka kifo cha Ballali, wakidai kwamba serikali imefanya njama za kumficha ili kulinda ufisadi ambao imekuwa inashitakiwa nao, kutokana na wizi uliokithiri wa mabilioni ya pesa za umma.

Kuna madai kwamba fedha hizi zimeingizwa katika kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliomuweka madarakani Rais Jakaya Kikwete. Kama kuna mtu aliyepaswa kueleza ukweli hasa wa wizi huo ni Ballali, akisaidiwa na maofisa wa CCM, serikali na BoT waliohusika katika ukwapuaji huo.

Wakati wananchi kadhaa wanatilia shaka kifo cha Ballali, wakisema serikali imekula njama na familia yake ili kunyamazisha sokomoko hili, wapo wananchi wenye kuamini kwamba Ballali ni hayati, na kwamba kifo chake kimesababishwa na serikali na wapambe wake.

Kwa vyovyote vile, wananchi wanaonekana kuchoshwa na serikali; hawana imani nayo, na wanaituhumu kwa mauaji na kushamirisha ufisadi. Katika hali yoyote iwayo, kwa msimamo wowote utakaoelezwa na kukubalika, Ballali anayetafutwa na wananchi, bado hajafa.

Kama amekufa, ni mwili wake tu; na kiwiliwili kimezikwa. Roho yake inaishi. Lakini makala hii haizungumzii uhai wa kiroho wa Ballali. Ballali anaishi katika kazi zake. Kazi alizosimamia, safi na chafu bado zipo katika ofisi yake aliyokuwa anaiongoza.

Mafaili yake yamebaki. Vile vimemo alivyokuwa anatumiwa na wakubwa serikalini ili kuruhusu pesa zitoke, bado vipo. Yale makaratasi ya vijikampuni feki vya wapambe wa CCM - Kagoda na wenzake - vipo katika kumbukumbu za Benki Kuu.

Uzuri ni kwamba hata wamiliki wa makampuni feki yaliyotumiwa kuchota pesa hizo wapo hai, na wengine ndio wanasemekana kuharakisha 'kifo' cha Ballali. Hata maofisa wa BoT waliohusika na ukwapuaji huo bado wapo.

Hata aliyekuwa Mkurugenzi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Peter Noni ambaye anatajwa kuwa alisaini mkataba wa ununuzi wa madeni kati ya kampuni ya Kagoda Agriculture Limited na BoT; na hatimaye Kagoda kuchotewa zaidi ya Sh. 40 bilioni bado yupo.

Si hivyo tu, hata mfanyabiashara kigogo ambaye aliyesaini mkataba huo kwa niaba ya Kagoda, bado yupo mitaani anatanua.

Kwa sababu hiyo, iwapo serikali ina nia ya kuchunguza ukweli kuhusu wizi wa Benki Kuu, haiwezi kusingizia kukosa ushahidi au vielelezo, eti kwa vile Ballali kafa.

Kama ingekuwa serikali makini, ingekuwa imekamilisha hata kumhoji kabla hajakata roho.

Zipo taarifa kwamba ingawa serikali ilikuwa ikitoa taarifa kuwa haikujua nchi alikokuwa, hospitali alikolazwa na ugonjwa anaoumwa, baadhi ya maofisa waandamizi wa BoT na serikali walikuwa wakimtembelea mara kwa mara "kumjulia hali."

Ni serikali hii hii ambayo awali ilikiri kwamba inamlipia matibabu (ya ugonjwa isiyoujua na katika hospitali wasiyoijua)!

Ni serikali hii ambayo baadaye ilipobanwa, wiki moja kabla ya kifo chake, ilisema kwamba haimhitaji Ballali, na kwamba ikimhitaji haiwezi kushindwa kumpata kwa sababu ina "mkono mrefu."

Wanaoituhumu serikali wanasema mkono huo mrefu ndiyo umemmaliza, kwani serikali haikumhitaji. Sababu za kutomhitaji zinajulikana.

Ballali aliajiriwa na serikali, na alitumiwa na serikali kurahisisha wizi wa mabilioni yetu Benki Kuu.

Zaidi ya hayo, walioiba mabilioni hayo hawakuyatumia yote, bali waliyatumia kuwezesha serikali ya awamu ya nne kuingia madarakani.

Kwa sababu hiyo, serikali hii tunayotarajia itueleze ukweli kuhusu wizi wa Benki Kuu, ni zao la wizi huo huo; hivyo haiwezi kamwe kujidai kwamba inaweza kuchukua hatua dhidi ya wezi.

Kwa sababu hiyo, vyanzo vya habari vya gazeti hili, vingine vikitoka serikalini na Benki Kuu, viliwahi kueleza kwamba kama kuna mtu ambaye hataki Ballali arejee Tanzania, ni vigogo wa chama tawala.

Vilisema viongozi wa CCM wanaona aibu kila linapozungumzwa suala la Ballali na wizi wa Benki Kuu, kwani wizi huo ulifadhili kampeni zao; na baadhi ya waliohusika ni waliokuwa wanakamati wa mgombe urais.

Kwa hiyo, wizi huu wa mabilioni ya BoT ulikuwa sehemu ya mkakati wa ushindi wa CCM. Kwa hiyo, serikali inayoongozwa na chama hicho, kamwe hakiwezi kuwakamata wanamkakati wake wala Ballali na wengine wanaohusika.

Vyanzo hivyo vilieleza kuwa sababu hizo hizo ndizo zinamfanya rais kushindwa kuchukua hatua dhidi ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutokana na Ballali kuwa alikuwa anatekeleza maagizo ya wakubwa.

Kwamba kama Mkapa alituma vimemo BoT na vimemo hivyo vilimsaidia Kikwete, hakuna uwezekano wowote wa Kikwete kumshughulikia Mkapa katika suala hili.

Sasa ni dhahiri kwamba baada ya kifo cha Ballali, baadhi ya watendaji serikalini na wafanyabiashara waliokuwapua wanaweza kudhani kwamba "watapumua" kwa sababu shahidi mkuu ameondoka. Hakika, wanajidanganya.

Ushahidi ni zaidi ya kauli ya Ballali. Ingawa ni kweli kuwa kauli ya Ballali ingeongeza uzito katika kumulika mbinu chafu zilizotumika, na kuwatambua kwa majina watu waliomshinikiza kuidhinisha wizi (ingawa tayari wanajulikana), kumbukumbu alizoacha nyuma zinatosha kuweka mambo yote hadharani kama serikali ingekuwa na nia njema.

Mfano wa hivi karibuni wa matumizi ya kumbukumbu hizo ni pale Kamati ya Bunge chini ya Dk. Harrison Mwakyembe iliyochunguza kashfa ya mradi wa Richmond ilipoona ushahidi wa shinikizo la wakubwa katika ugawaji tenda kwa kampuni hiyo.

Ingawa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, aliyetumiwa vimemo hivyo, alikuwa ameshahamishwa wizara hiyo, kamati iliviona na ilivitumia kuwagundua waliohusika na shinikizo lililoipa tenda hiyo kampuni hiyo ya kitapeli.

Na kutokana na shinikizo hilo, Kamati ilihitimisha kwa kuwataja waliohusika na kupendekeza hatua za kuchukuliwa dhidi yao.

Ushujaa huu wa Kamati ya Mwakyembe ungetumika katika uchunguzi unaofanywa sasa Benki Kuu, tungeshuhudia mengi yanayofichwa na serikali, hasa katika kifo cha Ballali.

Lakini hatutarajii ujasiri kama huo ujitokeze sasa kwa sababu mwenendo wa mambo unaonyesha kuwa serikali imeunda kamati yake kwa nia ya kuficha si kufichua ukweli.

Na kwa kuwa serikali haipendi kuweka mambo bayana hadi hapo inapokuwa imebanwa sana, tunajua kuwa hata katika hili itaendelea kuharibu vimemo vya Ballali, Mkapa na wamiliki wa Kagoda ili kupoteza ushahidi wa vile "Ballali ameshakufa."

Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale. Ballali hakufa na vimemo. Ameondoka na roho yake, na kuacha ukweli nyuma.

Ukweli huu ndiyo tunaotaka serikali itueleze sasa. Isipofanya hivyo kwa hiari, wananchi wanaweza kuihukumu siku si nyingi, ili kulinda maslahi ya taifa.

Serikali ifanye itakavyo, lakini kwa wengi wetu, Ballali bado hajafa. Vimemo vipo, sahihi zake na wahusika wengine zipo. Vitumike kuanika ukweli wa mambo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: