Kikwete kataa kuwalipa kina Rostam


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 23 February 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Suleiman Al Adawi

WAHUSIKA wawili wakuu katika sakata la mkataba tata wa kufua umeme wa dharula kati ya shirika la umeme la taifa (TANESCO) na kampuni ya Dowans – Suleiman Al Adawi na Rostam Aziz ambao mara kadhaa wamekana kufahamu lolote juu ya kampuni hiyo, sasa wamejitokeza hadharani na kujitambulisha kuwa ndio wamiliki halisi wa Dowans.

Jumapili iliyopita, Al Adawi akisindikizwa na Henry Surtees, Mtunza Fedha wa kampuni ya Caspian (inayomilikiwa na Rostam Aziz), walijitokeza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza dhamira ya kampuni yao kuhakikisha majenereta yake yanatumika vyovyote iwavyo, na wanalipwa fedha zao.

Novemba 15 mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) iliamuru TANESCO kuilipa kampuni hiyo, Sh. 94 bilioni kutokana na kile kilichoitwa, “hatua ya TANESCO kuvunja mkataba.”

Sasa swali la kujiuliza: Kwa nini Al-Adawi amejitokeza sasa, wakati tayari amekana mara kadhaa kuifahamu kampuni hiyo? Kwa nini tunalishwa maneno kwamba Dowans ndiye mwokozi na serikali lazima inunue majenereta hayo kama inataka kujiokoa?

Kinyume na inavyoelezwa, Dowans haikurithi mkataba halali kutoka kwa dada yake Richmond Development Company (LLC). Hukumu ya ICC ambayo imeiamuru serikali kulipa kampuni hiyo, ilifikiwa wakati mahakama hiyo ikinyimwa taarifa muhimu kuhusu kesi hiyo.

Ni kwa sababu, mmiliki wa Dowans aliaminishwa na watawala kuwa ‘dili hili’ lingefanyika kiulaini. Mwenyewe amekiri hili katika maelezo yake na waandishi wa habari. Ambacho hakuulizwa, ni nani aliyemhakikishia hilo?

Lakini kuingia kwa kampuni yake mithili ya kimbunga katika mradi huu mara baada ya kampuni ya Richmond kushindwa kuleta majenerata ya kuzalisha umeme, ndiko kulikosukuma Dowans ambayo tayari ilikuwa imetinga nchini na kumpa Rostam Aziz nguvu ya kisheria 28 Novemba 2005, kujitosa katika mradi huu.

Kwa sababu, endapo watapatikana viongozi jasiri ndani ya Tanzania na kusema kuwa Dowans hailipwi Bw. Al Adawi atakuwa amepata hasara kubwa sana (kwani aliwekeza fedha yake nyingi kwenye kununua mitambo hiyo) na inaweza kuvuruga kabisa urafiki wake na Rostam Aziz na Rais Kikwete.

Hivyo, wanajikuta wamebakia na hoja ya kujaribu kupunguza tuzo halafu wakati huo huo mkataba mwingine uingiwe. Mpango huu utapata watetezi wengi na wengine watazungumza kana kwamba wanatoa hoja za kisomi.

Watasema “tuingie mkataba na Dowans” kwa muda ili tunusuru taifa na adha ya umeme.

Mojawapo ya hoja za ajabu kabisa ni hii inayotolewa na kuvutiwa kwa maneno ya “kizalendo” yenye kugusa vionjo. Kwamba Watanzania wamechoka na tatizo la umeme na hawataki kuendelea “kuteseka” wakati mitambo imekaa tu pale Ubungo. Kwamba mitambo iwashwe ili “kunusuru taifa” na hatimaye tutaweza kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo nchini.

Tukikubali hoja hii ni lazima tujiulize; mbona Nyerere alikuwa timamu pale alipokataa kufanya biashara na Afrika Kusini wakati wananchi wake walikuwa maskini na wanateseka?

Tungeweza kununua vitu mbalimbali kutoka nchini humo kuliko kununua kutoka Ulaya; tungeweza kupeleka wananchi wetu kusoma Afrika ya Kusini kuliko kuwapeleka China au Ujerumani! Kwanini Nyerere pamoja na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika zilikataa kufanya biashara na Afrika ya Kusini?

Nyerere aliandika katika gazeti la The Observer la London (Uingereza) tarehe 7 Machi, 1961. Makala yake ndiyo ilichangia kwa kiasi kikubwa kushawishi nchi za Jumuiya ya Madola kuiwekea ngumu Afrika ya Kusini kujiunga nao na kulazimisha Afrika ya Kusini kujitoa.

Nyerere alisema,  “Ili tuweze kujenga jamii nzuri katika nchi yetu ni lazima basi tueleze kutokupendezwa kwetu na mfumo wa Afrika ya Kusini katika matendo yetu yote.

“Serikali ya Tanganyika haiwezi kuwa na uhusiano wowote na Serikali ya Africa ya Kusini, na ni lazima – tukizingatia sheria za kimataifa – kuunga mkono wale wote wanaopambana kupinga mfumo wa kibaguzi.

Ni kwa sababu hizo basi, sisi kama serikali tayari tunaunga mkono kutogombea bidhaa za Afrika ya Kusini, na tumesitisha mikataba ya kutafuta ajira licha ya gharama kubwa ya kiuchumi katika eneo letu ambalo tayari ni maskini sana kiuchumi”.

Huo ulikuwa msimamo wa kiuongozi. Nyerere alitambua na wananchi walimwelewa kuwa ni bora kuvumilia shida kidogo kuliko kukumbatia uovu.

Tatizo la nishati nchini mwetu si la vyanzo vya nishati, ni la “kupungua maji bwawa la Mtera.”

Tatizo letu la nishati ni tatizo la kiuongozi lililoletwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Inawezekana vipi CCM na serikali yake wakaacha mitambo na mabwaya ya maji kufanya kazi chini ya uwezo wake?

Wanataka tuamini tatizo ni mvua, wakati ukweli ni kwamba mitambo mingi kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ya Hale, Nyumba ya Mungu, Mtera, Kidatu na Kihansi ni chakavu na serikali kwa karibu miaka arobaini sasa imeshindwa kuitengeneza na kuiboresha kwa kiwango stahili.

Hata kule ambako matengenezo yamefanyika, kama  Kidatu, hayakufanyika kwa kiwango kinachostahili. Matokeo yake, taarifa zinasema kurejesha mabwawa hayo katika kiwango chake cha juu cha uzalishaji, kunahitajika karibu dola za Marekani 2 bilioni (Sh. 3 trilioni).

Swali ambalo linabakia ni je kuna namna yoyote ya kutatua tatizo la nishati bila kuwalipa Dowans wala kuyawasha majenereta yao? Je, inawezekana kuwaelewesha wannachi kuwa serikali imeamua kulitatua tatizo hili bila kuwapigia magoti Dowans?

Tukiwauliza ‘wao’ watasema haiwezekani – kwani wanataka mitambo ya Dowans iwashwe kwa lazima! Rais Jakaya Kikwete akitaka anaweza kutumia nguvu alizonazo kikatiba na kisheria kuingilia tatizo hili la nishati na kuhakikisha ifikapo Juni 2011, taifa hili linapata suluhisho la muda juu ya tatizo la umeme wakati serikali inaanza kushughulikia ujenzi wa Stielgers Gorge kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya uchaguzi ya chama chake.

Swali linalobakia ni je, Rais Kikwete ana ujasiri wa kutekeleza kile alichoahidi? Je, Kikwete yuko tayari kuwakatalia marafiki zake?

Kama rais hawezi, nani ataweza kumsaidia kuwaambia Rostam na Al Adawi “fungasheni majenereta yenu,” kwani Watanzania wako tayari kuvumilia miezi michache ya matatizo  ili suluhisho bora zaidi na la haki lipatikane?

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: