Kikwete na Dowans: Bado ni mchezo wa kuigiza


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete amekubali hadharani kuwa kampuni ya kufua umeme ya Richmond ilikuwa “kampuni hewa” na kwamba kampuni ya Dowans ilirithi mkataba wa kufua umeme wa kampuni feki.

Kile ambacho rais anashindwa au anakataa kusema waziwazi ni kwamba, shetani huzaa shetani.

Rais alitegemewa na wananchi aeleze kilichoikumba serikali yake hadi kuingizwa mkenge na wanaojiita “wamiliki wa Dowans” wanaodai TANESCO fidia ya Sh. 94 bilioni kwa kukatisha mkataba wao. Ama ameshindwa au amekataa kufanya hivyo.

Akizungumza katika kilele cha sherehe za miaka 34 ya kuzaliwa kwa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Rais Kikwete alikiri kuwa Richmond Development Company (LLC), iliyorithisha mkataba wake kwa Dowans, ilikuwa “kampuni hewa.”

Hata hivyo, Kikwete alisema, “Dowans iliweza kuleta mitambo ya kuzalisha umeme” na kwamba mitambo iliyoletwa ikafanya kazi na “kupunguza makali ya mgao.”

Kauli ya rais kwamba Dowans ilileta mitambo ya kuzalisha umeme, mitambo ikafanya kazi na umeme ukapatikana, haiwezi kuhalalisha, kwa kiwango chochote kile, mkataba uliofungwa.

Kauli ya rais, wala haiwezi kushawishi wananchi kuwa Dowans inastahili kulipwa inachodai.

Bali wananchi sasa wanajiuliza: Kama rais alijua Richmond ilikuwa kampuni hewa na Dowans imerithi mkataba wa kampuni hewa, kwa nini anasema, “Tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka kulipa.” 

Anachotakiwa na hasa anachotarajiwa kusema ni, “Hatuwezi kutumia fedha za umma kuilipa kampuni hewa.” Basi.

Lakini kusema amepata ushauri ukiwamo uliosema, “Tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria,” hapa kuna kitu ambacho rais bado hajakisema.

Kwanza, kama rais alijua Richmond ilikuwa kampuni hewa, kwa nini ameshindwa kueleza hatua alizochukulia aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi aliyejigeuza mtumishi wa Richmond na Dowans kwa kutolea makampuni hayo taarifa za kuyakinga?

Pili, kama rais anasema Dowans ilirithi mkataba kutoka kampuni hewa, kwa nini anataka serikali ikishindwa mahakamani ilipe fedha hizo?

Tatu, kama rais anakiri kuwa Richmond ilikuwa kampuni hewa, kwa nini ameshindwa kumfuta kazi Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hoseah aliyeisafisha Richmond?

Nne, kama amekiri Richmond ni kampuni hewa, aeleze amemchukulia hatua gani Rostam Aziz, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama chake, mbunge na swahiba wake, aliyejitwisha mkataba wa kampuni feki kwa faida binafsi lakini kwa hasara kwa taifa hili?

Kikwete anajua, kwa jinsi taifa hili linavyojifunga katika mikataba yake na makampuni ya kigeni; na jinsi baadhi ya waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali za taifa walivyopoteza uzalendo, Dowans watalipwa.

Hili linajidhirisha hata katika maneno na vitendo vya wasaidizi wake. Mathalani, matamshi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, kwamba “hakuna sababu ya kupinga hukumu ya Dowans.” Haya yanathibitisha kuwa Dowans watalipwa.

Yuko wapi mwanasheria shupavu serikalini, mjuzi, mweredi wa kazi, mwadilifu na mtiifu kwa rais, kuliko Jaji Werema? Bila shaka hayupo?

Iwapo Jaji Werema ameshaeleza Dowans walipwe, bila shaka baada ya kuteta na aliyempa kazi, kauli kuwa rais ameagiza wanasheria kutafuta njia ya kuzuia malipo hayo zinatoka wapi na zina uzito gani? Ni nani hao wanasheria, nje ya mwanasheria mkuu? Au Kikwete aseme basi, amemfuta kazi Werema.

Katika kuhalalisha maelezo yake, Kikwete alifika mbali. Alisema aliyekuwa waziri wa nishati na madini wakati huo, Ibrahim Msabaha, alikwenda kumuomba aingilie kati ili kampuni ya Richmond ipewe malipo ya awali.

Alisema, “Nikataa na kumwambia waziri aachane nao kwani kampuni hiyo ni ya mashaka.”

Kampuni ya Richmond haikupewa malipo ya awali. Lakini serikali iliidhamini katika mabenki. Ililipiwa kile kilichoitwa, barua ya dhamana (Letter of Credit - LC).

Hapa rais anaibua hoja nyingine. Anathibitisha madai ya wengi kuwa vyombo vyake vya kiitelejensia, ama ni dhaifu au vimewekwa mifukoni na wenye fedha.

Haingii akilini kuwa Rais Kikwete ajue kuwa Richmond ni kampuni hewa, kama alivyosema kwa kimombo – phantom company – halafu  serikali yake isijue, isichukue hatua lakini Bunge ling’amue. Huu utaitwa mchezo wa kuigiza.

Kuna hili pia. Rais anasema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa umeme, TANESCO walishauri serikali ikodishe mitambo hiyo. Tenda ikatangazwa na mzabuni akapatikana.

Hapa rais atakuwa ama hajasema ukweli au amesahau. Kwanza, ripoti ya Bunge imeeleza serikali haikutaka mitambo ya kukodisha.

Ilisema kikao cha baraza la mawaziri cha 10 Februari 2006, kiliagiza TANESCO kununua mitambo yake yenyewe kupitia mpango wa ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji.

Barua ya TANESCO ya 20 Februari 2006 iliyotumwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, inathibitisha kwamba serikali haikupanga kuingia katika “mtego” wa makampuni ya kitapeli ya kufua umeme wa dharula.

Ripoti ya Bunge ilimtuhumu moja kwa moja Edward Lowassa, kukiuka maagizo ya serikali. Kama maelezo ya rais yangekuwa sahihi, ilitarajiwa kukanusha madai ya Bunge. Hakufanya hivyo. Alikataa au alishindwa kufanya hivyo.

Aidha, Richmond haikupatikana katika mchakato wa wazi. Ilibebwa na Lowassa. Ripoti ya Bunge na nyaraka kadhaa za serikali, vinathibitisha kuwa Richmond haikuwa na sifa ya kufanya kazi iliyoomba.

Hivyo basi, ni dhahiri kuwa maelezo ya Kikwete katika hili, yamelenga kumkosha Lowassa kwa kutomtaja katika kashfa hii na kujikosha mwenyewe mbele ya jamii kwamba yuko mbali na swahiba wake Rostam Aziz.

Kikwete hawezi kusema kuwa hajui kwamba Rostam ndiye Dowans na ndiye Richmond. Huyu ndiye mahakama ya usuluhishi imeridhika kuwa ni mwenye haki ya kusimamia mali, kuingia mikataba, kuajiri mawakili na kufungua mashitaka dhidi ya yoyote kwa niaba ya Dowans.

Rais anajua, angalau kwa taarifa za MwanaHALISI zinazonukuu vyanzo visivyopingika, kuwa Rostam – mjumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, mweka hazina wa zamani wa CCM na mwenye mamlaka ya uwakilishi ya kampuni ya Dowans – ndiye Dowans aliyeshitaki na anayedai serikali yake Sh. 94 bilioni.

Aidha, Rostam amewahi kukiri kwamba ni yeye aliyewaleta (Dowans) nchini. Katika hili, rais hana sababu za kuzunguka mbuyu wakati wa kuelezea suala la Dowans kwa wananchi.

Kwani ni Rostam-Dowans wanaodaiwa kufungua shauri katika moja ya mahakama nchini Uingereza ili serikali ikishindwa au ikikataa kulipa, basi mali zake zinazolingana na kiasi wanachodai ziuzwe ili kulipa deni.

Hilo likitokea itakuwa kama mtoto anayechongea nyumba ya baba yake iuzwe huku akiwa hana wazo juu ya atakapoishi. Itakuwa hadithi ya panya anayekula paka. je, Rostam ataendelea kuishi katika nchi aliyoanza kuuza vipandevipande kuanzia mali zake zilizoko nchi za nje?” Hapo Rais Kikwete atakuwa wapi?

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: