Kikwete na Katiba Mpya: Mkokoteni mbele ya Punda


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KATIKA hotuba yake ya kuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2011 Rais Jakaya Kikwete amesema mengi.

Lakini kubwa ambalo wengi watalikumbuka, ni kukubali kuwa katiba iliyopo, haifai na sasa taifa linahitaji katiba mpya.

Nampongeza rais kwa kutambua ulazima huu wa kihistoria, hasa kwa vile baadhi ya viongozi ndani ya serikali yake wamekuwa wapinzani wakuu wa hoja hii.

Hata hivyo, kabla ya rais kutoa kauli hiyo, nilitarajia angekaa na chama chake ili kwanza waweze kubadili sera ili ziendane na wazo la katiba mpya.

Kutoka hapo washirikishe vyama na wadau wengine kuweka utaratibu wa kuiandika katiba hiyo.

Sikufikiria hata mara moja, kwamba Kikwete ataunda “Tume ya Kupitia Katiba” bila kushirikisha chama chake.

Ni kwa sababu, hoja ya katiba mpya haijawahi kuwa hoja ya chama cha Kikwete. Kwa miaka yote hii, CCM imekuwa ikieleza kuridhika na katiba iliyopo na ilisisitiza mara kadhaa, kwamba kama kuna tatizo lolote, basi linaweza kufanyiwa mabadiliko.

Mwaka 2007 aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Sera), Kingunge Ngombare Mwiru aliutangazia ulimwengu kuwa “mjadala wa Katiba mpya umefungwa,” na kusisitiza, “Suala la katiba mpya haliko kwenye ilani ya CCM.”

Kutoka wakati ule hadi majuzi, karibu viongozi wote wa chama hicho wamekuwa wakieleza kuwa “katiba iliyopo inajitosheleza.”

Naye Jaji Frederick Werema, mwanasheria mkuu wa serikali alihitimisha mjadala huo kwa kusema,  “Serikali iko tayari kufanyia mabadiliko katiba, lakini haiko tayari kuandika katiba mpya.”

Kauli ya Werema aliitioa ikulu Dar es Salaam wakati wa kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohammed Chande.

Kati ya Kingunge na Werema kumekuwepo na wingu la viongozi wa serikali ambao walikuwa wamechukua msimamo wa kupinga katiba mpya na wengine kuunga mkono.

Matokeo yake CCM imejikuta imegawanyika katika makundi mawili.

Wala hakuna ubishi kuwa uamuzi wa Kikwete kukumbatia hoja ya katiba mpya haujatafakariwa vya kutosha serikalini na kama imefanyika si zaidi ya siku nne!

Ni kwa sababu, 27 Desemba 2010, Jaji Werema ametangaza hakuna katiba mpya, lakini 31 Desemba 2010, rais anasema anaunda kamati kuratibu kazi ya kuandikwa kwa katiba mpya.

Lakini ukiondoa hilo, kuna hili pia: Tume ya Kupitia Katiba si ya lazima, na kwamba rais ameenda nje ya madaraka ya chama chake.

Katiba ya CCM Ibara ya 105:1 inasema kazi za Mkutano Mkuu wa CCM ya kwanza kabisa ni “Kupanga Siasa ya CCM na kusimamia utekelezaji wa shughuli zake.”

Kwa maneno mengine, mkutano mkuu ndiyo unaoweza kubadilisha siasa za chama na kwamba unaweza kukasimu madaraka yake kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Siasa ya CCM “Katiba iliyopo inatosha” na kwamba hakuna wakati wowote ambapo chama hicho kimetoa msimamo tofauti.

Hivyo basi, uamuzi wa sasa wa kutaka kuandikwa katiba mpya ni uamuzi binafsi wa rais mwenyewe. Siyo uamuzi wa CCM. Labda kama vikao vya chama hicho vimepoteza maana katika siku za karibuni.

Binafsi wala nisingekuwa na tatizo kama baada ya kuzidiwa na hoja juu ya katiba mpya, CCM ingeamua kuitisha mkutano au kikao chenye madaraka hayo na kuja na msimamo wa kukubaliana na hoja hiyo.

Lakini kwa uamuzi wake wa kuunda tume kupitia katiba, rais Kikwete atakuwa amefanya mambo mawili. Moja, atakuwa amewazunguka wenzake katika chama na pili atakuwa amewazunguuka wapinzani.

Hivyo, tukikubali pendekezo lake la kuunda tume na kuiacha tume hiyo ifanye kazi jinsi ambavyo rais anataka, tutakuwa tunakubali uporaji wa wazi wa hoja ya katiba mpya.

Kwani, rais atakuwa ameunda tume ambayo yeye ndiye anateua wajumbe, wanawajibika kwake na yeye ndiye anaowapa maagizo ya nini kifanyike.

Kwa mujibu wa mtandao wa CCM – tovuti – tume itakayoundwa itafanya kazi zifuatazo:

“Kuongoza na kuratibu mchakato utakaoshirikisha wananchi wote...kutoa maoni yao juu ya yatakayohusu Katiba ya nchi yao.”

Tovuti ya CCM inasema, “Baada ya kukamilisha kukusanya maoni, Tume itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya kikatiba kwa kufanyiwa uamuzi.”

Hivyo, tume aliyoiunda Rais Kikwete ameipa jukumu la kukusanya maoni tu; si tume ya kupitia uundwaji wa katiba.

Tume haijapewa kazi ya kusimamia mchakato wa kuunda katiba mpya; wala rais Kikwete hajaunda tume ya kusimamia uundwaji wa katiba.

Alichokifanya  ni kuunda tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya. Basi! Ikimaliza kazi yake itatoa “mapendekezo.”

Kwa ufupi hii tume haitapeleka matakwa ya wananchi; bali itaangalia maoni yao na baadaye kutoa “mapendekezo.”

Tume inayoshangaliwa na watu mbalimbali haina nguvu yoyote ya kisheria au kikatiba kupeleka matakwa ya wananchi kwa watawala, isipokuwa kupeleka mapendekezo.

Tatizo la pili kwenye hili ni kuwa mapendekezo haya yatapelekwa kwa “vyombo stahiki vya kikatiba.”

Hivi kuna mtu amejiuliza ni vyombo gani hivi “stahiki” vya kikatiba? Je, yeye kama rais ni chombo mojawapo? Je, mapendekezo haya yatapelekwa bungeni?

Kama ndiyo, kwa nini Bunge ambalo ndiyo mwakilishi halali wa wananchi wasiletewe hoja ya kuunda tume ya kusimamia mchakato huu?

Kwa kadiri tume hii inavyokuwa, ni wazi kwamba Bunge halitakuwa na nguvu ya kusimamia mjadala wa katiba kwani kazi hiyo sasa imetekwa na ikulu.

Tovuti ya CCM inafika mbali zaidi. Inasema, “Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa ianze kutumika.”

Kwa maneno mengine, “Vyombo stahiki vya kikatiba” vikikubaliana na mapendekezo hayo, basi vitatupatia katiba mpya kwa siku itakayoamuliwa kuanza kutumika.

Rais Kikwete hajatuambia ni chombo gani hicho kitakachopokea mapendekezo hayo, na ambacho kitabadili katiba na kupanga tarehe ya katiba hiyo  kuanza kutumika.

Lakini jambo lililojificha hapo ndani ni kuwa rais hajaahidi taifa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 kitu ambacho Dk. Willibrod Slaa aliahidi kukitenda.

Kwa kushindwa kutuahidi katiba mpya kabla ya 2015, Kikwete aweza kuliingiza taifa katika janga ambalo halitaweza kusahaulika.

Ni muhimu akaweka utaratibu wa majukumu ya tume itakayoundwa, muda wa kufanya kazi na akaeleza hicho kinachoitwa, “Vyombo vya maamuzi” ni kitu gani.

Bila kuweka ratiba huo, atakuwa hajawatendea haki wananchi wake. Ni kwa sababu, tume  inaweza kuja hata na mapendekezo ya katiba mpya ianze kutumika mwaka 2020 au 2050. Matokeo yake, nchi kutumbukia katika vurugu.

Kwa maoni ya wengi, katiba mpya ipatikane kabla ya mwaka 2014 ili uchaguzi ujao wa serikali za mitaa ufanyike kupitia katiba mpya.

Katika hili hakuna kurudi nyuma wala kusalimu amri. Tusiruhusu kile ambacho mahafidhina ndani ya CCM wanaita, “Tumpe Rais nafasi”.

Wala suala la katiba mpya si suala la CCM. Limebebewa bendera na wapinzani. Tutakuwa watu wa ajabu tukiamua kuwaaachia CCM  wateke hoja hii na kutupa kile ambacho wao wanataka.

Ni vema rais akaachwa kuteue mwenyekiti wa Tume tu, na Bunge likafanya kazi ya kuteuwa wajumbe wengine wa tume hiyo. Vinginevyo, uwekwe utaratibu ambapo wajumbe watapatikana kwa njia ya usaili badala ya uteuzi ili kuepuka kuwapo mwanya wa kupeana ulaji.

Nje ya hapo, tutakuwa tunaruhusu mkokoteni kuvuta punda, badala ya punda kuvuta mkokoteni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: