Kikwete hana jema alilolifanya?


John Adam's picture

Na John Adam - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

MIAKA mitano ya kwanza ya utawala wa Kikwete ilipofika ukingoni, makala za gazeti la MwanaHALISI zikaanza kumsakama kwa ukali na kejeli za kisiasa.

Kati ya lawama zilizotolewa kwa rais katika gazeti hilo, ni pamoja na kumshambulia waziwazi. Baadhi ya mashambulizi hayo yalilenga familia yake.

Miongoni mwa shutuma zilizoandikwa na gazeti hili kuhusu familia yake, ni kujitokeza katika kampeni za uchaguzi kwa mke wake Mama Salma na mtoto wake, Ridhiwani Kikwete.

Ushiriki huo ulitafisiriwa kuwa ni kugeuza kampeni yake ya kusaka urais kuwa ya kifamilia na sio tena jukumu la chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, ushiriki wa familia yake ulielezwa kuwa ni ufujaji mwingine wa mali ya umma.

Kuna kosa gani kwa mke wa rais, Mama Salma Kikwete kumfanyia kampeni mumewe na CCM kwa jumla?

Kwani mama huyu amejitokeza sana katika kazi za kutumikia umma tokea alipoingia ikulu akiwa na mumewe.

Naamini wapo watakaokubaliana nami kuwa kujituma kwake kiasi hicho, ni jambo ambalo hilijawahi kutokea siku za nyuma kwa wake za marais waliomtangulia.

Amekuwa akisafiri nchi nzima tangu mumewe alipoingia madakani akitoa misaada mbalimbali pale alipoweza kwa kutumia mfuko wake wa msaada wa WAMA.

Hivyo, haingii akilini kutegemea ajifiche wakati wa uchaguzi, lakini ategemewe tena kuanza safari zake za kuwatumikia wananchi baada ya kumalizika uchaguzi.

Hivi kweli mama huyu, ambaye ameonyesha kuwa mstari wa mbele kuwasidia akina mama na wototo, angetegemewa kukaa kimya wakati mumewe akiwa katika kampeni za kurejea madarakani?

Ridhiwani ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Vijana (UV-CCM), alitakiwa akae kimya bila kujitosa kwenye mchakato wa kusaka urais ili baba yake mzazi awaongoze Watanzania kwa kipindi kingine?

Fikra na mtazamo wowote wa kukubaliana na mawazo ya gazeti hili kama ambavyo lilitaka wananchi waamini, dhahiri ni kutaka kupotosha ukweli wa mambo.

Kosa liko wapi hapa kwa familia ambayo imelelewa katika mazingira ya kisiasa, kwa wanafamilia kuingia katika mchakato wa kampeni?

Msongo huu wa mawazo uliojaa jaziba na pengine chuki za kisiasa, kwa maoni yangu ni jambo la hatari kwa taifa.

Swali jingine ambalo nilijiuliza na pengine kupata jibu ambalo halitakubalika kwa wengine, ni kwamba si kweli kwamba safari hii Kikwete hakuhitaji wanamtandao, kutokana na kuingia uchaguzi akiwa rais.

Bali kwa kuangalia yaliyojitokeza katika uchaguzi uliopita, jibu lililonijia ni kwamba kati ya sababu zilizomfanya achukue hatua hiyo, ni kutaka kuepuka kukigawa zaidi chama chake.

Hili ni jambo mojawapo ambalo Kubenea na wengine wakiwa wachambuzi wazuri wa mambo, hususani vita dhidi ya ufisadi, wanatakiwa kuliona na kumsifu Kikwete hata kwa hilo moja jema.

Lakini kwa bahati mbaya halikuwa akilini mwake kama jambo jema lililofanywa na Kikwete ambapo wananchi walitakiwa kulijua.

<p> Mwandishi wa makala hii, &nbsp;amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI.&amp;nbsp; &nbsp;Anapatikana kwa imeili: ukweliniukweli@yahoo.com</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: