Kikwete jitose urais, lakini...


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version

SASA imethibitika kwamba Rais Jakaya Kikwete atagombea tena ngwe ya pili ya urais. Pamoja na kuwapo sababu 51 za msingi zinatosha kutokugombea tena, lakini bado Kikwete atataka kugombea tena kama alivyonukuliwa wiki iliyopita.

Alipogombea mwaka 2005, Kikwete alisema alikuwa na sababu lukuki za kufanya hivyo: Kwanza, alitaka kutimiza azma yake aliyokuwa nayo mwaka 1995 alipogombea kwa mara ya kwanza, lakini akashindwa na Benjamin Mkapa katika mchujo ndani ya chama chake.

Kauli mbiu yake katika uchaguzi uliopita, ilikuwa ni “Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania.” Tukamuamini.

Safari hii mazingira ya kisiasa nchini ni tofauti na kwamba Watanzania wanamfahamu zaidi kuliko alivyokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje.

Mazingira ya nchi nayo ni tofauti; vipimo vya kisayansi vyaweza kuangaliwa kujua jinsi gani rais Kikwete kama anakubalika zaidi na anapaswa kugombea tena. Vyovyote vile, Kikwete kama mwanasiasa mwingine hawezi kupoteza nafasi hii na kukubali kuwa Rais wa awamu moja.

Kutokana na mlolongo wa sababu mbalimbali, kutoka zile nzuri, zenye mashaka na hata zile ambazo ni mbaya na za kutisha, bado Kikwete hawezi kuacha kugombea.

Ni jukumu la kwanza la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho Kikwete anatoka kupima uzito wa sababu zitakazomfanya Kikwete kugombea, kabla ya wananchi kuamua kwenye sanduku la kura.

Kuna sababu nyingi ambazo zinamfanya Kikwete ajitose tena kugombea kipindi cha pili.

Kwanza, ni utamaduni wa kuwa na vipindi viwili. Katiba yetu haitoi nafasi ya uongozi kwa miaka kumi mfululizo; bali inatoa nafasi kwa rais kutawala vipindi viwili tu, bila kujali kama vipindi hivyo vinafuatana.

Hata hivyo, tangu mabadiliko ya kisiasa nchini yaliyoweka vikomo vya urais, watangulizi wote wa Kikwete wamekaa madarakani kwa vipindi viwili.

Hiki ndicho ndani ya CCM wanaita, “utamaduni wa kuachiana vipindi viwili.” Ndani ya CCM hata kama rais anayemaliza muda wake anaboronga, bado atapewa kipindi cha pili.

Hivyo basi, rais Kikwete atapewa awamu ya pili na kama tumesikia kelele za watetezi wa dhana hii potofu kuwa ni haramu kwa mwana CCM mwingine kujitokeza kumpinga Kikwete.

Mbili, Kikwete atataka kugombea ili kupata nafasi ya kukamilisha aliyoshindwa kuyatenda katika kipindi cha kwanza. Ni moja ya sababu kubwa ya wapambe wake ya kutaka kugombea tena.

Katika kujiuza tutasikia sana maneno haya “kipindi cha kwanza tulianza…” na kuwa katika kipindi cha pili “tunakusudia kukamilisha..” Hata kampeni yake itajikita katika kuonesha “mafanikio yaliyofikiwa” katika awamu yake ya kwanza na kuwa tukimpa nafasi ya pili atajitahidi “kukamilisha.”

Katika siasa hiki naweza kukiita ni “mnyororo wa kupokezana kushindwa;” yaani huyu anashindwa na akifika mwisho anampa mwingine ambaye naye atajitahidi kushindwa miaka nenda rudi.

Ninafahamu katika kupokezana huku watapokezana vile vile na yale ambayo watayaita ni mafanikio ambayo kimsingi itakuwa ni “idadi” ya kuongezeka vitu mbalimbali.

Tatu, Kikwete atagombea tena ili kukamilisha miradi yake binafsi hasa baada ya kuvunjwa kwa Azimio la Arusha. Kama alivyofanya Benjamin Mkapa katika awamu yake ya pili, binafsi natarajia Kikwete atatumia ngwe yake ya pili kukamilisha miradi yake binafsi ili kujitajirisha yeye na familia yake.

Kama Mkapa alivyoweza kutengenezea mazingira ya kutumia nafasi yake kuanza ujasiriamali pamoja na familia yake, kiasi cha kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya, ndivyo hivyo hivyo Kikwete atarajiwe atafanya yale yale.

Ingawa tayari Kikwete amesema hataki kuingia katika biashara, lakini kule kuwa karibu na wafanyabiashara kunatosha kumfanya kuwa mfanyabiashara.

Alipoingia madarakani hatujui aliingia akiwa na mali kiasi gani. Kikwete hakuweka hadharani mali yake au kama angekuwa na ujasiri kutaka fomu yake ya kutangaza mali kwa Tume ya Maadili iwekwa hadharani ili wananchi wajue rais wao mpya anaingia madarakani akiwa na mali ya kiasi gani.

Nina uhakika wa asilimia mia moja anapomaliza ngwe hii hatotangaza mali yake na ya familia yake ya karibu kwani watu wanaweza kukimbia.

Nne, atasema anagombea ili kupata fursa ya kusahihisha makosa ya ngwe ya kwanza. Sababu hii inategemea kama Kikwete anatambua kuwa kuna makosa yamefanyika chini yake.

Hadi sasa ni vigumu sana kwa rais Kikwete kukubali makosa ya kiuongozi au ya binafsi. Kuanzia suala la mkataba wa Buzwagi, sakata la Richmond, Dowans na mengineyo, kuna makosa mengi ambayo mtu mwingine anaweza kuyaona.

Yapo makosa ya kimaono, makosa ya kimkakati, makosa ya uzembe na makosa ya kiutendaji ambayo yanahitaji masahihisho.

Lakini kwa mtu ambaye anaweza kumwambia amekosea, ni vigumu kwa rais Kikwete kujua makosa yoyote ya kwake binafsi au ya viongozi ambao yeye ni mkuu wao.

Hata hivyo, sitoshangaa kama anaweza akakaa na kufikiria uongozi wake miaka hii mitano ya kwanza na akaona mapungufu yake na makosa yake. Akiwa mkweli kwa nafsi yake na kwa taifa lake anaweza akaamua kugombea ili kusahihisha makosa.

Hii litategemea kama Kikwete amekubali kwanza kuona makosa. Sitarajii Kikwete kufanya hivyo. Kwake kukiri makosa, ni udhaifu na chama chake hakiwezi kukubali akiri udhaifu wa aina hiyo.

Tano, atagombea ili kutafuta historia atakayowaachia Watanzania. Tangu Mwalimu Julius Nyerere hakuna rais aliyeingia madarakani nchini akiwa amebeba matumaini ya mioyo ya Watanzania kama ilivyokuwa rais Kikwete.

Ushindi wake wa asilimia 80 katika mfumo wa vyama vingi ni ushahidi wa wazi wa jinsi gani alivyokuwa amekubalika. Miaka mitano inayoisha imetufunulia yeye ni kiongozi wa namna gani.

Wataalamu mbalimbali wanatabiri kuwa mwaka huu hawezi kushinda kwa asilimia 80 tena au zaidi. Binafsi naamini kama hakutatokea mabadiliko makubwa ya kisiasa na hali ikawa kama ilivyo sasa, basi rais Kikwete anaweza kushinda kwa kati ya asilimia 60 na 70. Nilitabiri kwa usahihi sana kuwa Kikwete angeshinda kwa asilimia 80 alipogombea mara ya kwanza.

Kikwete atataka kuachia Watanzania kitu cha kukumbuka. Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alituachia “ruksa” japo siku za karibuni ameanza kukana baadhi ya matunda yake.

Mkapa kwa upande wake, alituachia matumizi mabaya kabisa ya madaraka nchini na uwanja wa mpira! Kama naweza kutabiri vyema, Rais Kikwete anaweza kuliacha taifa mikononi mwa wawekezaji.

Kikwete ni muumini mno wa dini ya uwekezaji ambapo Watanzania tunatakiwa kuabudu kwa hoja kwamba pasipo hao hatuwezi kuuona ufalme wa mbinguni.

Wakati Mwalimu Nyerere aliamini katika kujitegemea kifikra na kiutendaji, rais Kikwete haamini kama Watanzania wanaweza kujitegemea isipokuwa kwa uwekezaji kutoka nje.

Atakapoondoka madarakani, tusishangae kukuta tuna wawekezaji wa kuuza hadi ndala, samaki, na mitumba wametapakaa nchi mzima!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: