Kikwete haendi mahakamani


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete hataitwa mahakamani katika kesi inayomkabili mwanadiplomasia, Profesa Costa Mahalu, MwanaHALISI limeelezwa.

“Sisi kwa upande wetu hatumuhitaji. Hatutamwita,” ameeleza wakili Mabere Marando anayemtetea Prof. Mahalu.

Amesema waliyemtaka ni rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye tayari alitoa ushahidi wake juzi Jumatatu.

Prof. Mahalu anakabiliwa na mashitaka ya kufanya udanganyifu katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania jijini Rome, Italia.

Kesi hiyo pia inamkabili Meneja wa Utumishi na Utawala wa Ubalozi wakati huo, Grace Martin ambaye alitarajiwa kuanza utetezi wake jana.

Juzi Mkapa aliingia mahakamani Kisutu, jijini Dar es Salaam ambako mbele ya Hakimu Mfawidhi Ilvin Mgeta, alimtetea Mahalu akisema ni yeye (Mkapa) aliyeidhinisha ununuzi wa jengo hilo na kwamba utaratibu ulifuatwa.

Gazeti hili lilitaka kujua iwapo baada ya Mkapa kutoa ushahidi, ilikuwa zamu ya Rais Kikwete kutoa ushahidi upande wa utetezi kwa vile wakati jengo linanunuliwa, ndiye alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

Wakili Marando amesema ushahidi wa Kikwete katika nukuu za bunge (hansard) ambao uliishawasilishwa mahakamani, unatosha.

“Hatujamwita. Hatujapanga kumwita. Hatuna sababu ya kumwita. Hata kama atahitajika, halazimishwi kuja mahakamani kwa sababu ni rais. Sheria inakataza,” Marando amefafanua kwa ufupi kwa njia ya simu ya mkononi.

Ushahidi wa Mkapa ulijikita katika hati yake ya kiapo ya 31 Machi 2011 ambamo alieleza kuwa kila alichofanya Prof. Mahalu katika ununuzi wa jengo hilo, kilikuwa halali.

Alisema mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo ulifuata “misingi ya sheria” na kwamba ununuzi “ulifanywa kwa maslahi ya taifa.”

Katika ushahidi wake huo, Mkapa alieleza kuwa alipata taarifa kutoka kwa Balozi Prof. Mahalu juu ya ubora wa nyumba, kiwango cha fedha kinachohitajika na namna malipo yalivyopaswa kufanyika.

Mkapa alisema kwamba Prof. Mahalu alitoa taarifa kuwa mwenye nyumba aliweka masharti juu ya kulipwa fedha zake; akitaka malipo yafanyike kwenye akaunti mbili tofauti.

Alieleza mahakama kuwa aliridhia masharti hayo kwa kutoa kibali kwa ubalozi na serikali kuyatekeleza masharti alimradi tu waipate nyumba hiyo kwa sababu “ilikuwa bora.”

Alipohojiwa na wakili wa serikali iwapo masharti ya kulipwa katika akaunti mbili tofauti yalilenga kukwepa kodi, Mkapa alijibu, “Hilo litakuwa ni suala la serikali ya Italia na raia wao. Mimi nilichotaka ni nyumba. Alhamdulillah tuliipata.”

Mkapa alieleza kuwa tangu ununuzi wa jengo hilo ulipofanyika, hajapata manung’uniko wala malalamiko kutoka kwa serikali ya Italia wala kwa muuzaji, kwamba kulikuwa na dosari.

Alipoambiwa na wakili wa serikali kwamba aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Marten Lumbanga hakuwa na taarifa juu ya jengo hilo kununuliwa, Mkapa alijibu kuwa hilo linamshangaza.

Mkapa alidai kama Lumbanga amesema hakufahamu, basi (yeye) anashangazwa na hilo, bali “alipaswa kujua.”

Hati ya kiapo ya Mkapa, ambayo MwanaHALISI pekee ndilo liliiandika katika toleo Na. 239 la 27 Aprili 2011, inasema alielezwa kupitia mchakato wa vyombo vya dola, “nilijulishwa vilivyo kwamba jengo la ubalozi lilinunuliwa kwa dola milioni 3, wakati huo ikiwa ni sawa na Euro 3,098,741.40.”

Mahakamani juzi, Mkapa alieleza kuwa hajui nani aliagiza upelelezi wa ununuzi wa jengo la Italia.

Alipoulizwa iwapo ulifanywa wakati yeye akiwa bado rais wa jamhuri ya Muungano, alijibu, “Sijui.”

“Mimi nilikuja kuona Balozi Mahalu kashtakiwa mwaka 2007 nikiwa tayari nimestaafu… nilithibitisha taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kuwa ni kweli Mahalu ameshtakiwa,” alijibu.

Rais Mkapa alikuwa mkuu wa nchi kuanzia 1995 hadi 2005. Wakati huo, Rais Kikwete alikuwa waziri wa mambo ya nje.

Tarehe 3 Agosti 2004, Kikwete alitoa taarifa bungeni kuwa Tanzania imenunua jengo mjini Rome, Italia na kwamba mchakato mzima ulifuata misingi ya uwazi na taratibu zote zilizotakiwa.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za bunge, Kikwete alisema, “Mheshimiwa Naibu Spika, wizara yangu imenunua jengo la Ubalozi wa Italia, lengo likiwa ni kupunguza gharama za kupanga na kwamba taratibu za sheria ya manunuzi ya umma zilifuatwa….”

Kesi inaendelea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: