Kikwete, katiba na mafisadi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 February 2012

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

KATIKA hotuba yake ya kuadhimisha miaka 35 ya kuzaliwa kwa chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumapili iliyopita, mjini Mwanza, Rais Jakaya Kikwete alisema mengi.

Kubwa ambalo wengi watalikumbuka, ni hatua yake ya kukana ukweli huku na kuukubali kule.

Kwa mfano, Kikwete ambaye pia ndiye mwenyekiti wa chama hicho alisema, “Sisi tunayo ajenda yetu. Tunazo ahadi zetu; na yote ambayo tunatekeleza yametokana na yale tuliyoahidi.” Aliwataka wenzake wasikubali kuhama kwenye mstari.

Lakini nani asiyefahamu kuwa chama hiki tayari kimepoteza mwelekeo? Angalia kilivyobeba hoja ya kuwapo kwa katiba mpya; hoja ambayo haijawahi kuwa ya chama cha Kikwete.

Kwa miaka yote hii, CCM kimekuwa kikieleza kuridhika na katiba iliyopo na kilisisitiza mara kadhaa, kwamba “katiba iliyopo inajitosheleza.”

Mara kadhaa, chama cha Kikwete na baadhi ya viongozi wake walisikika wakiutangazia ulimwengu kuwa “mjadala wa katiba mpya umefungwa,” na kusisitiza, “Suala la katiba mpya haliko kwenye ilani ya CCM.”

Ndiyo maana kote alikopita Kikwete, hakuwahi kusema kuwa anakubaliana na hoja ya kuwa na katiba mpya. Hakusema anakubaliana na matakwa ya kuandika katiba mpya.

Je, pale Mwanza Kikwete alikuwa anamdanganya nani kuwa chama chake kinatekeleza yale ambayo yako kwenye mipango yake, sera zake na ilani yake?

Ujio wa katiba mpya umesukumwa na sauti kuu ya kiongozi wa upinzani nchini, Dk. Willibrod Slaa, katibu mkuu wa Chama cha Demekrasia na Maendeleo (CHADEMA), aliyekuwa mshindani mkuu wa Kikwete kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005.

Bali katika hotuba yake ya kuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2011, Kikwete alinukuliwa akikubali kuwa “…sasa taifa linahitaji katiba mpya. Ninaona kuwa atakiri sana, kwani mchakato wenyewe wa kupata katiba bado haujaanza.

Wakati angalau rais akionyesha msimamo moto-baridi, baadhi ya viongozi ndani ya serikali na chama chake wamekuwa wapinzani wakuu wa hoja hii; ama kwa kujua msimamo wake au kwa kutokuwa na uhakika wa kile anachotaka.

Wengi wa viongozi wake wateule hawajakubali kuwa katiba iliyopo haifai na hivyo inahitaji kuandikwa upya.

Ushahidi wa hili, ni hatua ya wabunge wake kutaka kukwamisha muswaada wa “Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, Na. 8 ya mwaka 2012.”

Pamoja na kwamba hili halimo kwenye mipango ya chama chake, sera na ilani yake ya uchaguzi, Kikwete ameonyesha kulibeba au hata tukisema kulishabikia. Kulikataa ni kujitosa kisiasa.

Hata mapendekezo ya CHADEMA ambayo yamemchota rais na kumuibua juu ya hoja hafifu za wahafidhina, bado zinaungwa mkono na wanachama wengine wa CCM ambao wana msimamo wa kimaendeleo na usio wa kimaslahi.

Kwa mfano, kifungu cha 6 (1) cha sheria hiyo sasa kinataka rais kuteua wajumbe kutoka miongoni mwa majina atakayopelekewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na vyama vya kitaaluma, kuwa wajumbe wa Tume ya Katiba.

Awali kifungu hicho kilitaka rais kuteua yeyote anayeona anafaa hata kama huko anakotoka wanaona hawezi kuwa mwakilishi wao.

Aidha, ndani ya sheria Na. 8 ya muswaada wa mabadiliko ya katiba, kumeongezwa kifungu cha 17 (10) kinachoruhusu watu binafsi, taasisi za kidini na vyama vya hiari, kutoa elimu ya uraia. Je, kifungu hiki kina ubaya gani kwa CCM?

Vilevile, mapendekezo yameondoa wakuu wa wilaya kuwa miongoni mwa wajumbe muhimu wa kusaidia kuitishwa kwa mikutano ya tume ya katiba, kuruhusu nani aitishe mkutano na nani azuiwe; yupi aende hapa na yupi aende pale.

Rais amekubali kuondokana na urasimu huo. Ametaka kazi ya kukusanya maoni ifanywe na tume yenyewe. Je, katika mazingira haya, CCM itakuwa bado inatamani kutaka kuendelea kutawala wakati inachokitenda ni kwa maslahi binafsi?

Bali Kikwete amekiri kuwa ikiwa CCM inataka kuendelea kushika dola, sharti ijibadilishe kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuongozi.

Anataka CCM iwe sikivu na makini; itende vile ambavyo wananchi wanataka. Amewataka viongozi wake wasimame kwenye maslahi ya taifa badala ya kuweka mbele maslahi binafsi.

Inawezekana kwa kulijua hilo, ndiyo maana ameanza yeye kuwa msikivu kwa kukubali kusikiliza kilio cha umma. Amekubali kusikiliza hoja za vyama vya upinzani, viongozi wa kidini, asasi za kiraia na wananchi wengine.

Hatimaye akakubali kupelekwa bungeni marekebisho makubwa ya sheria ya muswaada wa mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011.

Sikufikiria hata mara moja, kuona wabunge wa CCM wakimsaliti mwenyekiti wao. Hii ni kwa sababu, 23 Novemba 2011, chama ambacho wabunge hawa wamepitia, kilibariki hatua ya mwenyekiti wao kukubali kujadiliana na CHADEMA jinsi ya kupata katiba mpya.

Mkutano wa CHADEMA na Kikwete na ambao ulibarikiwa na CCM, ulifanyika wiki mbili baada ya chama hicho kususia mkutano wa Bunge kwa hoja kuwa, “serikali inauburuza.”

Tena kauli ya chama haikutolewa barabarani. Ilitoka ndani ya vikao halali vya chama – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC). Uongozi wa chama ulisema umepokea kwa furaha kubwa hatua ya mwenyekiti wao, kukubali kukutana na CHADEMA.

Baadhi ya wabunge ambao wamenukuliwa sasa wakipinga marekebisho ya muswada, ni wajumbe wa vikao hivi. Je, katika mazingira haya, nani anaweza kuamini kuwa CCM bado ni chama kimoja?

Jakaya Mrisho Kikwete amesikika akisema chama chake bado kiko imara. Hakijayumba na kinafahamu kinachokitenda.

Uko wapi uimara wa CCM wakati baadhi ya wabunge wake wanamtukana hadharani mwenyekiti wao? Kama chama kingekuwa imara, nani angesimama kupingana na mwenyekiti? Nani angeweza kusema, “tutapiga kura ya kutokuwa na imani na Kikwete?” Ushupavu huo angeutoa wapi?

Chama imara hakiwezi kuchezewa na wabunge wake. Chama imara hakiwezi kukubali kuyumbishwa na wanachama wake, hasa viongozi ambao walishiriki kwenye kikao cha kupitisha maamuzi na baadaye wanaibuka na kumkana mwenyekiti wao.

Wala chama imara hakiwezi kunyamazia mwenyekiti wake akidhalilishwa na wale aliowapigania kufika hapo walipo.

Ni pale tu, chama kinapokuwa legelege; ndipo kinapobeba hata wasiobebeka; kinaporuhusu hata asiye na sifa kuwa kiongozi na kinapogeuka kuwa genge la wahuni, badala ya kuwa chama kinachoongoza kwa kufuata dira na maslahi ya taifa.

Angalia mfano huu. Ndani ya Bunge la sasa, CCM ina idadi kubwa ya wabunge ukilinganisha na upinzani. Lakini angalia michango yao. Sikiliza hoja zao. Pamoja na wingi wao, wanaburuzwa kwa kila hoja na wabunge wa upinzani.

Ni kwa sababu hii, uchaguzi wa kupata wagombea ubunge ndani ya chama hicho, ulijaza hata wale wasiostahili. Baadhi ya wabunge wake baadala ya kusimamia hoja, wanaishia kupiga vijembe, mithili ya waimbaji wa taarabu. Tuondoke hapo.

Jakaya Mrisho Kikwete amesema kiongozi wa CCM sharti afanane na wale anaowaongoza. Ametaka wote wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali, zikiwamo tuhuma za ufisadi, wasipitishwe kuwania uongozi kwenye uchaguzi ujao.

Lakini nani aliyepitisha watuhumiwa wa ufisadi kwenye vikao vya juu vya CCM? Nani aliyesafiri hadi kwenye majimbo yao ya uchaguzi kuwaombea kura? Nani aliyehakikisha wanabebwa kwa gharama yeyote na kuwajaza ndani ya Bunge wanaowatuhumu ufisadi? Bila shaka, ni Jakaya Kikwete.

Baadhi ya wale ambao Kikwete anataka chama chake kisiwapitishe, ndiyo washauri wakuu wa serikali katika uundaji wa sheria.

Andrew Chenge, mmoja wa wanaoitwa na chama hicho kuwa gamba, ameonekana kwenye picha za televisheni wiki iliyopita, akishauri mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji Frederick Mwita Werema, kuhusu muswada wa sheria ya usafirishaji fedha haramu.

Chenge alijitosa kushauri serikali baada ya John Mnyika, mbunge wa Ubungo (CHADEMA), kupendekeza adhabu ya matumizi ya fedha haramu kuongezwa; kutoka kifungo kisichozidi miaka mitatu au faini ya kati ya Sh.100 milioni hadi Sh. 500 milioni ili iendane na kiwango cha fedha au majengo ambayo mtuhumiwa amekutwa nayo.

Nani anaweza kuamini kuwa Chenge alikuwa anatetea maslahi ya taifa au chama chake? Iko wapi taswira ya Chenge mbele ya jamii inayoweza kuisaidia CCM kuonekana imepata mtetezi?

Hatua ya Chenge kuonekana bungeni, tena akimnong’oneza mwanasheria mkuu wa serikali na kisha mwanasheria mkuu akapinga hoja ya kuongezwa adhabu kwa watu ambao watapatikana na hatia ya makosa ya fedha haramu, ni kielelezo kingine kuwa CCM imetota.

Kikwete anafahamu au anapaswa kufahamu kuwa chama chake kimejaa mafisadi. Kinaendeshwa na watuhumiwa wa ufisadi. Hata sherehe za kuadhimisha miaka 35 ya kuzaliwa kwake, baadhi ya waliokichangia, ni watuhumiwa wa ufisadi.

Hivyo basi, kuhubiri kuwa wanaotuhumiwa ufisadi wasipitishwe kuwania uongozi, ni sawa na kutamani kuishi peponi, wakati bado uko hai. Kama yeye ameshindwa kufukuza wanaotuhumiwa ufisadi – Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz – nani anataka amfunge paka kengele?

Akiongea kwa ukakamavu, Kikwete alisema, “Ni muhimu CCM ikaongozwa na watu wenye uwezo wa kutusemea na kusikilizwa.” Akaonya, “Kukubaliana na wanaotata tubaki kama tulivyo, kutatupeleka kubaya.”

Amesema kazi ya kukisafisha chama kwa kuondokana na wale wanaokipa chama hicho taswira mbaya mbele ya jamii, iwe kazi ya kudumu; isiwe kazi ya matukio.

Wako wapi wenye uwezo wa kukitetea chama na kukipigania, wakati rushwa ndiyo nguzo kuu ya kupatikana viongozi? Wako wapi wanaoweza kukipigania chama, ikiwa uongozi ndani ya chama unanadiwa mithili ya bidhaa sokoni?

Hata katika sherehe hizo za miaka 35, Kikwete ameshindwa kuonyesha umma namna ambavyo chama chake kimejipanga kushughulikia masuala ambayo aliyatolea kauli mwaka jana mjini Dodoma .

Kwa mfano, Kikwete hakueleza uhusiano wake na kampuni ya Dowans ambayo katika hotuba yake ya 5 Februari 2011, alikana kuifahamu.

Hakusema kile ambacho Lowassa alikieleza ndani ya mkutano wa NEC; kwamba kila alichokitenda kilikuwa na baraka zake.

Kama Kikwete angesimama mjini Mwanza na kutangaza kuendesha operesheni ya kuondoa wanaowaita mafisadi ndani ya chama chake kwa vitendo, badala ya maneno; kwa kuanza kuwafukuza uongozi palepale, hata kama asingejibu kauli ya Lowassa angalau angeeleweka.

Nje ya hapo, Kikwete atakuwa ameruhusu mkokoteni kuvuta punda, badala ya punda kuvuta mkokoteni. Asikubali kufikishwa huko.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: