Kikwete hachaguliki


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version
Mzimu wa Lowassa wamtafuna
Migawanyiko CCM yamponza
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete hauziki kama ilivyokuwa wakati akiingia madarakani, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejiridhisha.

Ili kumrejesha kwenye kinyang’anyiro kipya kwa ajili ya muhula wa pili wa urais, sharti kitumie karibu zaidi ya mara mbili ya fedha zilichotumia mwaka 2005.

Taarifa za ndani ya CCM zinasema zitahitajika zaidi ya Sh. 50 bilioni “kumbakiza Kikwete madarakani” kwa miaka mingine mitano ya muhula wake wa mwisho kikatiba.

Hata hivyo, juzi Jumatatu, Mwekahazina Amos Makalla alitangaza kuwa chama chake kitakusanya Sh. 40 bilioni kwa njia ya simu za mkononi (sms).

Mwaka 2005 CCM ilikisiwa kutumia zaidi ya Sh. 20 bilioni kwa uchaguzi, kiasi ambacho kitakuwa zaidi ya mara mbili mwaka huu, zimeeleza taarifa za ndani ya chama hicho.

Kuongezeka kwa matumizi ya chama hicho kunakuja wakati serikali ya Rais Kikwete ikibanwa kwa kutokuwa makini, kutochukua maamuzi na kutotekeleza ahadi zake lukuki zilizotolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005.

Aidha, matumizi ya fedha zaidi yanakuja wakati kuna mivutano na mgawanyiko dhahiri katika chama unaotokana na misimamo miwili iliyoibuka baada ya kashfa ya Richmond tangu mwaka 2007.

Wachambuzi wa siasa za CCM wanaona hatua hii ya kukusanya fedha nyingi ina lengo la kujihami dhidi ya “hujuma yoyote inayoweza kufanywa na wanaotaka kuchukua fursa ya udhaifu” uliopo ndani ya utawala.

Udhaifu huu imedhihirika kwa njia ya baadhi ya mawaziri kuzomewa na wananchi kila walipokwenda na kushindwa kujibu maswali ya wananchi.

Kiwango hiki kikubwa cha fedha kinalenga pia kupambana na upinzani ndani ya chama hicho; upinzani ambao umezaa makundi na mfarakano usiosuluhika, wanaeleza wachambuzi.

Naye wakili wa mahakama kuu, Mabere Marando ameliambia MwanaHALISI kuwa “Wanakusanya fedha nyingi kwa kuwa wanataka kuhonga nchi nzima…wasipohonga watashindwa.”

Akijibu swali kwa nini CCM itumie kiasi chote hicho, Marando alisema, “Kikwete hakutekeleza ahadi zake; wabunge wake hawakutekeleza ahadi zao; na wananchi wanajua kuwa wao ni mafisadi. Lazima wahonge ili kupata kura.”

“Miaka yote mitano imeishia kugombania madaraka. Na hizo Sh. 40 bilioni wataiba tu kwa sababu hawawezi kuzipata kutoka kwa mashabiki wao. Ni mbinu za wizi ndani ya serikali na sisi tunajua…” alisema Marando.

Wakati Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa akisema “CCM hawachaguliki…ndio maana watatumia fedha nyingi sana,” Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu amesema matumzi ya aina hiyo hayawezi kuleta “siasa safi za utawala bora.”

Ladhu amesema siasa za Tanzania zitaendelea kudhibitiwa na wenye fedha ambao watakuwa wanaichagia CCM kwa mlango wa nyuma.

Kuliko katika kipindi kingine chochote, CCM itaingia uchaguzi ujao ikiwa imegubikwa na tope la kashfa mbalimbali za ufisadi ambazo zimedhoofisha viongozi wake mbele ya umma.

Wizi katika Benki Kuu (BoT) kwa njia ya makampuni ya kitapeli; mkataba wa utata na upendeleo kwa kampuni ya Richmond ambao ulimg’oa Edward Lowassa kwenye uwaziri mkuu; na rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi, ni baadhi ya kashfa zilizoichafua serikali mbele ya wananchi.

Mikataba ya kinyonyanyi ya madini, uhamishaji wananchi kutoka maeneo yao ya kuishi miaka yote ili kupisha watu kutoka nje kwa madai ya uwekezaji; na ubaguzi na bughudha kwa wafugaji – vyote vimeleta sura mbaya ya serikali kwa wananchi.

Mgogoro mkubwa na wa aina yake kati ya serikali na walimu umemomonyoa hadhi ya serikali.

Wachunguzi wanasema kwa vile walimu wako kila mahali na kwa kuwa “wako karibu na wazazi na vijana nchini kote, athari zao ni kubwa sana kisiasa. Hili linahitahi kujihami kisiasa na hata kujitahidi kuziba mapengo.”

Kasoro nyingine kubwa ambayo inatajwa itakuwa mzigo mkubwa kwa CCM ni mgomo wa wafanyakazi uliopangwa kufanyika nchi nzima Mei mwaka huu.

Madai ya nyongeza ya kima cha chini kwa wafanyakazi wa serikalini na sekta binafsi yanaendelea kuwa mwiba kwa serikali ya Kikwete.

Hata hivyo, kilicholeta kiwewe cha aina yake miongoni mwa watawala ni chama kipya – Chama Cha Jamii (CCJ) ambacho kuanzishwa kwake kulikuja wakati CCM ikitota kwa malumbano ya wabunge.

Ilitabiriwa kwamba chama hiki ambacho hakijapata usajili wa kudumu, kingechukua “vigogo” wengi kutoka CCM na hivyo kusababisha viongozi wa chama tawala kutoa kauli za kupaparika.

Ongezeko la matumizi ya fedha za kampeni za CCM kwa karibu zaidi ya mara mbili, kumehusishwa pia na ongezeko la vijana waliojiandikisha kupiga kura mwaka huu.

Kumekuwa na misururu ya vijana waliojitokeza kujiandikisha kupiga kura katika sehemu mbalimbali nchini, jambo ambalo siyo la kawaida. Inadaiwa kuelekeza nguvu hii mpya katika siasa za utashi kutahitaji gharama zaidi, hivyo kupanda kwa bajeti ya CCM katika uchaguzi.

Ahadi nyingi za Rais Kikwete bado hazijatekelezwa. Hata kile alichoita “Mabilioni ya Kikwete” kusaidia wajasiriamali kinadaiwa kufikia wachache au kupotea njiani.

“Hapa ndugu yangu, itabidi rais atafute jinsi ya kuziba nyufa. Vijana hawatamwelewa, kwa hiyo sishangai kusikia wanahitaji mabilioni yote hayo,” ameeleza Mzee Juma Mzee wa Kikwajuni Zanzibar alipohojwa na mwandishi wa gazeti hili.

Katika hali ya kawaida, mgombea mpya ndiye anahitaji kutumia fedha nyingi kwa utambulisho na kukata mbuga sehemu kubwa ya nchi ambako alikuwa hafahamiki.

Lakini kwa kuwa mwaka 2005 wananchi walimpigia Kikwete kura kwa sababu ya imani waliyokuwa nayo kwake, mwaka huu atapimwa kwa utendaji wake katika kipindi cha kwanza cha ngwe yake.

“Mwaka huu ni tofauti. Wananchi watakuwa wakimuuliza, kila atakapokwenda wakati wa kampeni, ‘mzee hapa ulituahidi lambo, barabara, shule, mbona hatujapata?’

“Uchaguzi uliopita ilikuwa rahisi kwa Kikwete kwa vile alichotakiwa kufanya ni kuahidi tu. Lakini mwaka huu, wananchi watataka matokeo ya kile alichoahidi,” ameeleza Merenciana Kuboja wa mtaa wa Kasaba, Mwananyamala, Dar es Salaam.

Katika kampeni za kuwania urais mwaka 2005, Kikwete alitoa zaidi ya ahadi 300 nchini kote.

Hatua ya CCM kutangaza matumizi makubwa kumekuja kama kejeli kwa vyama vingine vya siasa ambavyo wiki iliyopita vilipendekeza matumizi ya uchaguzi wa mgombe urais kuwa Sh. 5 bilioni.

Lakini Msajili wa vyama vya siasa John Tendwa aliliweka wazi pale aliposema “vyama visivyo na fedha visione wivu kwa vile vyenye uwezo wa kukusanya fedha nyingi.”

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kiwango cha chini kwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu kinatakiwa kuwa Sh. bilioni moja.

Kwa nafasi ya ubunge, ofisi hiyo inapendekeza kiasi cha kuanzia Sh. 10 hadi 40 milioni kulingana na ukubwa wa jimbo, idadi ya wakazi na miundombinu.

Mapendekezo hayo yanatokana na Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa kwa mbwembwe na Rais Kikwete hivi karibuni na inatarajiwa kuanza kutumika wakati wa mchakato wa uchaguzi mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: