Kikwete chupuchupu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 February 2012

Printer-friendly version

MPANGO wa kuzima wabunge kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nusura umwengue Rais Jakaya Kikwete.

Katika kikao cha rais na wabunge na baadaye katika halmashauri kuu, mapendekezo ya kuzuia wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kugombea ujumbe NEC lilipingwa kwa nguvu, MwanaHALISI limeelezwa.

Ilikuwa katika kikao na wabunge, rais aliambiwa kuwa kujaribu kuzuia wabunge kugombea NEC ni kama “kutenganisha kofia;” na kwamba iwapo hilo litatokea kwa wabunge basi “litakwenda hadi juu.”

Kauli hiyo iliyoonekana kuwa tishio kwa rais ilitolewa na mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka ambaye taarifa zinasema ililenga kufafanua kuwa utenganishaji kofia utahusu pia nafasi ya rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, jambo ambalo alisema ni “hatari kwa sasa.”

Kwenye ukurasa wa 10 wa mapendekezo ya marekebisho ya uchaguzi wa CCM, Toleo la Februari 2010, inatamkwa kuwa hakuna atakayeteuliwa kugombea ujumbe wa NEC iwapo tayari ni “mwakilishi wa wilaya hiyo katika vikao vingine vya kitaifa, hususan bunge na baraza la wawakilishi.”

Alikuwa Said Nkumba, mbunge wa Sikonge aliyeanza kumhoji Rais Kikwete katika kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika ukumbi wa White House, Ijumaa mjini Dodoma.

Nkumba alimtaka Rais Kikwete kutoa ufafanuzi juu ya kuwapo kwa madai kuwa katika mabadiliko ya katiba ambayo yamepangwa kupitishwa, kuna sharti linalozuia wabunge kutoruhusiwa kugombea nafasi za NEC kupitia wilayani.

Akijibu madai ya Nkumba na hasa baada ya kusoma sura za wabunge, mtoa taarifa anasema Rais Kikwete alisema kwa sauti ya upole, “…katika mabadiliko ya katiba yanayoandaliwa, hakuna mpango wa kuwazuia wabunge kugombea nafasi za NEC.”

Iwapo mjadala juu ya “kofia mbili” za NEC na ubunge ungeendelea, taarifa zinasema baadhi ya wabunge walikuwa tayari wamejipanga kumwambia rais kuwa naye aachie cheo kimoja kwa ajili ya ufanisi.

Pamoja na maelezo hayo, wasiwasi ulizidi kuwakumba wabunge, kuwa huenda wakazuiwa kuingia kwenye chombo hicho muhimu, huku wajumbe wengine wa NEC wakihofia kukosa nafasi ya kuwania ubunge hapo baadaye.

Katika kikao cha NEC, Jumapili ndiko kulizuka mjadala mwingine mkali, huku mkongwe wa siasa na mshauri wa rais, Kingunge Ngombale- Mwiru alikataa kukubaliana na maamuzi juu ya mabadiliko yoyote katika katiba.

Akiongea kwa sauti yake kali, Ngombale alikaririwa akipinga kwanza, kuenguliwa kwa viongozi wakuu wastaafu kwenye chama kwa njia ya kuwaundia Baraza la Ushauri. Alisema hatua hiyo itafanya chama kikose watu wa kukilea.

Aidha, Ngombale alisema, “NEC haina madaraka (ya kufanya mabadiliko) hayo,” na kuongeza kuwa kubadili katiba kwa njia hiyo halikuwa jambo sahihi.

Mapendekezo ya marekebisho ya katiba ambayo yalipitishwa, yanasema viongozi wakuu wastaafu “hawatakuwa wajumbe wa vikao vya chama ngazi ya taifa;” badala yake wanaundiwa Baraza la Ushauri ambalo litatoa ushauri kwa CCM na serikali zake.

Kwa mujibu wa maamuzi hayo, wastaafu wataitwa kuhudhuria vikao vya kitaifa pale tu uongozi wa chama utakapoona kuwa “busara zao zinahitajika, hususan katika masuala magumu na nyeti.”

Kuhusu mpango wa kuzuia wabunge kuwa wajumbe wa NEC, Ngombale alisema, “Huwezi kufanya haya kama unakitakia mema chama hiki. Labda kama mtakuwa mnathibitisha madai kuwa kuna agenda iliyojificha.”

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Ngombale alisema, “Nataka niwekwe kwenye rekodi; huu si uamuzi sahihi.

Hata mkipeleka wajumbe wa NEC kwenye ngazi ya kata, kama serikali iliyopo madarakani ambayo inatokana na chama hiki haitimizi wajibu wake, hakuna jambo lolote litakaloleta matumaini.”

Kwa msisitizo, Ngombale alisema, “Naomba mniweke kwenye kumbukumbu kwamba nimelipinga jambo hili.”

Mtoa taarifa ameliambia gazeti hili kuwa wakati wa kupitisha suala hilo, Ngombale alisema, “Pitisheni, hilo la kwenu.”

Ngombale amenukuliwa akisema, utaratibu wa kupata wajumbe wa NEC kutoka wilayani, utakuwa na athari kubwa kwa chama hicho kwenye siku za usoni; kwani utakifanya chama kuwa na makundi makubwa ya ugomvi na visasi.

Kabla ya Ngombale kuchangia, Peter Serukamba , mjumbe na mbunge wa Kigoma Mjini, alisimama na kupinga utaratibu mpya wa kutaka kung’oa viongozi wakuu wastaafu kwenye vikao vya maamuzi.

Lakini alikuwa Abdulrahman Kinana, mjumbe aliyewahi kuwa meneja wa kampeni wa Rais Kikwete mara mbili, aliyepigilia msumari wa mwisho kwa kueleza kuwa “hata wastaafu wenyewe wamekubaliana na jambo hili.”

Huku akimtolea macho rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Kinana alisema, “Au siyo Mzee Mwinyi.” Mwinyi aliitikia kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana.

Mpango wa kuwatelekeza wastaafu katika baraza la ushauri umekuwa ukijadiliwa tangu mwaka jana. Makamu mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Samwel Malecela alinukuliwa Novemba akisema, mpango huo “haukubaliki.”

Wachunguzi wa mambo ya siasa wanasema Malecela ana haki ya kusema hivyo kwa kuwa utaratibu mpya unampokonya hadhi ya kuwa “Mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM” aliyopewa na Rais Kikwete mara baada ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Naye Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipotakiwa kufafanua suala la Malecela, alisema hoja ya Baraza la Ushauri sharti itazamwe “kwa nyadhifa badala za watu na majina yao.”

Alipobanwa kwa ufafanuzi zaidi, alisema kuwa yakitolewa maamuzi mapya ya vikao sasa, “kwa vyovyote vile yanafuta maamuzi ya zamani.”

Nape akizungumzia nafasi ya wajumbe wa NEC wanaogombea kutoka wilayani huku wakitakiwa kuwa “viongozi wa kazi za muda wote,” alisema zipo nafasi kama ile ya mwenyekiti wa wilaya, diwani, mbunge – kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa CCM – ambazo si za ajira lakini za muda wote.

“Hawa wanafanya kazi za chama za kila siku ndani ya chama, si waajiriwa wala hawalipwi mshahara. Hivyo hawa wajumbe wa NEC wa wilaya pia watakuwa katika kundi hili,” alifafanua.

Wakati huohuo, marekebisho hayo yameongeza idadi ya wajumbe wa NEC kutoka kati ya 100 na 200 hadi karibu 370 ambao wanaelezwa na baadhi ya wajumbe kuwa ni wengi na watakuwa mzigo mkubwa kwa chama.

Kikao hicho kitakuwa na wajumbe10 kutoka Tanzania bara, 10 kutoka Visiwani na wengine 10 wa kuteuliwa na mwenyekiti wa CCM taifa.

Pia wamo wanaoingia kwa nafasi zao kama wenyeviti wa CCM mkoa, spika na waziri mkuu wanaotokana na CCM, wenyeviti na makatibu wa jumuiya za chama na makamu wa rais wa Muungano na Zanzibar wanaotokana na CCM.

Wajumbe wengine watakaotoka kwenye vyombo vya uwakilishi ni wabunge 10 (bara 8, Zanzibar 2);

wajumbe watano wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe wanaochaguliwa kutoka wilayani ambao ni 221.

Vilevile watakuwamo wajumbe kutoka kwenye jumuiya za chama, 15 kutoka UWT (bara 9, Zanzibar 6); UVCCM 10 (bara 6, Zanzibar 4) na watano kutoka Wazazi (bara 3, Zanzibar 2).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: